Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakuu wa shule wanavyowabania waliojifungua kurejea shule

Muktasari:

  • Utafiti wabaini walimu, wakiwamo wakuu wa shule hawana uelewa wa kutosha kuhusu mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi, wadau washauri kutungwa sheria.

Dar es Salaam. Tangu mwaka 2022, Serikali ilipoanza utekelezaji wa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi, wakiwamo waliopata ujauzito, imeshuhudiwa mabadiliko hasa katika maeneo ya haki ya elimu kwa wasichana.

Mwongozo huu uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Februari, 2022 unakusudia kutoa fursa ya pili kwa wanafunzi waliokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali kuendelea na elimu.

Mwongozo huu ulitanguliwa na waraka namba 2 wa mwaka 2021 uliotoa ruhusa ya kurejea shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.

Katika utekelezaji yamekuwapo mabadiliko chanya, kwamba kuna ongezeko la idadi ya wasichana wanaorejea shuleni, ikiwa ni ishara kuwa jamii inaanza kuelewa na kukubali umuhimu wa elimu kwa kila mtoto bila kujali changamoto alizopitia.

Jamii imeanza kubadilika kifikra, ikiondoa unyanyapaa dhidi ya wasichana waliopata ujauzito wakiwa bado wanafunzi.

Kwa upande mwingine, mashirika ya kiraia na wadau wa elimu wamekuwa mstari wa mbele katika utoaji elimu ya haki za watoto na kuhamasisha jamii kuunga mkono juhudi hizi.

Serikali imeongeza jitihada za kutoa elimu ya afya ya uzazi shuleni na kuwawezesha walimu na maofisa elimu kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi wanaorejea, hivyo kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi.

Hata hivyo, bado kuna hali ya unyanyapaa na ubaguzi kwa wanafunzi wanaorejea shuleni kutoka kwa walimu, wanafunzi wenzao na hata baadhi ya wanajamii.

Kutokana na hayo, kumekuwapo athari za kisaikolojia kwa wanafunzi kwa uwezo wao wa kujifunza. Si hivyo tu, baadhi wanakosa ufuatiliaji wa karibu kuhusu maendeleo yao ya kitaaluma na kihisia.

Kwa maeneo ya vijijini, kutokana na changamoto ya upungufu wa walimu wa ushauri, vifaa vya kujifunzia, na mazingira rafiki kwa wasichana, wanafunzi wanaorejea wanaathiriwa.

Ufuatiliaji uliofanywa na Mwananchi katika baadhi ya mikoa umebaini wapo wanaoshindwa kurejea shuleni kutokana na vikwazo kadhaa, ikiwamo kukataliwa na wakuu wa shule.


Ushuhuda wa mabinti

Diana Nyamahanga (18) ni miongoni mwa walioathiriwa na kikwazo hicho alipoomba kurejea katika Shule ya Sekondari Idodi mkoani Iringa, miezi michache baada ya kujifungua.

Alikatiza masomo akiwa kidato cha nne kwa sababu ya ujauzito ikiwa ni miezi mitano kabla ya kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari.

Akiwa na shauku ya kurejea baada ya kujifungua ili kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanasheria, aliambiwa asingeweza kurudi shuleni hapo kwa sababu ataharibu wanafunzi wengine.

“Nilipofika shuleni nilipokewa na viongozi wa shule, nilieleza nia yangu ya kuendelea na masomo. Niliambiwa natakiwa kukaa miezi sita nyumbani kabla ya kurudi shuleni ili nipate muda wa kumnyonyesha mtoto.

“Nikawaambia nyumbani na shuleni si mbali naweza kutumia muda wa mapumziko kwenda kumnyonyesha mtoto, wakasema watakaa kikao, baada ya mazungumzo niliambiwa siwezi kurudi kwa sababu nitawafundisha tabia mbaya wasichana wengine maana inajulikana nilipata ujauzito,” anasema.

Diana anasema kwa msaada wa ndugu zake alipata shule nyingine Iringa mjini lakini alitakiwa kuacha mtoto nyumbani.

“Nilikataa kwa sababu sikutaka kuwa mbali na mtoto wangu. Niliamua nitasoma popote nikiwa naye,” anasema.

Kwa mujibu wa mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatiza masomo ya elimu ya msingi na sekondari wanaruhusiwa kuchagua kurudi katika shule ya awali au kuhamia nyingine kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mwananchi ilimtafuta Mkuu wa Shule ya Sekondari Idodi, Bakari Msangi ambaye alikataa kuzungumzia suala hilo hadi atakapopata kibali cha mkurugenzi wa halmashauri.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya alipotafutwa alisema hana taarifa ya suala hilo na kuahidi kulifanyia kazi.

“Sifahamu chochote, ningelifahamu hilo si tatizo kwa sababu mwongozo umeweka wazi, mwanafunzi akishajifungua na kuwa tayari kurudi shule utaratibu ni kwamba mzazi anatakiwa aandike barua inayoweza kupita kwa mkurugenzi lakini anaandikiwa katibu tawala wa mkoa. Baada ya utaratibu huo mtoto anatakiwa kurudi shuleni bila masharti, anaweza kupangiwa shule nyingine endapo itaonekana mazingira yale si mazuri kwake kurudi lakini kuhusu huyu mwanafunzi sina taarifa zake ila nitazifuatilia,” amesema.

Familia ya Diana ilimpeleka mkoani Songwe alikojiunga na kituo cha Open Vwawa chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuendelea na masomo.

Diana anasema licha ya mazingira magumu kutokana na kuchanganya masomo na malezi ya mtoto, lakini hajafikiria kukata tamaa ya kuifikia ndoto yake.

“Kwa sasa nasoma ili nifanye mtihani wa kidato cha nne lakini huo si mwisho wangu, nitahakikisha naenda hatua inayofuata na nyingine zinazoweza kunitengeneza kuwa mwanasheria,” anasema na kuongeza:

“Nikifika shuleni nahakikisha namnyonyesha mtoto ashibe vizuri, namkabidhi kwa mlezi. Muda wa mapumziko nakwenda kumnyonyesha tena. Kuna muda nakuwa darasani lakini mawazo yanakuwa kwa mtoto hasa pale anapokuwa mgonjwa lakini namshukuru Mungu siku zinasonga na maisha yanaendelea,” anasema.

Queen Johnbosco sawa na Diana, yeye alipata ujauzito akiwa kidato cha tatu mkoani Ruvuma katika sekondari ambayo hakutaka kuiweka wazi.

Anasema baada ya kubainika ana ujauzito, yeye na wazazi wake walikwenda shuleni kuzungumza na mkuu wa shule aliyewaeleza masomo yake yatasimamishwa na ataruhusiwa kurejea baada ya kujifungua.

“Baada ya kujifungua nilikwenda shuleni, mkuu wa shule akawasiliana na ofisa elimu akamwambia kurudi pale ni hadi upite mwaka mmoja, sikutaka kupoteza muda zaidi sikukubaliana na sharti hilo. Ndani ya siku chache nikiwa nyumbani lilipita gari likitangaza kuhusu shule ya taasisi ya elimu nikamwambia mama, tukaenda tena shuleni ambako mkuu wa shule alizungumza na mtu wa taasisi ya elimu nikaanza kusoma,” anasema.

Kwa upande wake, Lulu Richard, anasema alikataliwa na mkuu wa shule kurejea akielezwa atasababisha wasichana wengine waliopata ujauzito kutaka kurejea shuleni hapo.

Baada ya kupata ujauzito akiwa kidato cha nne mwaka 2023, anasema alisimamishwa shule miezi sita kabla ya kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari.

“Ujauzito uligundulika nikiwa na miezi saba, nilisimamishwa shuleni. Katika barua niliyopewa niliambiwa nitaruhusiwa kurudi kufanya mtihani baada ya kujifungua. Hayo yalifanyika baada ya kujulikana kwamba nitajifungua mwezi wa tisa na mtihani unafanyika Novemba.

“Ulipokaribia mtihani nilikwenda shuleni kukamilisha taratibu za kufanya mtihani, niliambiwa niondoke. Mwaka mpya wa masomo ulipoanza nilikwenda tena shuleni Januari 2024 ili nianze na walioingia kidato cha nne mwaka huo nikakataliwa,” anasema.

Mama wa binti huyo akizungumza Aprili, 2024 wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Hakielimu alisema: “Niko tayari kulea mjukuu na mtoto wangu anataka kurudi shule lakini mwalimu mkuu hataki kumpokea, sina uwezo wa kumhamishia kwingine naumia nikiona ndoto zake zinayeyuka.”


Ripoti ya utafiti

Yaliyowasibu Diana, Queen na Lulu yanashabihiana na ripoti ya Taasisi ya Hakielimu iliyotolewa Mei, 2024 ikiwa ni matokeo ya utafiti uliofanyika katika mikoa 12 nchini na kubaini wasichana wanaotaka kurejea shuleni wanakataliwa au kukutana na unyanyapaa kutoka kwa walimu, wanafunzi wenzao na jamii kwa ujumla.

Katika utafiti huo uliofanyika kwenye mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya, Mwanza, Kigoma, Arusha, Dodoma na Morogoro walihojiwa wasichana 28 na asilimia 61.2 ya wahojiwa walieleza wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya udhalilishaji, wakiitwa majina yasiyofaa na yanayokatisha tamaa.

Asilimia 53.2 walieleza licha ya shauku waliyonayo ya kurejea shuleni wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kutolewa mfano kila wakati.

Walimu wakuu wametajwa katika utafiti huo kwamba wanachangia waliopata ujauzito wasirejee shuleni ikielezwa huwakataa kwa hofu ya kuwaharibu wanafunzi wengine.

Mtafiti Dk Joyce Mbepera, anasema utafiti huo ulibaini wapo wakuu wa shule ambao wanakataa kuwapokea wanafunzi waliojifungua licha ya mwongozo kuwapa jukumu la kuwahamasisha warejee shuleni.

Dk Joyce anasema utafiti huo ulibaini walimu, wakiwamo wakuu wa shule hawana uelewa wa kutosha kuhusu mwongozo huo.

“Asilimia 29.4 ya wahojiwa walieleza wamejaribu kurejea shuleni lakini wanakataliwa na wakuu wa shule wakihofia kuwafundisha wanafunzi wengine tabia mbaya. Tuna mfano wa mzazi ambaye alikwenda mara kadhaa shuleni kuomba mtoto wake arejee masomoni baada ya kujifungua lakini amekataliwa hadi sasa yupo nyumbani,” alisema.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Franklin Rwezimula aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo alielekeza suala hilo kushughulikiwa.

“Serikali imeshatoa mwongozo, changamoto ninayoiona hapa ni baadhi ya watekelezaji kutokuwa na uelewa wa nini wanachotakiwa kufanya, muhimu kila mmoja kufuata majukumu yake kama ilivyoainishwa,” alisema.

Hata hivyo, alipozungumza na Mwananchi Aprili 2, 2025 Lulu alisema bado hajarejea shuleni kwa sababu uongozi wa shule haujakubali kumpokea.

Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahaba alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mwenendo wa baadhi ya wakuu wa shule kuwazuia waliojifungua kurudi shuleni, anasema msimamo wa Serikali ni kusimamia utekelezaji wa mwongozo.

“Serikali imeshatoa mwongozo na unaeleza wazi kwamba, mwanafunzi anaweza kurudi shule ileile au akachagua kwenda nyingine, hili la wakuu wa shule kuwakatalia ni kinyume cha mwongozo, hivyo nitalifuatilia nipate taarifa na hatua zitachukuliwa,” anasema.


Sheria yatajwa

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi anasema ili kukabiliana na changamoto hiyo kuna haja ya yaliyomo kwenye mwongozo kuwa na nguvu ya kisheria.

Rebeca anasema kwa kufanya hivyo uamuzi wa kuwarejesha shuleni utakuwa si utashi wa kiongozi aliye madarakani, bali ni suala la kisheria na utekelezaji wake unapaswa kusimamiwa kikamilifu.

“Ni suala ambalo tumelipigia kelele tangu utekelezaji wa mwongozo uanze na hata ripoti ya utafiti wa Hakielimu imependekeza ni lazima kuwe na sheria inayosimamia suala la wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni,” anasema.

Anasema sheria hiyo ibainishe vipaumbele vya kibajeti kuwezesha mambo yanayoendana na utekelezaji wa mwongozo huo wenye lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu.

“Ni muhimu kwenye sheria ionekane utaratibu wa kumuondoa na kumrejesha shuleni aliyepata ujauzito, isiwe amegundulika leo halafu anafukuzwa shuleni. Kama ujauzito wake ni mdogo aachwe hadi pale atakapokaribia kujifungua ndipo aondoke.

“Sheria ionyeshe huduma atakazopata binti aliyejifungua na kurejea shuleni, katika hali ya kawaida ni lazima apate huduma za unasihi ili kumweka sawa. Pia, sheria ionyeshe mtoto atakayezaliwa atapata huduma zipi, hapa tunazungumzia vile vituo vya kulelea ili mama yake awe anapata muda wa kumnyonyesha huku akiendelea na masomo,” anasema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema wakuu wa shule wanaozuia wanafunzi waliojifungua kurudi shule wanakiuka mwongozo na mkataba wa kimataifa ambao Serikali imeridhia.

Anasema: “Suala hili lilitolewa kama tamko kisha ukatolewa mwongozo, nafikiri hii ni nyaraka inayopaswa kuheshimiwa. Wakati tunasubiri sheria ni lazima tuzingatie mwongozo, hawa wanaowazuia wasichana kurudi shuleni baada ya kujifungua wanafanya kosa na wanapaswa kuchukuliwa hatua.”

Anawaomba wazazi wasisite kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokutana na changamoto za aina hiyo.

“Usikubali kumuacha mtoto akae nyumbani wakati Serikali imeruhusu arudi shule kupambania ndoto zake,” anasema.

Usikose mfululizo wa makala haya. Kesho tutaangazia namna wasichana hawa wanaokataliwa wanavyotumia madarasa ya elimu ya watu wazima kama kimbilio lao.


Habari kwa udhamini wa Bill and Melinda Gates Foundation