Sara, binti aliyepata mimba shuleni anavyofukuzia ndoto ya udaktari

Muktasari:
- Mwaka 2022 akiwa kidato cha pili afya ilizidi kutetereka, ikamlazimu kukatisha masomo ili kupata tiba. Aliporejea shuleni wenzake walikuwa tayari wameshasajiliwa kwa ajili ya mtihani wa Taifa, hivyo alilazimika kurudia kidato cha kwanza.
Dar es Salaam. Tangu utotoni ndoto yake ilikuwa kuwa daktari, kadiri alivyokua shauku ya kuikaribia taaluma hiyo iliongezeka.
Aliamini njia pekee ya kufanikisha ndoto hiyo ni kuongeza juhudi kwenye masomo, jambo alilotekeleza hadi pale alipoanza kusumbuliwa na maradhi.
Mwaka 2022 akiwa kidato cha pili afya ilizidi kutetereka, ikamlazimu kukatisha masomo ili kupata tiba. Aliporejea shuleni wenzake walikuwa tayari wameshasajiliwa kwa ajili ya mtihani wa Taifa, hivyo alilazimika kurudia kidato cha kwanza.
Sara Lusoko, hakukubaliana na uamuzi huo akawaomba wazazi wake wamruhusu akasome katika kituo maalumu aweze kufanya mtihani na kuhitimu kidato cha nne ndani ya miaka miwili, lengo likiwa kufupisha muda wa masomo ili kuendana na matatizo yake ya kiafya.
Bado siha njema haikuwa upande wake, hata akiwa huko aliendelea kusumbuliwa na maradhi akashindwa kuendelea na masomo, akalazimika kukaa nyumbani.
Huo ukawa mwanzo wa anguko la Sara mkazi wa Vwawa mkoani Songwe. Akiwa na miaka 17 akaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi uliomsababishia ujauzito.
“Nilikuwa nyumbani najishughulisha na mambo mengine, ikatokea nikampata mwenzangu tukaanzisha uhusiano haikuchukua muda mrefu nikapata ujauzito. Kwa bahati nzuri alikuwa na shughuli zake za kumuingizia kipato, hivyo hakukataa ujauzito.
“Alikuja nyumbani akazungumza na wazazi wangu akafuata taratibu zote hatimaye anakioa. Niliendelea kufikiria ndoto yangu ya udaktari lakini sikuona ikitimia katika maisha yangu mapya. Nilikuwa navutiwa kuona wenzangu wakiendelea na shule, wakipanda hatua moja hadi nyingine,”anasema na kuongeza:
“Hali hii ilifanya matamanio yangu ya kupata elimu yasipungue, changamoto ikawa itawezekana vipi kusoma na mimi ni mke wa mtu, niliwaza mume atanielewaje nikimwambia nataka kurudi shule.”
Anasema alimshirikisha mama yake suala hilo, akawa upande wake akamsisitiza umuhimu wa kurudi shuleni.
“Sikuishia hapo nikazungumza na baba, hakupinga uamuzi wa mimi kurudi shuleni, alisema kwa kuwa tayari ni mke wa mtu, mume wangu ndiye anapaswa kutoa uamuzi, hivyo nimshirikishe kwa kina kuhusu hilo,” anasema.
Majibu ya wazazi wake yalimpa moyo, moja kwa moja alikwenda kituo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima cha Vwawa Open School kilichopo mjini Vwawa akachukua fomu kwa ajili ya kujiunga na shule.
“Nilirudi nyumbani kuzungumza na mwenzangu, nilimweleza nia yangu ya kurudi shule. Mwanzoni alishangaa na kunihoji inawezekanaje kurudi shule wakati mimi ni mke wa mtu, nikamwambia hakuna kitakachoharibika kwa sababu nitakuwa nakwenda na kurudi.
“Bado alikuwa na wasiwasi, nikamweleza nashinda nyumbani bila shughuli yoyote tena nikiwa peke yangu kwa sababu yeye anakwenda kwenye shughuli zake, hivyo muda ninaokuwa mwenyewe ni heri niende kusona na ratiba inaonyesha masomo yanaisha mchana, anaporudi atanikuta nyumbani,” anasema.
Haikuwa rahisi Sara kumshawishi mume wake amruhusu kurejea shuleni, lakini hatimaye alimwelewa kwa sharti kwamba hatahusika kwa chochote kinachohusu shule.
Sara alishindwa kuanza shule mwanzoni mwa mwaka huu kwa sababu alikosa mahitaji muhimu yakiwamo madaftari, akafikiria kuachana na wazo la kusoma abaki kuwa mama wa familia.
“Nilimuomba baba anisaidie fedha kwa ajili ya vifaa ya shule akasema kwa wakati huo hawezi kwa sababu na mdogo wangu pia alitakiwa kuripoti shuleni. Nikaona hakuna namna naweza kufanikiwa, hivyo niachane na mawazo ya kusoma.
“Januari ikaisha, Februari baba akanipigia simu kuuliza maendeleo yangu nikamwambia sijaenda shule kwa sababu sina madaftari, akanipatia pesa. Yakanijia mawazo mengine, hivi nikienda huko shuleni nitaonekanaje watu hawatanishangaa na mtoto wangu mgongoni maana sikuwa na mtu wa kumuachia,” anasema.
Mawazo yaliendelea kutawala kichwani mwake, lakini kwa kuwa nia alikuwa nayo akaamua kwenda shuleni kuanza safari kupambania ndoto yake ya udaktari.
Alipofika shuleni alishangaa kujiona si peke yake mwenye mtoto mgongoni, alikutana na wasichana wengine wenye umri wake walioamua kurudi shuleni baada ya kukatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali, ukiwamo ujauzito.
“Kuwakuta watu wenye hali kama yangu ilinipa moyo kwamba siko peke yangu, hivyo napaswa kuitumia vyema fursa hii kuhakikisha ndoto yangu inatimia. “Kituoni nimekuta kuna mlezi anayewaangalia watoto muda ambao sisi tuko darasani, hilo limenipa wasaa mzuri wa kuzingatia kile kinachofundishwa,” anasema.
Katika juma la kwanza, anasema alianza kupata matumaini kwamba hatimaye anaenda kuipata elimu itakayomwezesha kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari wa watoto.
Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu alianza kupata changamoto kutokana na uamuzi aliofanya.
Anasema kama ambavyo mume wake alimuahidi asingehusika kwa chochote katika elimu yake, ameshikilia msimamo huo hivyo kuna wakati anashindwa kwenda shuleni kwa kukosa nauli.
“Mume wangu yuko tayari kutoa matumizi yote ya nyumbani lakini si kugharimia chochote kinachohusu shule, hata nauli nalazimika kubana anazotoa kwa ajili ya chakula nyumbani au nimuombe baba ndipo niweze kufika shuleni. Ikitokea baba hana pesa na nimeshindwa kubana bajeti basi siendi shuleni.
“Hilo nilikuwa tayari kulivumilia kwa sababu alisema tangu awali, changamoto nyingine iliyoibuka ni namna anavyosumbuliwa na msukumo wa wanajamii. Watu wanamsema inakuwaje anamruhusu mke wake asome, wanamshangaa kwa nini mwanamke ambaye ameshazaa anaachwa aende shule, wapo waliomwambia nikifanikiwa kufika chuo kikuu nitamuacha niende kwa wanaume wengine,” anasema.
Sara anasema: “Maneno hayo na mengine mengi ya kukatisha tamaa yanamfanya mume wangu awe mgumu kwangu, amekuwa mkali hataki kusikia kuhusu mimi kusoma, anatafuta visingizio kwamba simuangalii mtoto vizuri. Imefika hatua hata ndoa yangu iko hatarini na nimemwambia achague moja kama hataki nisome basi tuachane nirudi nyumbani.”
Anasema kwa sasa hakuna namna ataruhusu vikwazo vikatishe safari yake ya kusaka elimu kwa kuwa ametambua kama hatosoma maisha yatakuwa magumu, hivyo ni lazima asimame imara kuhakikisha anatimiza ndoto yake.

“Najitahidi nisimpe sababu, licha ya kusoma nahakikisha nafanya majukumu yote ya nyumbani kama mke na mama kabla ya kwenda shuleni. Pia mfumo wangu wa maisha najaribu niwe tofauti na walivyo wanafunzi angalau asione kusoma kwangu kumenibadilisha kwa namna moja au nyingine,” anasema.
Subira Mtindya, mama yake Sara anasema huwa anamsihi binti yake kumheshimu mume wake kwa kuwa ni wanaume wachache wanaoweza kuwaruhusu wake zao wasome.
“Sisi wazazi tunafurahia kumuona binti yetu amerudi shule, hata kama ni mke wa mtu tunashukuru kwa huyu mwanaume kuruhusu hilo. Kuhusu mahitaji hatuoni shida kuhakikisha anapata kila anachohitaji ili kumsaidia kwenye safari yake ya masomo,” anasema na kuongeza:
“Namsisitiza aendelee kumheshimu na kumsikiliza mume wake ili kisitokee chochote ambacho kinaweza kubadili mawazo yake akamzuia asiendelee na masomo, tunaamini kwa kurudi shuleni ndoto yake itakwenda kutimia. Niko tayari kumlea mtoto ili apate wasaa mzuri wa kusoma.”
Mkufunzi Mkazi wa elimu ya watu wazima mkoani Songwe, Camillus Mwila anamtaja Sara kuwa miongoni mwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa darasani na shauku ya kujifunza, hivyo taasisi inaendelea kumjenga kisaikolojia aendelee kuwapo shuleni.
“Wasichana wanaoamua kurudi shule wana uwezo mkubwa kitaaluma na Sara ni miongoni mwao. Unapozungumza naye unaweza kuelewa ni kwa kiasi gani binti huyu ana upeo mkubwa na shauku ya kupata elimu.
“Binafsi nafahamu changamoto aliyonayo na nimeshakutana na mumewe kuzungumza naye, nitaendelea kufanya hivyo kumshawishi amuunge mkono kwenye safari hii ya kusaka elimu. Ninachoona hawa wote ni vijana, bado kuna ile hali ya utoto lakini kwa sababu binti ana nia ya kusoma tutahakikisha lengo lake linatimia,” anasema.
Mwila anasema wana programu maalumu za ushauri kwa ajili ya wanafunzi, wakiwamo wasichana wanaorejea shuleni.
Anasema wataalamu mbalimbali hufika kuzungumza nao na kuwajenga kisaikolojia.
“Hata Sara kuendelea kuwapo shuleni hadi sasa ni jitihada zinazoendelea kufanyika katika kumjenga na kumpa hamasa ili asimamie ndoto yake, asifikirie kukata tamaa kwa sababu akiacha shule itakuwa vigumu kutimiza ndoto ya kuwa daktari. Naamini kwa kuwa ana nia itakuwa rahisi kwake kutimiza,” anasema.
Habari hii ni kwa udhamini wa Gates Foundation