Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya pamba yabaki Sh1,150 kwa kilo, wakulima walalamika

Mkulima Mashaka Matilanya wa Kijiji cha Mwakibuga Wilaya ya Bariadi akionyesha pamba yake iliyo tayari kwa kuuza wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa zao hilo iliyofanyika kijijini hapo Mei 2, 2025.

Muktasari:

  • Serikali imetangaza bei ya pamba daraja la kwanza kubaki Sh1,150 kwa kilo msimu wa 2024/25, hali iliyozua malalamiko kutoka kwa wakulima wakidai gharama za uzalishaji zimeongezeka.

Bariadi. Serikali imetangaza kuwa bei ya kununua na kuuza kilo moja ya pamba safi daraja la kwanza kwa msimu wa kilimo wa 2024/25 itabaki kuwa Sh1,150, hatua iliyozua hisia mseto miongoni mwa wakulima waliokuwa wakitarajia ongezeko la bei.

Tangazo hilo limetolewa jana Ijumaa, Mei 2, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa ununuzi wa pamba iliyofanyika katika Kijiji cha Mwakibuga, Wilaya ya Bariadi.

Aidha, pamba ya daraja la pili itanunuliwa kwa Sh575 kwa kilo, ikiwa ni nusu ya bei ya daraja la kwanza.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), uzalishaji wa pamba nchini unatarajiwa kufikia zaidi ya tani 500,000 msimu huu, ukilinganishwa na tani 149,361 zilizozalishwa msimu uliopita.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima wameeleza kusikitishwa na uamuzi huo, wakidai kuwa gharama za uzalishaji zimeongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo bei hiyo haiendani na uhalisia wa hali ya uchumi vijijini.

“Wakulima tulitarajia bei kubwa zaidi msimu huu, angalau Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa kilo, lakini sasa tumebaki na bei ile ile ya mwaka jana. Kwa hali hii hatuwezi kufaidika,” amesema Ndongo Malili, mkulima wa pamba kutoka Kijiji cha Mwakibuga.

Malili, aliyelima ekari tano msimu huu, amesema anatarajia kuvuna kati ya kilo 800 hadi 900 kwa ekari, lakini faida halisi itakuwa ndogo kutokana na kupanda kwa gharama za kukodisha mashamba, kulima na kununua pembejeo.


TCB: Tija ni suluhisho, si bei pekee

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Marco Mtunga, amesema suluhisho la kudumu kwa wakulima ni kuongeza tija katika uzalishaji badala ya kutegemea ongezeko la bei pekee.

“Kadri mkulima anavyovuna zaidi kwa ekari, ndivyo kipato chake kinavyoongezeka. Tunatoa wito kwa wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo ili kuongeza mavuno na hatimaye kipato,” amesema Mtunga.

Mtunga ameeleza kuwa mkulima anayevuna kati ya kilo 800 hadi 900 kwa ekari ana nafasi ya kupata faida zaidi ukilinganisha na yule anayevuna kilo 200 hadi 300.

Ametoa mfano wa mkulima bora wa msimu wa 2023/24 aliyepata kilo 2,750 kwa ekari, akisema ni ushahidi kuwa tija inawezekana.

Aidha, Mtunga amebainisha kuwa TCB inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kupitia maafisa ugani waliopo hadi ngazi ya kata, sambamba na kusambaza pembejeo kwa bei nafuu.

“Changamoto nyingine ni kushuka kwa ubora wa pamba baada ya mavuno. Hili linaathiri bei ya pamba yetu katika soko la kimataifa. Tunawahimiza wakulima kulinda ubora wa pamba kuanzia shambani hadi sokoni,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kihongosi, amesisitiza kuwa halmashauri, wakuu wa wilaya na viongozi wa vijiji wanapaswa kupewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa kilimo bora kwa karibu, ili kuongeza tija kwa wakulima na mapato kwa Serikali kupitia kodi na ushuru.

Ametoa agizo kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) na kampuni za ununuzi kubandika taarifa ya bei mpya kwenye vituo vyote vya ununuzi, ili kuepusha udanganyifu.

Pia, ametangaza marufuku kwa wanasiasa kujihusisha na usambazaji wa pembejeo za kilimo, ili kuondoa uwezekano wa kuzitumia kisiasa.

“Tuache siasa kwenye sekta ya kilimo cha pamba. Tuache wataalamu wafanye kazi yao kuongeza uzalishaji, tija na mapato ya mkulima,” amesema Kihongosi.


Wito wa Masoko Mapya

Mkulima Mashaka Matilanya kutoka Mwakibuga ameitaka Serikali kupitia TCB kutafuta masoko mapya ya kimataifa, ili pamba ya Tanzania iuzwe kwa bei ya ushindani itakayowanufaisha wakulima moja kwa moja.

“Bila soko la uhakika, wakulima hatutaweza kufaidika. Tunaomba Serikali isaidie bei ipande hadi angalau Sh2,000 kwa kilo msimu ujao,” amesema Matilanya.

Kwa sasa, zaidi ya wakulima 700,000 katika mikoa 17, wilaya 56 na halmashauri 64 wanajihusisha na kilimo cha pamba, sekta ambayo ina mchango mkubwa kwa uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.