Asha Baraka 'The Iron Lady' asiyekubali kushindwa

Dar es Salaam. Desemba 17 mwaka jana, bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, African Stars ‘Twanga Pepeta’ ilizindua albamu yake ya 15 ‘Twanga Pepeta Forever’ ikiwa ni miaka 24 imepita tangu kuanzishwa kwake.

 Bendi hiyo imeendelea kutikisa anga za burudani ikiwa chini ya mwanamama nguli na mashuhuri, Asha Baraka ambaye Januari 29 mwaka huu, alichaguliwa tena kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba katika Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.

Miongoni mwa wasanii machachari waliotikisa katika bendi hiyo ambao wameshatangulia mbele ya haki ni Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, Abuu Semhando, Adolf Mbinga, Khamis Kayumbu ‘Amigolas’, Soud Mohamed ‘MCD’, na wanenguaji machachari Aisha Madinda na Halima White.

Hata hivyo, bado kuna wakongwe wengi ndani ya bendi hiyo, akiwemo Luiza Mbutu, Ali Choki, Super Nyamwela na Chaz Baba. Licha ya bendi hiyo kudumu imekuwa na panda shuka zilizoitikisa kwa kipindi fulani. Asha Baraka amefanya mahojiano ya kina na Mwananchi ambapo ameelezea ugumu wa kuendesha bendi ya muziki wa dansi Tanzania.

“Kuendesha bendi ya muziki wa dansi kuna changamoto nyingi, inahitaji uvumilivu ndani ya kazi, kwani kuna kipindi inaingiza pesa na siku unakosa, sasa huwezi kuanza kusema ooh mimi naacha, lazima ujiulize kwa nini unakosa na unatakiwa kufanya nini ili upate kama jana,” anasema.

Anasema kuna nyakati vifaa vya muziki vinaweza kuungua ghafla ni lazima kuhakikisha vinanunuliwa vipya ambavyo ni gharama. “Mkapambana na vifaa vya muziki wa dansi, mmeshatengeneza nyimbo tayari mmebuni mnataka kurekodi video mliyemshirikisha akatoka akaenda bendi nyingine.

“Au akapatikana mtu anataka kufanya hiyo biashara akaja akakuchukulia wanamuziki zaidi ya 10, ni changamoto ambazo zinakukuta, ukichukuliwa wanamuziki 10 ukiwa na roho nyepesi unakata tamaa, unasema mimi muziki basi,” anasimulia. Licha ya kupata changamoto kutoka kwa washindani wake, Asha Baraka anasema hakuna kazi ngumu kama kulea wasanii, iwe waimbaji, wanenguaji au wapiga vyombo kwa kuwa asilimia kubwa hupenda usasa, hivyo ni rahisi kuingia katika magenge yasiyofaa.

“Wanaweza kushauriana mazuri au mabaya na wakaingia wengine hata kwenye mambo ya kutumia bangi au dawa za kulevya, msimamizi anakutana na hizo changamoto sana, kwa hiyo anasimamia kwa kuwa tunataka wanamuziki wa Kitanzania ambao wanapata ajira, siyo kwamba hatutaki wageni, ila tunapunguza ajira za Tanzania,” anasema. Asha anasema aliendelea kukomaa na bendi ili kutositisha ajira za wanamuziki 60 ambao aliwataja kuwa ni wengi na inapunguza vijana kuzurura mtaani, huku akisema kwa sasa bendi hiyo ina wanamuziki 38.

Anasema lengo la Twanga Pepeta lilikuwa kufanya muziki wa kimataifa, hivyo jitihada ilikuwa ni kutafuta masoko ya nje, kama bendi iliwekeza zaidi kufanya shoo nje ya nchi.

“Tuliweza kuingia kwenye tamasha la Oman linalofanyikia Oman kama mara tano na tumepata tuzo, hayo ni maonyesho makubwa ya biashara yanayokutanisha wasanii mbalimbali pia zaidi ilikuwa muziki wa kizazi kipya.”

Anasema ili kuhakikisha wanafanikiwa katika soko la muziki wa dansi kimataifa walienda nchi mbalimbali, ikiwemo Sweden, Norway, Uholanzi ambako huko kote waliwapata mashabiki wachache chini ya 50, huku wakitumia fedha zao za mfukoni. “Unaingia ukumbini mashabiki hawafiki 50, tulienda kwa nguvu zetu wenyewe tukishirikiana na Mtanzania mmoja anayeratibu ile shughuli, tunatumia pesa nyingi, lakini hairudi, ili wanamuziki wale wapate posho utatumia milioni 50 na tiketi, ile pesa hairudi, utatumia hiyo inarudi milioni 10 na milioni 40 unapoteza,” anafafanua.

Asha anasema bendi ya Twanga Pepeta imefanya maonyesho matatu nchini Uingereza, huku shoo ya kwanza ikipigwa uwanja mkubwa wa mpira ambayo ilipokelewa vizuri na mashabiki na bendi haikupata hasara wala faida.

Shoo ya pili hawakupata faida wala hasara na shoo ya tatu walienda kutumbuiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania wakishirikiana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza ambapo bendi ilijigharamia yenyewe.

“Shoo ilikuwa nzuri, tulitengeneza pesa, lakini hatukupata hasara wala faida, lakini tulikuwa tunaijenga Twanga Pepeta isimame kimataifa. Nchi kama Kenya tumeenda na kufanya shoo kwa miaka miwili mfululizo, hizo zote ziliisaidia Twanga Pepeta kujitangaza,” anasema.


Miaka 24 ya Twanga

Asha anasema miaka 24 kuongoza bendi haikuwa kazi rahisi na kwake anaamini si katika burudani pekee, bali kitu chochote kama mwanamke lazima awe na malengo, juhudi ili kile unachotaka kufanya kifanikiwe.

“Burudani nimefanya muda mrefu, kwa sasa nakaribia kukamilisha miaka 25, nilianza kidogokidogo na nikajipanga ili shughuli zangu zisikwame. “Sikuanzia huko, kwanza nilikuwa mchezaji wa netiboli, mwaka 1994 nilijiongeza nikaanza kujifunza vitu vidogo vidogo, nilianza rasmi burudani mwaka 1998 na nikaanza kujikita huku baada ya kuangalia ubora wake na changamoto zake. “Nilianza taratibu na mwaka 1999 nikajikita kwa mara ya kwanza nikatafuta njia gani ya kuweza kupata vyombo vya muziki, pale ndiyo nilipata nyenzo zote, nikawachukua kina Lwiza Mbutu, Adolf Mbinga, marehemu Abuu Semhando, marehemu Soud Mohamed ‘MCD’ na Amigolas, ndio walikuwa vinara,” anasimulia.

Anasema mwaka 2000 aliingiza kundi lililotoka Billbums la wanenguaji, anayependa kuwaita waburudishaji na wanogeshaji akiwemo Super Nyamwela, Aisha Madinda na Halima White na wengine wakaongezeka, lilianza kidogo kidogo, baadaye likawa na watu 10 ambao ndio walinogesha zaidi bendi.

Asha anasema wanamuziki walikuwa wanaingia na kutoka, lakini kupitia kwa mastaa kama Luiza Mbutu, Banza Stone, Deo Mwanambilimbi na marehemu Joseph Watuguru lilitungwa jina la Twanga Pepeta na Banza ndiye alilinogesha zaidi jina likapata umaarufu, baadaye zikaingia simu zikapewa jina la Twanga Pepeta na hapo ndipo likajizolea umaarufu.

“Muziki ni ajira na unalea familia, hata mimi watoto wangu wamekua kupitia muziki, kwa mfano mimi licha ya kwamba ni mfanyakazi wa shirika la taifa la bima bado nilisimamia bendi.

“Nimetengeneza wanamuziki kumtoa sehemu fulani kwamba wewe utakuwa mwanamuziki imba, huwa nasimamia mpaka studio na naelekeza ila na msanii uwe na ubunifu na mimi nakuwa na ubunifu wa asilimia 50 kwamba nataka wewe Msafiri Diouf imba Safari,” anasema.


Kudumu kwa Luiza

Asha anamzungumzia Luiza Mbutu kama mfano wa kuigwa, “Nina watu wawili niliowabeba sana, Jesca Charles na marehemu Aisha Madinda, hawa walikuwa waandamizi ndani ya Twanga na nikajaribu kumuongeza Khadija Mnoga ‘Kimobitel’, lakini alishindwa kwa kuwa hakuwa na msimamo.

“Lakini Luiza Mbutu siyo mtu wa papara, huwa anaangalia sisi ni wasanii tunatafuta nini na nilimpa kuwa kiongozi wa bendi hajawahi kuangusha jahazi miaka na miaka, maana unaweza kupewa jahazi ukaliangusha naenda kuanzisha, waweza kuanzisha chako kisisimame, kwa hiyo vitu vya msingi vyote alikuwa anavisimamia, anaipenda kazi yake na ana nidhamu ya kazi,” anasema.

Anasema kutokana na nidhamu yake ya kazi kwa sasa amechaguliwa kama Rais wa chama cha muziki Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha muziki wa dansi Tanzania (Chamudata) kwa kuwa wamemuona ana msimamo na kwamba Twanga Pepeta kwa sasa ni Mkurugenzi.

Akimwelezea zaidi anasema familia ya Luiza na yake zimejenga udugu kwa kuwa amekuwa naye muda mrefu huku wakipanga pamoja mikakati ya kuisimamia bendi hiyo.

“Baadaye akapata ndoa imesimama vizuri na ana mtoto mmoja ambaye ni mkubwa. Unapomzungumzia Luiza katika tasnia ya muziki wa dansi lazima umzungumzie na msimamo wake,” anasema.


Ngoma tano bora

Aisagia bongofleva

Wakati muziki wa dansi miaka ya zamani ulitamba, Asha Baraka anasema walisaidia kwa kiwango kikubwa kuusukuma muziki wa bongo fleva nao ujulikane, lakini kwa sasa wasanii wa upande huo hawataki kutoa ushirikiano.

“Ukienda nje unaambiwa tunataka mwanamuziki wa Tanzania, tuliwahi kumratibu Mr Nice kwenda Nairobi, Dully Sykes mara mbili kwenda Uholanzi na Uingereza.

“Hatukuwahi kuwa na choyo lakini utakuta wakati tunaanza kina Mr 11 Sugu, tukiwa tunapiga wanakuja mpaka ikatungwa rapa ya ‘Twanga Pepeta Sugu, Mr Two Sugu’ aliileta yeye akaimba Ali Choki, tuliwashirikisha kipindi kile… “Bongo Fleva wa sasa hivi wana choyo na muziki wa dansi hawataki kushirikisha wanamuziki wa dansi kwenye muziki wao, lakini wakisahau kwamba wao pia wakati wanataka kutoka walitumia majukwaa ya Twanga Pepeta, ikiwemo Leaders na maeneo mengine,” anasema na kuongeza;

“Ninataka kuwaambia Bongofleva sisi sote ni wasanii, umepata bahati umekuwa juu, umejiweza kwa nini unasahau hata kwamba ulitumia jukwaa la Twanga Pepeta kupanda, kwa nini usiwaite ukawasaidia.” Asha anasema Twanga Pepeta ni daraja, wasanii wengi wamepita ambao wana mafanikio, hivyo wakumbuke walikoanzia na walikotoka na kuwainua waliokuza muziki wanaoufanya sasa.

sisi tutaendelea kusimama palepale.”


Huyu ndiye Asha Baraka

Licha ya wengi kumfahamu kupitia muziki wa dansi, mwanamama huyu amejizolea umaarufu katika maeneo makuu mawili, ikiwemo katika siasa na soka.

Tofauti na anavyoonekana, ukiingia nyumbani kwake utapata kumjua yeye ni nani pamoja na historia ya maisha yake kulingana na picha kadhaa kubwa zilizonakshiwa vema zinazotunza kumbukumbu ya maisha yake tangu akiwa binti mbichi akicheza mpira wa netiboli. Uchezaji wake ulimpa umaarufu hadi kutamba na timu ya Bima.

Picha hizo zinamuonyesha kadiri umri wake ulivyoendelea kusogea sambamba na picha za watoto wake tangu wakiwa wadogo.

Asha anasema licha ya kufanya shughuli za muziki ambazo ni mchana na usiku, hakusahau familia wala kumcha Mungu wake, kwa kuwa kila ifikapo Ijumaa ni siku ambayo hatoki nyumbani na atakwenda kuswali na kurejea tena.

“Nikiwa nyumbani nakuwa mama na mtu wa kawaida kabisa, naingia jikoni kama kinamama wengine na najua wajibu wangu kama mzazi, nini kifanyike nahakikishe mambo yote yapo sawa,” anasema.

Kwa wanaomfahamu Asha Baraka wanajua namna anavyojua kusimamia hoja, lakini wengi wanamchukulia kama mkorofi hapa anafafanua;

“Kila mtu atanihukumu anavyoweza, binafsi nasimamia kile ninachokiamini ni bora kwangu na kwa watu wengine ilimradi simtukani mtu, simpigi mtu wala sivunji sheria yoyote ya nchi.

“Lakini ukiwa unajitoa kufanya vitu vingi lazima utapewa jina, ukiwa mwanamitindo utaambiwa malaya, wanasema Asha mkorofi ni sawa ili nisipate wanaume wakaja kunitongoza kila wakati, maana ukiwa mrahisi kila mtu atakufuata, bora wakuchukulie mkali ilimradi unafanya yako na shughuli zako haziharibiki,” alisema.

Licha ya hulka ya tabia yake hiyo, Asha anasema ndio maana hata katika mavazi amekuwa ni mtu wa kubadilika. “Navaa kufuatana na naenda kwenye shughuli gani, nikienda ya dini ninakuwa Hajat, nikienda shughuli ya harusi nina mavazi yangu, siasa, mpira mavazi ya mpira, kwenye mavazi mimi sieleweki, inategemea naenda kufanya nini,” anasema. Licha ya shughuli zake zote, Asha anasema hakuwa mtu wa kukesha kwenye bendi, kwani mara nyingi alikaimisha shughuli zake kwa viongozi wa bendi. “Kabla sijaweka uongozi nilikomaa mwenyewe, baadaye nikawa siendi usiku, lakini nahakikisha kila kitu kipo sawa, ninaweza kuonekana mara moja au nisionekane kabisa, zamani nilikuwa nafanya kazi Shirika la Bima ya Taifa, nilikuwa bado msichana, mwanamuziki kachukuliwa huku napambana kule,” anasimulia.


Soka

Pamoja na mambo mengine, Asha Baraka amejikita kwenye mpira wa miguu ambapo pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, lakini akiwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya klabu ya soka la Wanawake Simba Queens, iliyotwaa mara tatu mfululizo taji la Ligi Kuu (WPL).

“Tangu nimeingia kwenye bodi, Simba Queens inafanya vizuri, tunashirikiana wote pamoja na wanachama tumefanikiwa, kwani tuliishia robo fainali. Tumepambana na tumeweza kushinda Afrika Mashariki na kati tumesogea mbele mashindano ya CAF na kumaliza nafasi ya nne ikiwa timu ya kwanza ya Afrika Masharika kufika nusu fainali ya michuano hiyo mipya Afrika.