Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuhuma za upendeleo, rushwa ajira za walimu zaiibua Serikali

Muktasari:

  • Serikali imejibu tuhuma hizo kutoka kwa umoja unaojiita ‘Neto’ huku ikitaja mchakato wa kuwapata watumishi wapya serikalini.

Dodoma. Wakati ‘Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (Neto)’ ukidai kuna vitendo vya upendeleo na rushwa katika usaili wa nafasi za ajira za kada hiyo, Serikali imesema tuhuma hizo ni upotoshaji.

Msingi wa hoja za umoja huo usio rasmi ambao unadai ni wasomi wa kada hiyo waliokosa ajira tangu mwaka 2015 hadi 2023 ni kutokana na usaili unaoendelea wa nafasi 14,648 za walimu zilizotangazwa na Sekretarieti ya Ajira.

Akijibu tuhuma hizo Februari 19, 2025 kupitia taarifa kwa umma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Sekretarieti ya ajira, Lynn Chawala amesema: “Usaili wa kada ya ualimu kujaza nafasi 14,648 zilizotolewa na Serikali  kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini ulianza Januari 14, 2025 na unatarajiwa kukamilika Februari 24, 2025 Tanzania Bara na Zanzibar.

“Ambapo hadi kufikia Februari 18, 2025, jumla ya walimu 6,055 waliofanya usaili na kufaulu wamepangiwa vituo vya kazi katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kukamilika kwa mchakato wa ajira zao.”

Chawala amesema ili kutekeleza dhana ya uwazi, usaili wa kada za ualimu unasimamiwa kwa ushirikiano wa viongozi kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais (Utumishi), Ofisi ya Rais (Tamisemi), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Utumishi wa Walimu,  Taasisi nyingine za Umma pamoja na Ofisi za Wakuu wa Mikoa kote nchini.

Kuhusu kuwapo kwa upendeleo, taarifa iliyotolewa na Chawala imeeleza kuwa: “Wataalamu wanaohusika na usahihishaji wa mitihani ya usaili pamoja na wale wanaoshiriki kwenye majopo ya usaili wameratibiwa na Katibu wa Sekretareti ya Ajira kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa chini ya uratibu wa Makatibu Tawala wa Mikoa.

“Matokeo ya usaili wa kada za ualimu yamekuwa yakiingizwa kwenye mfumo wa kidigitali wa Ajira Portal baada ya usaili kukamilika kwenye vituo husika katika mikoa yote nchini.”

Chawala ameongeza kuwa wasailiwa waliofanya vizuri katika usaili huo wamepata fursa ya kuajiriwa na waliofaulu na kukosa nafasi katika usaili majina yao yataendelea kuhifadhiwa katika kanzidata ya Sekretarieti ya Ajira kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Hivyo, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inapenda kuwakumbusha wale wote wanaotoa taarifa za kupotosha kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea nchini kote kuacha upotoshaji huo. Vilevile, tunawaomba wadau wote kupuuza upotoshaji huo kwani lengo la utaratibu huu ni kupata nguvu kazi ya walimu wenye uwezo na weledi watakaochangia katika kuifikisha nchi yetu katika malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika nafasi 14,648 zilizotangazwa za ualimu zinazolalamikiwa sasa, walioomba walikuwa 201,707.