Mambo matano kuimarisha uhuru wa wanataaluma Afrika

Muktasari:
- Masuluhisho hayo yametolewa baada ya wasomi hao katika mkutano wa siku nne ulioratibiwa na Kitivo cha Sayansi za Jamii cha UDSM kwa kushirikiana na Baraza la Maendeleo ya Utafiti wa Sayansi za Jamii barani Afrika (Codesria) kujadili uhuru wa kitaaluma katika bara la Afrika, kuibua changamoto mbalimbali zinazopelekea kuminywa kwa uhuru wao wa kitaaluma.
Dar es Salaam. Wanazuoni wameainisha mambo matano muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ili kufanikisha upatikanaji wa uhuru kamili wa kitaaluma kwa wasomi na taasisi za elimu ya juu barani Afrika.
Mambo hayo waliyoyabainisha ni pamoja na matumizi ya lugha ya kufundishia inayoeleweka vyema, mamlaka kukubali kukosolewa, mazingira huru ya utawala kwa vyuo vikuu, ufadhili huru na wazi, pamoja na wanataaluma kuzingatia maadili na wajibu wao katika jamii.
Masuluhisho hayo yametolewa baada ya wasomi hao katika mkutano wa siku nne ulioratibiwa na Kitivo cha Sayansi za Jamii cha UDSM kwa kushirikiana na Baraza la Maendeleo ya Utafiti wa Sayansi za Jamii barani Afrika (Codesria) kujadili uhuru wa kitaaluma katika bara la Afrika, kuibua changamoto mbalimbali zinazopelekea kuminywa kwa uhuru wao wa kitaaluma.
Baadhi ya changamoto walizozibainisha katika mkutano huo ni pamoja na lugha, uhaba wa fedha za tafiti, kuingiliwa kisiasa na kiutawala, shinikizo katika baadhi ya taasisi, pamoja na uoga wa wasomi wenyewe.
Akizungumza na Mwananchi Mwanazuoni Mkongwe na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Profesa Fikeni Senkoro amesema uhuru wa kitaaluma hauanzii vyuoni bali hujengewa misingi yake kuanzia kazi za awali, msingi na sekondari.
Senkoro amesema lugha ya kufundishia ina nafasi katika kutengeneza msingi wa wanataaluma kuanzia ngazi za awali katika elimu.
"Kwa mfano kwa Tanzania kama lugha ya kufundishia ikiwa ni Kiswahili inamaanisha wanafunzi tumewapa uhuru wa kitaaluma na kujieleza mawazo yao kwa lugha wanayoielewa vizuri," amesema.
"Pia, walimu kufundisha kwa kutumia lugha wanayoielewa vyema hivyo mawasiliano baina ya mwanafunzi na mwalimu yakifanyika katika lugha ambayo wote wawili wanaielewa huo ndio mwanzo wa uhuru tunaouongelea," amesema.
Vilevile aligusia suala la ufundishaji kwa kwa kutumia nadharia zilizobuniwa na watu kutoka nje na kutoa wito kwa wasomi wazawa kubuni nadharia hizo.
"Tusiishie tu kulalamika bila sisi kuziunda nadharia hizo tutaendelea kutumia za kutoka nje," ameeleza.
Kauli ya Senkoro imeungwa mkono na Profesa Keneth Simala ambaye ameeleza kuwa hata nadharia zinazotumika kuchanganua fasihi pamoja na isimu za lugha ya Afrika ni za kigeni.
"Hii inatulazimisha kuendeleza fikra na mitazamo ya kikoloni, hauwezi kuzungumzia uhuru wa kitaaluma bila kuizungumzia lugha," ameongeza.
Kukubali kukosolewa
Mwanasiasa na mwanataaluma Profesa Anna Tibaijuka akichangia mada katika mkutano huo ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kushirikiana na wanataaluma na wanazuoni pamoja na kukubali kukosolewa.
"Vyuo vikuu ndio sehemu ambapo maarifa mengi yanazalishwa na hilo haliwezi kufanyika kwa ufanisi kama hakuna uhuru wa kitaaluma," amesema.
Pia, ametoa wito kwa wanataaluma kuendelea kushirikiana na kupaza sauti kupitia makongamano na mijadala mbalimbali kufikia uhuru kamili wa kitaaluma.
Utawala wa vyuo vikuu
Awali katika mahojiano na Mwananchi, mwanazuoni mkongwe Profesa Issa Shivji amesema mwaka 2000 nchini ulianzishwa utaratibu uliowatambua wanazuoni kuwa sehemu ya watumishi wa umma na utaratibu huo umesababisha Serikali iingilie kila hatua ya uendeshaji wa vyuo.
"Sasa kama Serikali inaingilia utapata watu watakaokuwa na ujasiri wa kuzungumza? Na uongozi wa chuo utatakiwa kulinda uhuru wa chuo husika," amesema.
Alieleza kuwa kunahitajika kuwepo kamisheni itakayokuwa mwamvuli wa wanataaluma na wawe huru na wasitambuliwe kuwa watumishi wa Serikali.
Uwepo wa ufadhili wa wazi na huru wa tafili
Akizungumza na Mwananchi, ofisa kutoka Taasisi ya Utafiti nchini Kenya, George Omondi, amesema watafiti wengi katika Bara la Afrika hutegemea ufadhili kutoka taasisi mbalimbali za nje ambazo wakati mwingine huja na masharti mbalimbali.
Amesema wakati mwingine masharti hayo yanaweza kuwa na athari katika tafiti na kuingilia uhuru wa kitaaluma.
Ili kuondokana na hali hiyo wasomi hao wameshauri uwepo wa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Afrika utasaidia kubuni mbinu za kufadhili tafiti bila ya kutegemea hisani ya wadau kutoka nje ya bara la Afrika.
Pia, ufadhili wa pamoja kati ya serikali za Afrika na wafadhili wa nje, ili kudhibiti ajenda ya utafiti.
Vilevile serikali za Afrika kuongeza uwekezaji katika utafiti na kuanzisha sera thabiti za sayansi na ubunifu.