Katiba ni ya watanzania sio ya wanasiasa wa Tanzania

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba (katikati) akiwa pamoja na aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, Dk Salim Ahmed Salim (kushoto) na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa (kulia).
Muktasari:
Watanzania walio wengi wanayatazama makundi yote mawili lile la Ukawa na lile la Tanzania kwanza (CCM) yanayounda Bunge maalumu la Katiba kama yenye ubinafsi na yaliyosahau jukumu walilopewa na wananchi, la kuwapatia Katiba mpya.
Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wamegawanyika vipande viwili. Kipande kimoja kiko Dodoma kikiendelea na mchakato wa kujadili upatikanaji wa Katiba mpya.
Kipande kingine cha wajumbe wanaounda Bunge hilo maalum kimeendelea na na msimamo wake wa kugomea mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba hadi watakapokubali kuheshimu maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba.
Kipengele kinacholeta mzozo ni muundo wa serikali ambapo kundi linaloundwa na upande wa CCM linasimamia kwenye muundo wa muungano wa serikali mbili badala ya tatu zilizo katika rasimu hiyo.
Watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wametoa ushauri wao kwa wajumbe wa Bunge hilo maalumu la Katiba wakiwataka kutumia busara zaidi badala ya nguvu katika kutekeleza jukumu hilo lililopo mbele yao.
Mbali na viongozi wa vyama vya siasa, wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida vile vile wamekuwa na maoni, ushauri na maombi yao kwa wajumbe hao kurejea misimamo yao na kutazama mzigo waliopewa na wananchi
Wakati Bunge likiendelea watu wa kada mbalimbali, wasomi kwa wasiosoma, wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima, wote kwa ujumla wao neno lao ni moja kuwa watanzania wanataka Katiba itakayotokana na maoni na mapendekezo yao waliyoyatoa katika Tume ya warioba.
Ujumbe huo wa watanzania umeelekezwa moja kwa moja kwa makundi yote mawili yanayounda Bunge maalum, lile linalounda Ukawa na lile linalobebwa na Chama tawala CCM.
Watanzania walio wengi wanayatazama makundi yote mawili lile la Ukawa na lile la Tanzania kwanza (CCM) yanayounda Bunge maalumu la Katiba kama yenye ubinafsi na yaliyosahau jukumu walilopewa na wananchi, la kuwapatia Katiba mpya.
Kwamba makundi hayo yamewaweka kando wanaowawakilisha na kuamua kujiwakilisha wenyewe na vyama vyao. Kwamba mchakato unavyoonekana sasa ni kuwa umetekwa na wanasiasa kila kimoja kikilenga kujinufaisha.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na Katiba wanasema kinachoonekana kukwamisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ni ubinafsi wa wanasiasa na kwamba kinachopaswa kufanyika ni kwa wanasiasa wote waliopo ndani ya Bunge hilo maalumu kujivua uanasiasa wao na kubaki na Utanzania.
Kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waweke pembeni upenzi, ushabiki na ukereketwa wa yale makundi yaliyowapeleka bungeni na kubakiza utanzania na uwakilishi wa wananchi.
Buberwa Kaiza, Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora nchini, anasema, wajumbe wa bunge maalumu wanapaswa watambue jambo moja kuwa wanawawakilisha wananchi na sio kujiwakilisha wenyewe au vyama vyao.
Buberwa akizungumza katika kipindi maalum kilichorushwa hewani la luninga ya ITV anasema kikubwa kinachopaswa kuzingatiwa na wajumbe hao ni kuwaangalia watanzania kwanza wanataka nini na kusahau kuhusu nafasi zao za kisiasa.
Anasema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa ujumla wao wajue kuwa wao kama wawakilishi wa wananchi, na sio wa chama chochote cha siasa, jukumu lao ni moja tu, kuwapatia wananchi Katiba yao.
Anaongeza kuwaasa wajumbe wa Bunge maalum la Katiba, waache makundi na mawazo ya kuibuka washindi au washindwa na badala yake wawaangalie wale wanaowawakilisha wanataka nini na wamewatuma nini.
“Wajumbe wa Bunge Maalum wanapaswa kuzingatia kile kinachotakiwa na wananchi…wasifikirie kushinda au kushindwa kwasababu hakuna kundi la ushindi…unapowaza kushinda na kushindwa hapo hakutakuwa na Katiba” anasema.
Kaiza anasema bila kujali wanatoka katika kundi lipi, wajumbe wa Bunge Maalumu kwa ujumla wao wanalo jukumu moja tu ambalo ni kuhakikisha wanazingatia maudhui ya Katiba bila kutoka kwenye rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Warioba.
“Wajue wanawawakilisha wananchi na waangalie wananchi wanataka nini…wajue kuwa maoni ya wananchi ndio msingi unaopaswa kulindwa” anasema.
Kaiza anasema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakae kama taifa lenye koo moja na nia moja ambayo ni kuwa na makubaliano na sio kushindana na kupata mshindi na au mshindwa.
Ushauri wa aina hiyo ulitolewa mapema na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ambaye alipozikutanisha pande mbili zinazoundwa na wajumbe hao wa Bunge Maalumu aliwataka watumie busara zaidi.
Mutungi alisema hatima ya Watanzania ya kupata Katiba Mpya itategemea busara za viongozi wa vyama vya siasa.
“Ninavyoona mimi, hapa hatima ya Watanzania ya kupata Katiba Mpya itategemeana na busara za viongozi wetu wa vyama vya siasa pekee na si kitu kingine” anasema na kuongeza kuwa..
“Yote haya yanaweza kumalizika ikiwa busara itatumika... kwa viongozi wa vyama vya siasa, kwa kila chama, kuweka mbele busara na utaifa kwanza na mchakato utaendelea vizuri,” anaongeza Jaji Mutungi.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Kituo cha msaada wa sheria kwa wanawake (WLAC) Juvenal Rwegasira anasema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katba wanapaswa wajue jukumu lililowapeleka bungeni ni kuwawakilisha wananchi ili ipatikane Katiba yenye manufaa kwa wananchi wote na sio kundi Fulani katika jamii.
Naye Mwanasheria wa kituo cha Haki Ardhi, Joseph Chombola anasema bunge hilo maalumu la Katiba linalo jukumu ya kutumia nafasi lililo nayo kujadili kwa uwazi na kutimiza wajibu wake wa kuwawakilisha vyema wananchi.
Anasema kinachoonekana sasa ni kuwa mchakato mzima umehodhiwa na wanasiasa. “Muundo wa upatikanaji wa wajumbe unaonekana wazi kuwa ulikuwa na hitilafu, idadi kubwa ya wajumbe ni wanasiasa.
Katiba ni ya watanzania sio ya wanasiasa wa Tanzania
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule ya Sheria ya Kenya (KSL), Profesa Patrick LumumbaPatrick anasema ili mchakato uende sawa na uje na matokeo chanya, wanasiasa wakiwa kule wasahau u-ukawa wao, wajue wao ni watanzania, wasabau uCCM wao wajue wao ni watanzania, na wanatafuta Katiba ya watanzania wote na sio ya vyama vyao.
Anasema nchi za Afrika Mashariki zilipata katiba zao kwa njia ya machafuko, hivyo Tanzania lazima itafute njia sahihi inayokubalika kwa wananchi wote.
“Tanzania ndio itakuwa nchi ya mwisho katika Afrika Mashariki kupata Katiba, kwa hiyo, muhakikishe makosa yaliyofanyika Kenya hayajirudii hapa...., piteni njia sahihi, hili ndio jambo la busara” anasema.
Profesa Lumumba vile vile akawakumbusha Ukawa kuwa zipo njia tofauti tofauti ya kuwasilisha ujumbe, ya kwanza ni kupambanisha hoja kwa hoja, kuna kupiga kura na wakati mwingine ni kuondoa kwenye mkutano.
“Lakini kujiondoa huko ni hatua ya mwisho na sio ya kwanza..... na” anasema.