Elimu ya watu wazima inavyookoa mabinti wanaokataliwa shule baada ya kujifungua

Muktasari:
- Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kupitia mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari (Sequip-AEP) imekuwa kimbilio la wasichana wengi waliopata ujauzito wakiwa shuleni kujiunga kuendelea na masomo ya sekondari.
Dar es Salaam. Licha ya kuwapo mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi, wakiwamo waliopata ujauzito imebainika wengi wanajiunga na mfumo usio rasmi, ikiwamo elimu ya watu wazima.
Takwimu zilizochapishwa kwenye matokeo ya ufuatiliaji wa wasichana waliorejea shuleni baaada ya kujifungua uliofanywa na Shirika la Msichana Initiative uliotolewa Novemba 2024 zinaonyesha hadi kufikia Machi 2024, wasichana 22,844 nchini Tanzania walirudi shuleni chini ya mwongozo uliotolewa na Serikali.
Wasichana 5,142 walirudi katika mfumo rasmi, huku wengine 17,702 walirudi katika mfumo usio rasmi.
Mwongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Februari, 2022 unakusudia kutoa fursa ya pili kwa wanafunzi waliokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali kuendelea na elimu. Ulitanguliwa na waraka namba 2 wa mwaka 2021 uliotoa ruhusa ya kurejea shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kupitia mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari (Sequip-AEP) imekuwa kimbilio la wasichana wengi waliopata ujauzito wakiwa shuleni kujiunga ili kuendelea na masomo ya sekondari.
Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2022 hadi kufikia mwaka huu umetoa fursa kwa wasichana 13,242 kurudi shuleni baada ya kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali zikiwamo ujauzito, utoro, ugonjwa na umaskini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Sequip-AEP katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa programu hiyo walisajiliwa wasichana 3,833. Mwaka 2023 walisajiliwa 3,616, mwaka 2024 walisajiliwa 3,290 na mwaka 2025 wamesajiliwa 3,003.
Shuhuda za wasichana
Lydia Mkirya (20), Loveness Mlelwa (18) na Grace Anyitikisye (19) ni miongoni mwa waliorudi shuleni kupitia mradi wa Sequip-AEP.
Lydia alikatisha masomo miezi miwili kabla ya kufanya mtihani wa kidato cha nne baada ya kugundulika ana ujauzito wa miezi minane, akiwa Sekondari ya Sili iliyopo Peramiho mkoani Ruvuma.
Alifikwa na kadhia hiyo kutokana na uhusiano wa kimapenzi aliokuwa nao na dereva wa bodaboda aliyekuwa akimpeleka shuleni na kumrudisha nyumbani.
“Nilipojifungua niliamua kurudi shuleni, niliambiwa haiwezekani mtu mwenye mtoto kurudi tena shuleni. Sikutaka kubishana nikafikiria kuitafuta elimu nje ya mfumo rasmi,” anasema.
Mwaka 2024 alijiunga na elimu ya watu wazima kituo cha Mahenge, Songea mjini na mwaka huu anatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.
Kwa upande wake, Loveness alikatisha masomo baada ya kupata ujauzito akiwa kidato cha tatu katika sekondari ya Luwawasi mkoani Ruvuma.
“Baada ya kujifungua nilikuwa na shauku ya kuendelea na masomo lakini sikutaka kurudi shule niliyokuwa nasoma kwa sababu ya unyanyapaa, nilishaanza kunyooshewa vidole, mtaani nikipita nazungumzwa.
“Nikawaambia wazazi nataka kusoma lakini si kwenye shule za kawaida waniruhusu nikasome kwenye kituo cha elimu ya watu wazima. Nashukuru walinielewa na sasa natarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu,” anasema.
Grace yeye alipata ujauzito akiwa kidato cha pili. Licha ya kufahamu kuwa alikuwa na nafasi ya kurudi Shule ya Sekondari ya Milundikwa, iliyopo Sumbawanga mkoani Rukwa alikokuwa akisoma kabla ya kupata ujauzito, hakurudi kutokana na namna alivyokuwa akizungumzwa.
“Mwaka 2023 nikasikia kuna shule zimeanzishwa kwa ajili ya waliopata ujauzito, nikasema hii ndiyo nafasi ya kutimiza malengo yangu. Kikwazo kikawa mtoto, walisema bado mdogo ilibidi nisubiri hadi alivyofikisha miezi minne nikamwambia mama sasa naweza kwenda kusoma,” anasimulia.
Grace ni mwanafunzi katika kituo cha Vwawa Open School kilichopo mkoani Songwe akiwa miongoni mwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Kuhusu mradi
Akizungumza na Mwananchi, Baraka Kionywaki, Mratibu wa mradi wa Sequip-AEP anasema kati ya wasichana 13,242 asilimia 13 pekee ndio wameweka wazi kuwa walikatisha masomo kwa sababu ya ujauzito.
“Sisi tunachoangalia msichana alikatisha masomo anataka kurudi shuleni, sababu gani ilimfanya akatishe ni hadi pale atakapoamua kueleza mwenyewe. Huku ni elimu ya watu wazima, huwezi kumlazimisha mtu aseme mambo yake binafsi ila kwa wale ambao wameamua kuweka wazi ni asilimia 13.
“Hii ina maana kila kwenye wasichana 100 tulionao kwenye shule na vituo vyetu basi 13 walikatisha masomo kwa sababu ya ujauzito. Hili hatuna takwimu zake za uhalisia kwa sababu si lengo letu, tunachotaka wasichana wapate elimu kama tulivyoelekezwa na Serikali,” anasema.
Kionywaki anasema huenda sababu hiyo inawafanya wasichana wengi kuvutiwa na elimu iliyo katika mfumo usio rasmi kwa sababu hawakutani na mazingira yatakayowafanya wahisi kunyanyapaliwa.
Anasema unyumbufu wa utekelezaji wa programu hiyo unafanya mazingira ya kujifunzia yawe rafiki na yanayohamasisha kuweka mkazo kwenye masomo wakati mwanafunzi akipata fursa ya kuendelea na mambo mengine, ikiwamo malezi ya mtoto.
“TEWW iko nchi nzima halafu kupitia mradi huu tumejenga vituo 14 maalumu kwa ajili ya hawa wasichana, sita tayari vimeanza kufanya kazi na kwenye vituo hivi kuna miundombinu wezeshi kwa ajili ya wao kuwa na watoto wao,” anasema na kuongeza:
“Mama akiwa anasoma halafu anajua mtoto wake yupo katika mazingira karibu na alipo anaweza kwenda kumnyonyesha au kumlisha ni rahisi kwake kuweka mawazo yote darasani tofauti na yeye kuwa shule hajui mtoto ana hali gani, anahudumiwa vipi hapa kidogo kunaweza kuwa na changamoto.”
Anasema kwenye vituo wamezingatia hilo kwa kuweka vyumba kwa ajili ya watoto ambao hukaa na matroni.
“Wadau katika baadhi ya maeneo wanaunga mkono kwa kutoa huduma ya hosteli ili hawa wasichana wasilazimike kutembea umbali mrefu kutafuta elimu wasije kuangukia tena kwenye vishawishi,” anasema.
Mratibu huyo anasema mbali na elimu ya darasani, mfumo wa elimu ya watu wazima unatoa nafasi kwa wasichana hao kujifunza vitu vingine ambavyo vina msaada katika maisha yao.
Akizungumzia hilo, Dk Hellen Lyamuya, meneja wa kampasi ya elimu ya watu wazima mkoani Ruvuma anasema kupitia somo la stadi za maisha wanafunzi hufundishwa mada kuhusu malezi, maisha, shughuli za ujasiriamali na namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa.
“Kupitia somo hili tunawafundisha kuwa wanajamii, kutambua hali walizonazo na jinsi gani wanaweza kuendana na ujifunzaji na majukumu yao kama wazazi. Pia, namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kwenye jamii.
“Wakati mwingine tunawapatia semina, wanakuja wataalamu kuwafundisha kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo magojwa na jinsi ya kuchukua tahadhari kwa sababu hawa bado ni watoto na wapo hatarini,” anasema.
Anasema walimu wanaishi kwa urafiki na wanafunzi, kama inavyoitwa elimu ya watu wazima.
“Tunajitahidi kuwa nao karibu kiasi cha kumfanya awe huru kukueleza pale anapofikwa na changamoto, mwingine anashindwa kusoma kwa sababu mtoto anaumwa na hajui kama anaumwa, kwa hiyo ukiwa naye karibu atakuelezea na utamshauri ampeleke hospitali,” anasema.
Mbali na somo hilo, anasema huduma za ushauri hutolewa kupitia madawati ya ushauri ya vituo, hivyo husaidia kuwaondolea msongo wa mawazo wanapokutana na mazingira yanayowakatisha tamaa.
Anasema huduma za ushauri huwasaidia kuendana na mazingira ya ujifunzaji, malezi ya watoto wao na namna ya kuishi kama wanajamii.
Mkufunzi mkazi wa elimu ya watu wazima Mkoa wa Songwe, Camillus Mwila anasema katika vituo vyote vilivyopo mkoani humo kuna mtu maalumu kwa ajili ya kutoa ushauri kwa wanafunzi anayezungumza nao mara mbili kwa wiki.
“Tuna utaratibu wa wiki mara mbili kuzungumza na wanafunzi, hii inajumuisha wote wa kike na wa kiume. Pia kunakuwa na nafasi ya mtu mwenye changamoto kuzungumza naye,” anasema.
Anasema udahili wa walimu unazingatia wengi wa kike ili iwe rahisi kwa mabinti kuwaona kuwa ni wenzao, wawe huru kuzungumza nao na kuwaweka vizuri kisaikolojia.
Mwila anayesimamia kituo cha mfano kiitwacho Vwawa Open School kilichopo mkoani Songwe anasema kinachowavutia wasichana kuendeleza ndoto zao za elimu kwenye kituo hicho ni uwepo wa mlezi wa watoto.
“Inawezekana kuna msichana anataka kusoma lakini hana wa kumuachia mtoto, hapa kwetu kuna mlezi na chumba maalumu kwa ajili ya watoto, wakati mama anaendelea na masomo darasani mtoto atabaki hapo na atakuja kumnyonyesha muda wa mapumziko,” anasema.
Neema Mbati, mlezi wa watoto kwenye kituo hicho anasema kwake ni baraka kuwasaidia wasichana wenye nia ya kufufua ndoto zao.
“Si kwamba napenda wanafunzi wapate ujauzito, ila ikitokea amepata basi asiruhusu hilo liwe kikwazo cha yeye kupata elimu. Serikali imesharuhusu wasichana warudi shule naamini wataitumia vyema fursa hii.
“Nafurahi kwa ajili ya wasichana hawa ambao wamerudi, kama mlezi kila siku nawaambia wazingatie masomo na waniachie uangalizi wa watoto wao muda ambao wako darasani. Ni safari ya muda mfupi hivyo wanapaswa kuweka juhudi,” anasema.
Itaendelea kesho sehemu ya mwisho kuonyesha ndoto za mmoja wasichana hao.
Habari kwa udhamini wa Gates Foundation