Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamlaka za maji zitafute njia mbadala kuzidai taasisi za umma

Mkurugenzi mtendaji wa Souwasa, Patrick Kibasa akieleza mikakati iliyopo kuhakikisha wananchi wengi zaidi wa Manispaa ya Songea wanaunganishwa kwenye mtandao wa majisafi na salama. Picha na Joyce Joliga.

Muktasari:

  • Mkurugenzi mtendaji wa Souwasa, Patrick Kibasa anasema taasisi za Serikali hazilipii huduma kwa wakati na mpaka Januari zilikuwa zinadaiwa Sh618.20 milioni hivyo kuifanya mamlaka hiyo ishindwe kulipa baadhi ya gharama za uendeshaji kwa wakati.

Kukabiliana na ucheleweshaji wa malipo ya ankara za maji unaofanywa na taasisi za umma, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea (Souwasa), imeanza kuzifungia maalumu za malipo ya kabla.

Mkurugenzi mtendaji wa Souwasa, Patrick Kibasa anasema taasisi za Serikali hazilipii huduma kwa wakati na mpaka Januari zilikuwa zinadaiwa Sh618.20 milioni hivyo kuifanya mamlaka hiyo ishindwe kulipa baadhi ya gharama za uendeshaji kwa wakati.

Kukabiliana na changamoto hiyo, anasema: “Mamlaka imeanza kuzifungia taasisi za Serikali mita za kulipia huduma kabla ya kutumia (prepaid meters) na tayari mita 72 zimeshafungwa ili deni lisiendelee kuongezeka.”

Souwasa si mamlaka pekee inayozidai taasisi hizo deni kubwa. Akizindua Mradi wa Maji wa Ruvu, Juni mwak ajana, Rais Johna Magufuli aliitaka Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kusitisha huduma zake kwenye taasisi ambazo hazilipi bili.

Mpaka wakati huo, Dawasco ilikuwa inadai kiasi cha Sh40 bilioni huku yenyewe ikidaiwa Sh8 bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Madeni ya taasisi hizi kutokana na kutolipa kwa wakati bili za nishati tofauti inazotumia imekuwa kero ya muda mrefu. Licha ya maji, madeni mengine yapo kwenye umeme pia.

Mpaka Januari mwaka 2016, Tanesco ilikuwa inazidai taasisi za Serikali kiasi cha Sh129 bilioni, kati ya hizo Sh70 bilioni inadaiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Aidha, wateja binafsi na kampuni mbalimbali zilikuwa zinadaiwa Sh104 bilioni.

Mkakati huo wa Souwasa unatekelezwa wakati mamlaka hiyo ikiongeza usambazaji wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea baada ya kukamilika kwa mradi wa kuvuna maji katika Bonde la Mto Luhira.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa Mei 2016 kwa fedha za Serikali umekuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita 9,000 za ujazo hadi 10,500 kwa siku hivyo kuongeza idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa maji safi na salama.

Songea

Katika jitihada za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata majisafi, mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga Sh1.37 bilioni kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi ili kuhudumia maeneo ambayo hayajafikiwa.

Kukamilika kwa mradi huo kumeyanufaisha maeneo ya Ruvuma Darajani, Madizini, Lizaboni, Ruhuwiko Shuleni, Msamala kwa Gasa, Mkuzo Kwa Nchimbi, Mkuzo Sapientia na Mkuzo Maliasili ambako jumla ya wateja wapya 1,181 wameunganishwa katika mtandao wa majisafi na salama.

Wateja hao wameunganishwa kutokana na ushirikiano unaofanywa kati ya Souwasa na mkandarasi. Ushirikiano huo pia umeshuhudia mabomba yenye urefu wa kilomita 79.7 yakitandazwa mmjini Songea.

Mkurugenzi mtendaji wa Souwasa, Kibasa anasema kutoa fursa kwa wananchi wengi kupata huduma hiyo, mamlaka ilitoa punguzo maalumu kwa wateja wanaotakiwa kulipa gharama husika ndani ya miezi sita.

“Hii ni katika kuhakikisha wananchi wengi wa Manispaa ya Songea wanapata majisafi inayotolewa na Souwasa kwa kuzingatia kipato cha Mtanzania,” anasema.

Kutokana na mradi huo uliofika wananchi wameondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji au kutumia maji yasiyo salama ambayo huongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa hasa ya matumbo.

Kibasa anasema, kwa sasa asilimia 80 ya wananchi wa manispaa hiyo wameunganishwa lakini mpango uliopo nikuwafikia asilimia 95 hadi mwaka 2020.

Kuhakikisha upatikanaji wa maji unakua endelevu, anasema mamlaka hiyo inahakikisha vyanzo vya vilivyopo vinatunzwa pamoja na kutafuta vingine, vipya.

Kuhakikisha hilo, anasema jumla ya miti 2,500 imepandwa katika Bonde la Mto Luhira na zaidi ya mingine 5,000 inategemewa kupandwa katika vyanzo vya Mlima Matogoro baadaye mwaka huu.

Wananchi

Mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Madizini mjini Songea, Salome Haule anasema baada ya kusota kwa muda mrefu hatimaye ameunganishwa kwenye mtandao wa majisafi kwa gharama nafuu.

“Nimeikosa huduma kwa kwa muda mrefu hali iliyonifanya niione Serikali imenitenga lakini kwa sasa nimefarijika. Kuna ndoa zilikuwa na migogoro iliyotokana na muda mwingi unaopotezwa kutafuta maji,” anasema Salome.

Mkazi wa Mjimwema, Joyce Mbawala anasema maji ni uhai na ni kila kitu kwa maisha ya binadamu hata wanyama kwani unaweza kukosa huduma nyingine ukatafuta namna ya kukabiliana na upungufu lakini lakini si maji.

Anasema amepata faraja baada ya kuunganishiwa maji ya bomba nyumbani kwake hivyo kuondokana na foleni ndefu za kusubiri maji maeneo ya mbali alilkokuwa analazimika kuyafuata.

“Muda tuliokuwa tunaupoteza kutafuta maji sasa tutautumia kufanya mambo mengine hivyo kupiga hatua ya maendeleo,” anasema Joyce.

Wakati wananchi wakifurahia haki hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Souwasa, Kibasa anasema upo mwingine utakaokamilika hivi karibuni ambao utaongeza uzalishaji wa maji kutoka mita 10,500 za ujazo mpaka 13,740 kwa siku hivyo kuongeza idadi ya wanaonufaika.

“Mradi huo umegharimu Sh360 milioni ambazo, kati yake, Sh300 milioni zimetolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maji na Sh60 milioni zimetolewa na Souwasa,” anasema mhandisi huyo wa manispaa.

Vilevile amesema Mamlaka imepanga kuendelea kupanua mtandao wa majisafi kwa mapato yake yenyewe na mikopo ya gharama nafuu ili kuwafikia wakazi wa Manispaa ya Songea ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo.

Changamoto

Licha ya mafanikio hayo, mamlaka hiyo bado ina changamoto inazokabiliana nazo ambazo ni pamoja na kufikisha huduma eneo maalum la eka 5,000 lililotengwa kwa ajili ya viwanda.

Kibasa inatafuta fedha za kusogeza mtandao wa majisafi katika eneo dogo linalotegemea kuanza kutumika wakati inasubiri uwekezaji mkubwa unaotegemewa kufanywa na Serikali ambao utahusisha ujenzi wa bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi mita milioni tano za ujazo na uboreshaji wa miundombinu ya majisafi.

Licha ya mipango hiyo ya ujenzi, Kibasa anawaasa wananchi wa Manispaa ya Songea kuilinda miundombinu hiyo ya maji kwa kuwa inajengwa kwa fedha nyingi na kuwataka kulipia ankara zao kwa wakati ili mamlaka iendelee kuboresha na kuongeza idadi ya wananchi wapya wanaounganishwa.

Licha ya wateja wapya wanaounganishwa, anasema mahitaji huenda yakaongezeka kutokan ana viwanda vinavyotarajiwa kujengwa kuchakata malighafi muhimu kama madini na mazao ya kilimo yanapatikana mkoani Ruvuma.

Kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji kupitia Bandari ya Ziwa Nyasa na barabara za lami zinazounganisha mkoa huo na inayouzunguka, wananchi wanaweza kufanya biashara na kuimarisha kipato chao.