Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hakielimu: Elimu ipewe asilimia 15 ya bajeti kuu

Muktasari:

  • Azimio la Incheon la mwaka 2015 linazitaka nchi zilizo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga angalau asilimia 15-20 ya bajeti kuu za serikali zao kwa ajili ya sekta ya elimu.

Dar es Salaam. Wakati bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikitarajiwa kuwasilishwa bungeni Mei 12 na 13, 2025, Taasisi ya Hakielimu imetoa mapendekezo matano ya kuwekewa nguvu ili kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu nchini.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti ya sekta elimu kufikia angalau asilimia 15, iwe jumuishi na yenye mlengo wa kijinsia, kuandaa mkakati mahususi wa ajira na mafunzo kupunguza uhaba wa walimu pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya uchapaji na usambazaji wa vitabu vya mtaala mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Mei 5, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage amesema Azimio la Incheon la mwaka 2015 linazitaka nchi zilizo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga angalau asilimia 15-20 ya bajeti kuu za Serikali zao kwa ajili ya sekta ya elimu.

Kalage amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilitenga na kuidhinisha Sh6.17 kwa ajili ya sekta ya elimu, sawa na asilimia 12.5 ya bajeti ya Taifa iliyokuwa Sh49.3 trilioni.

Amesema kiwango hicho ni chini ya kiwango kilichopendekezwa na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Elimu (ESDP III) pia azimio la Incheon.

Hivyo wameitaka Serikali kuongeza bajeti hiyo kufikia angalau asilimia 15 ya bajeti kuu kama ilivyo katika makubaliano hayo ya kikanda.

“Tanzania imekuwa na mwenendo usioridhisha katika kufikia azma hii kwa kushindwa kufikia walau asilimia 15 ya bajeti ya Taifa kwa miaka mitano mfululizo, HakiElimu inatarajia ongezeko la Sh2.8 trilioni ili kufikia Sh8.2 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026,”amesema.

Ameongeza iwapo Serikali ingekuwa inatenga bajeti ya elimu kwa kiwango hicho ingeweza kutatua kwa kiwango kikubwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu.

Pia amegusia changamoto ya uhaba wa elimu na kuitaka Serikali kutenga bajeti na kuandaa mkakati mahususi kupunguza tatizo hilo.

Amesema Wizara ya Tamisemi (2024) kwa Kamati ya Bunge ya Elimu imeonyesha kuwa shule za awali zina upungufu wa walimu 61,559, shule za msingi 124,826, na shule za sekondari 82,517 hivyo kufanya jumla ya upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari kufikia 268,902.

Ili kupunguza uhaba wa walimu ameshauri Serikali kuja na mkakati wa muda mfupi angalau miaka mitano kuajiri walimu wapya wasiopungua 40,000 kila mwaka.

“Katika upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2025/2026, tunapendekeza Serikali itenge bajeti maalumu kwa ajili ya kuajiri walimu wapya wasiopungua 40,000 kila mwaka,” ameeleza.

Amesisitiza mkakati wa kuongeza walimu utoe kipaumbele kwa walimu wa sayansi, hisabati pamoja na elimu maalumu.

“Ingawa Serikali imechukua hatua kuajiri walimu 1,022 wa elimu maalumu katika shule za Serikali, bado uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu umebaki kuwa 1:77, kinyume na miongozo inayopendekeza uwiano kuwa 1:10,” amesema.

Ili kutengeneza mazingira rafiki ya ujifunzaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu taasisi hiyo imeitaka Serikali kupunguza au kuondoa kabisa kodi na tozo za uingizaji wa vifaa visaidizi, pamoja na kutoa ruzuku na motisha kwa wazalishaji wa ndani wa vifaa hivyo.

Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kushusha gharama za ununuzi wa vifaa hivyo ili familia ziweze kumudu pamoja na kuongeza uzalishaji wa vifaa hivyo visaidizi ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Pia wametaka kutengwa kwa bajeti ya uchapaji na usambazaji wa vitabu vya mtaala mpya pamoja na kuongeza wigo wa usambazaji wa vitabu kwa njia ya maktaba mtandao itakayosaidia kuongeza wigo wa matumizi ya teknolojia katika kujifunza na kufundishia.

Kuongezwa kwa ruzuku

Kwa upande wake, Meneja Idara wa Utafiti, Ubunifu na Uchambuzi wa Sera HakiElimu, Mwemezi Makumba amegusia ruzuku zinazokwenda katika shule za Serikali na kutaka kiwango chake kuongezwa kutoka Sh10,000 hadi Sh25,000 kwa mwanafunzi wa msingi na kutoka Sh25,000 hadi Sh50,000 kwa sekondari.

Pia ameitaka Serikali kupitia upya mwongozo wa ugawaji wa fedha hizo ili kutenga fedha maalumu kwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike.

“HakiElimu inapendekeza Sh2,500 kutengwa kwenye kila ruzuku ya mwanafunzi kwa ajili ya mahitaji haya ya taulo za kike mashuleni,” amesisitiza.