Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Lumumba: Bila miundombinu soko huru Afrika halitafanikiwa

Profesa wa Sheria kutoka Kenya, Patrick Lumumba. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kukosekana kwa miundombinu bora kutaweka ugumu katika usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi za Afrika, jambo ambalo litakwamisha lengo la kuanzishwa kwa Soko la pamoja la biashara Afrika (AfCFTA).

Dar es Salaam. Profesa wa Sheria kutoka Kenya, Patrick Lumumba amesema ili Afrika iweze kufanikiwa katika mipango yake ikiwemo kuona matunda ya soko la pamoja la biashara Afrika (AfCFTA), ni lazima iwe na miundombinu ya uhakika ikiwemo barabara.

Miundombinu hiyo ndiyo itakayowezesha bidhaa kusafirishwa kirahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi tofauti na hali ilivyo sasa.

Profesa Lumumba ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 27, 2024 katika kongamano la Kimataifa la miundombinu lilioandaliwa na Chama cha Wahandisi washauri Tanzania (ACET) kupitia mwamvuli wa vyama hivyo Afrika, Fidic Afrika.

Akitumia dakika 24, mjuvi huyo wa masuala mtambuka, ameelezea kwa nini ni muhimu Afrika kufanya uwekezaji katika maeneo tofauti, ikiwemo miundombinu tena kwa kutumia wataalamu wake wenyewe, badala ya kutegemea wale wanaotoka nje ya nchini.

Amehoji akisema:  ‘’Bila kufanya uwekezaji nchi za Afrika zitawezaje kufanya biashara zenyewe wakati hazina miundombinu bora?

“Ili muweze kufanya biashara lazima muwe na miundombinu bora, soko huru la Afrika litakuwa na maana kama kutakuwa na miundombinu itakayosaidia ufanyaji biashara, hivi ndivyo tunafanya biashara,” amesema Profesa Lumumba.

Katika kufanikisha hilo amesema ni lazima kuangalia ikiwa zipo barabara zinazowezesha mtu kusafirisha bidhaa kutoka Ethiopia kwenda Senegal au mtu kusafirisha bidhaa kutoka Afrika Kusini kwenda Misri. Pia ni vyema kuangalia ikiwa upo mtandao wa reli ambao utawezesha bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Amesema tangu miaka ya 60 nchi nyingi za Afrika zilipopata Uhuru zilikuwa zikiahidi kuwa na barabara nzuri, reli, nishati ya uhakika jambo ambalo alihoji kama ahadi hizo zimefikiwa.

Badala yake alisema Afrika imeendelea kusalia nyuma katika mambo mengi huku akitolea mfano suala la mtandao, kwa kile alichoeleza kuwa mtu anaposafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine lazima atahangaika kwa sababu ya kutokuwapo kwa miundombinu inayowezesha mtu kutumia mtandao wa nchi yake katika eneo analokwenda.

“Safari ya saa moja kutoka Nairobi hadi kufika Tanzania nilihangaika na mtandao, mtu akitoka Botswana kwenda nchi nyingine atahangaishwa na mtandao,” amesema Profesa Lumumba.

Ametaka nchi za Afrika kujitafakari na kuangalia ikiwa zina uwezo wa kutumia rasilimali zake za ndani, ikiwemo wataalamu wake kufanya vitu inavyotaka kufanya.

Amesema amekuwa akiona miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwemo barabara zinazojengwa maeneo tofauti kama Nairobi, Tanzania ikiwa chini ya Wachina huku akihoji kuwa ni kitu gani kimetokea kwa wahandisi wa ndani.

“Tunaendelea kutegemea wengine, tunaendelea kutegemea uvumbuzi kutoka kwa wengine, tunao wataalamu wanaozalishwa na vyuo vyetu wanakwenda wapi?” amehoji Profesa Lumumba na kuongeza:

“Hivi ndiyo vitu vya kuzingatia katika mkutano huu kama si hivyo bara hili litaendelea kuwa tegemezi kwa wengine,” aliongeza.

Alichosema Makamu wa Rais

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa mgeni rasmi,  amesema nchi nyingi za Afrika hivi sasa zinatekeleza miradi mbalimbali ya maendelo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya reli, uzalishaji umeme na barabara.

Hata hivyo, pamoja na jitihada zote zinazofanywa, nchi nyingi za Afrika na serikali zake zimekuwa zikikutana na changamoto zinazohusiana na wahandisi washauri ikiwemo rushwa katika zabuni za kazi mbalimbali.

Pia amesema kumekuwapo na ongezeko la gharama za miradi, jambo ambalo alitaka suluhu ya pamoja kutafutwa katika changamoto hizo.

“Pia tuangalie suala la baadhi ya wahandisi washauri kushindwa kufikia vigezo vya soko la ajira, jambo ambalo limefanya wahandisi wengi wanaotumiwa kuwa wa nje ya nchi,” amesema Dk Mpango.

Ili kuacha kutumia wataalamu kutoka nje, Naibu Waziri wa Ujenzi wa Tanzania, Godfrey Kasekenya, amesema umefika wakati wa kuangalia namna ya kutengeneza wahandisi washauri wazuri ndani ya nchi na bara la Afrika, ili kuacha utegemezi wa wataalamu hao kutoka nje ya nchi.

“Lengo ni kazi nyingi zifanywe na Watanzania kwa sababu hata kukiwa na miradi mingi inayotekelezwa nchini,  lakini ikifanywa na watu wa nje,  fedha nyingi zitakwenda nje,” amesema Kasekenya.

Kwa upande wake, Rais wa Fidic Africa, Abe Thele amesema,  uwekezaji katika miundombinu ni suala lisilokwepeka kwani tafiti mbalimbali zinaonyesha hali si nzuri hasa maeneo ya vijiji.

“Ni asilimia 30 pekee ya barabara za vijijini ndiyo zinaweza kupitika vipindi vyote, hivyo ipo haja ya kufanya uwekezaji zaidi katika miundombinu,” amesema Thele