Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nondo za Profesa Lumumba kwa nchi za Afrika

Mwanasheria nguli Afrika, Profesa Patrick Lumumba.

Muktasari:

  • Mwanasheria huyo nguli na mzungumzaji mahiri katika mihadhara mbalimbali, Profesa Patrick Lumumba, amesema nchi nyingi za Afrika zimepiga hatua kiuchumi, ila zinapaswa kuhakikisha uchumi wao unakua kwa kasi kubwa ili kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Arusha. Mwanasheria nguli Afrika, Profesa Patrick Lumumba, amezitaka nchi za Afrika kujitafakari juu ya hatua za kuchukua kuhakikisha zinakuwa nchi zilizoendelea kiuchumi.

Aidha, amesema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikijipongeza kwa hatua za maendeleo ya kiuchumi walizopiga, lakini zimekuwa ndogo mithili ya mwendo wa kinyonga na kobe.

Profesa Lumumba amesema hayo leo, Jumamosi Mei 3, 2025, akizungumza katika jukwaa la kiuchumi mkoa wa Arusha lililokutanisha wadau mbalimbali.

Akitolea mfano, amesema nchi kama Vietnam iliyopigana vita hadi mwaka 1975, ambayo kwa sasa ina wananchi wasiozidi milioni 50, ila uchumi wao ni mkubwa kuliko nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Tujiulize Wakorea walifanya nini wakapiga hatua? Vietnam hakuna jeshi la malaika waliotua kule kujenga Vietnam, ila walifanya kazi. Lazima tutafute fursa na kuziangalia kwa jicho chanya."

"Mfano, nchi za EAC tukipata wageni milioni mbili, iwe Kenya au Tanzania, tunasherehekea kwa nderemo na vifijo, ila nchi ya Singapore inapata wageni kwa mwaka wasiopungua milioni 30,” amesema Profesa Lumumba

Amesema licha ya nchi za Afrika kujitahidi kuwa nchi zilizoendelea kiuchumi, bado hazishirikiani ipasavyo katika fursa walizonazo.

“Mfano, Tanzania wana hifadhi nyingi za wanyama, lakini baadhi ya nchi za Afrika haziiipi kipaumbele katika kuzitembelea, na badala yake wengine wamekuwa wakienda nchi nyingine kuangalia wanyama kwenye bustani (zoo).

“Pia tuna bidhaa ambazo nchi zetu za Afrika zinatengeneza na kuzalisha, lakini bado tumekuwa tukiagiza mazao na bidhaa, ikiwemo tishu au vijiti vya meno kutoka nchi za Ulaya; huo ni unafiki, kutokutakiana maendeleo, ambayo itazidi kutuchelewesha katika kuendelea kiuchumi,” amesema.

Profesa Lumumba amesema ni muhimu Serikali za nchi za Afrika, zinapokuwa na fursa au miradi iliyopo maeneo ya vijijini, zihakikishe wananchi wanaozizunguka wananufaika.

Profesa Lumumba ametolea mfano akisema, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema siri ya maendeleo ni watu, ardhi na siasa safi.

“Alichokisema Mwalimu Nyerere bado kina umuhimu. Nchi zote ambazo zimeendelea zina watu ambao wamejitolea kuhakikisha wameboresha maisha ya watu, nchi hizo zina ardhi inayotumiwa kwa njia inayostahili, na zina siasa safi zinazounda mazingira wezeshi.

“Nyerere aliulizwa akasema tena, mbali na hayo matatu, siri nyingine ya maendeleo ni kuwa na vijana wenye malezi bora, siha njema na bongo kali. Tunapoungana katika kongamano hili kuna maswali nyeti ya kujiuliza; tumepiga hatua, lakini ni hatua za kobe na kinyonga.”

Kwa kuanzia, Profesa amezitaka nchi za EAC kupambana kuweza kujitegemea kwenye bajeti zao za maendeleo kwa kutumia rasilimali walizonazo, kuliko sehemu kubwa ya miradi ya maendeleo kutegemea ufadhili wa wahisani.

Akizungumzia jukwaa hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kuwa lengo ni kuwapa fursa wananchi wa Arusha kupata taarifa sahihi juu ya fursa za uwekezaji na biashara kwa ajili ya kuzichangamkia.

“Tumegundua kuwa watu wetu wengi wanafanya uwekezaji au biashara bila kuwa na taarifa sahihi. Mfano, anaona mtu fulani kafanikiwa, anatafuta taarifa ya anachofanya, na yeye anaenda kufanya biashara hiyo hiyo. Mwisho wanakuwa wengi, uhitaji unakuwa mdogo, na soko linashiba. Mwisho unasema biashara mbaya, mnaanza kulogana na kutafutana ubaya,” amesema.

Amesema kuwa lengo lingine ni kuwapa nafasi wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla kuzijua fursa za uwekezaji zilizotengenezwa na Serikali katika sekta mbalimbali ili wazichangamkie katika kujinufaisha kiuchumi.

“Hapa pia tunalenga wananchi wetu wajiulize kama fursa zinazotengenezwa na Serikali wanafahamu, au tunajua sisi viongozi pekee. Kama kuna ambazo hawazifahamu, wazijue hapa kupitia mawaziri wetu na waone fursa za fedha zilizojificha, wazichangamkie kupata pesa,” amesema Makonda.