Huu ndio umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu ya awali

Muktasari:
- Kuwekeza kwenye darasa bora la elimu ya awali, ni hatua muhimu inayoweka msingi thabiti wa mafanikio ya mtoto katika maisha ya baadaye.
Katavi. Wakati utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 ukiendelea, wadau wa elimu wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha uwekezaji mkubwa unafanyika kwenye elimu ya awali.
Hatua hiyo inalenga kutengeneza mazingira wezeshi ya kujifunzia kwa watoto ambayo yatakuwa rafiki kujifunzia, yaliyo na vifaa vya kujifunzia vinavyofaa umri wao, pamoja na walimu waliobobea katika malezi na elimu ya awali.
Hayo yameelezwa na wadau wa elimu walipotembelea madarasa ya awali ya mfano katika shule ya msingi Ikuba iliyopo Halmashauri ya Mpimbwe yanakofanyika maadhimisho ya juma la kimataifa la elimu (GAWE).
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet) Martha Makala, amesema darasa bora ni nguzo muhimu ya kuhakikisha elimu ya awali inakuwa yenye ubora na tija.
Amesema hilo si jukumu la Serikali pekee, bali linahitaji ushirikiano wa jamii nzima wazazi, mashirika na wadau wa elimu ili kuhakikisha kila mtoto anaanza safari yake ya elimu katika mazingira bora.
“Uwekezaji kwenye elimu ya awali unahusisha kuwa na mazingira salama na ya kuvutia kwa mtoto kujifunza.Darasa lenye mwonekano mzuri, rangi zenye kuvutia na vifaa vya kuchezea vya kielimu, huamsha ari ya mtoto kujifunza.

“Watoto hujifunza vizuri zaidi wakiwa kwenye mazingira yanayowapa furaha na usalama wa kihisia.Darasa linapaswa kuwa na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia, vinavyosaidia watoto kujifunza kwa vitendo kupitia michezo, nyimbo, hadithi na mazoezi,” amesema Martha.
Mwalimu wa awali katika Shule ya Msingi Ikuba, Mlegimlegi Mtinga, amesema walimu ni nyenzo muhimu katika elimu ya awali.
“Mwalimu wa elimu ya awali si tu mfundishaji, bali pia mlezi, mshauri na mfano wa kuigwa. Uwepo wa walimu wenye uelewa wa mahitaji ya watoto wadogo huchangia sana katika maendeleo yao ya awali,” amesema Mtinga.
Katika hatua nyingine Shirika la Room to Read limetoa msukumo unaolenga kukuza stadi za watoto kujisomea kwa kuwawekea mazingira rafiki yanayohamasisha usomaji.
Kwa kushirikiana na halmashauri shirika hilo linatekeleza mradi wa kukuza usomaji, ambao unahusisha kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo ukarabati wa vyumba vya maktaba ili kuwawezesha watoto kupata mahali pazuri pa kujisomea.
Akizungumza kwenye maonyesho wakati wa maadhimisho ya juma la elimu mkoani Katavi , Ofisa programu wa Room to Read, Rachel Mbushi amesema maktaba zinazoanzishwa na shirika hilo katika shule za msingi huwekewa vitabu vya hadithi vya watoto vyenye maudhui yanayovutia watoto kusoma na kujifunza.
Amesema sambamba na hilo, shirika pia linajihusisha na uchapishaji wa vitabu vya hadithi za watoto na vitabu vya ziada vya stadi za usomaji kwa darasa la kwanza na la pili.
“Ili kuhakikisha mradi unafikia malengo ya kukuza stadi za usomaji na tabia ya kujisomea miongoni mwa watoto, tunatoa mafunzo ya ufundishaji, kwa walimu wa darasa la kwanza na la pilli, na pia mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa maktaba kwa walimu wakuu, walimu wa lugha na walimu wakutubi katika shule za mradi.
Mbali na maktaba hizo zinazoanzishwa shuleni, shirika hilo pia linatekeleza mradi wa maktaba mtandao unaotoa fursa kwa watu kusoma vitabu kupitia intaneti.