Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walimu, wafanyakazi shule ya CCM watishia kuacha kazi

Askari Polisi wakiwa wametanda shule ya Sekondari Ivumwe baada ya taharuki kwa watumishi kupinga kuondoka kwa Mkuu wa Shule hiyo, Oscar Mwaihabi

Muktasari:

  • Shule hiyo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa ambapo Mwaihabi amehudumu kwa takribani miaka miwili, huku akisimamia ujenzi wa madarasa manane, maabara tano za kisasa na kuongeza ufaulu shuleni hapo.

Mbeya. Hali ya taharuki na sintofahamu imetokea katika Shule ya Sekondari Ivumwe baada ya watumishi zaidi ya 40 kutishia kugoma wakipinga kuondolewa kwa Mkuu wa shule hiyo, Oscar Mwaihabi.

Kufuatia mvutano huo, Jeshi la Polisi lilifika shuleni hapo ili kuhakikisha ulinzi na usalama wakati kikao cha Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na bodi ya shule kilipokuwa kikiendelea kujadili taharuki hiyo.

Mwananchi Digital imemtafuta kwa simu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Mbeya, James Mwapondele azungumzie kadhia hiyo, ambapo amesema hana taarifa za taharuki hiyo.

Amesisitiza kuwa hakuna jambo lolote linalofanywa ndani ya chama kinyume cha utaratibu.

Hata hivyo, amesema mabadiliko kama hayo ya kumuhamisha mtumishi ni uamuzi wa muajiri ambaye huwa anayafanya kwa nia njema inayolenga kuongeza ufanisi katika eneo jingine la kazi.

"Sina taarifa kuhusu taharuki hiyo, lakini hakuna jambo lisilo la kisheria linalofanywa ndani ya chama. Huenda mwajiri ana nia njema ya kumpanga sehemu nyingine kwa masilahi makubwa zaidi. Kwa sasa sina taarifa kamili, naomba nilifuatilie," amesema Mwapondele.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana shuleni hapo leo, watumishi waligoma kushiriki kikao kilichokuwa kinaendelea, wakidai hoja zao hazikusikilizwa na hawakukubaliana na mchakato wa mabadiliko hayo.

Selestine Mtweve, mmoja wa watumishi wa shule hiyo, amesema hawako tayari kufanya kazi na mkuu mpya aliyeteuliwa kwa sababu wana taarifa zisizoridhisha kuhusu alikotoka, na wanaiomba Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa kupitia Katibu Mkuu Ally Hapi kufuta mabadiliko hayo.

"Tuko zaidi ya watumishi 40, mabadiliko haya yamekuja ghafla. Mwaihabi ametumia akili na ushawishi wake kubadilisha shule hii, ufaulu umepanda, tunaona madarasa manane na maabara za kisasa," amesema Mtweve.
"Hatuko tayari kufanya kazi na mtu mpya. Tunaomba Katibu Mkuu Hapi atengue mabadiliko haya. Sisi ni wataalamu na hatukubali kufanya kazi kwa namna hii," ameongeza.

Joel Marambugi amesema wameshtushwa na mabadiliko hayo ya ghafla, akieleza kuwa Mwaihabi alikuwa na mipango mizuri na tayari amefanya mageuzi makubwa shuleni hapo.

"Tunaomba kwa sasa mabadiliko haya yasitishwe. Tuko kwenye kipindi cha uchaguzi na yamekuja ghafla mno. Taasisi imepata mafanikio makubwa. Hatukatai mabadiliko kwa manufaa ya chama na taasisi, lakini tunajiuliza huyu anayekuja analeta mabadiliko gani, na hata huko alikotoka amefanya nini,” amesema.

Kwa upande wake, Yohana Mwakasambo amesema wamepata mshtuko kwa kupelekewa kiongozi ambaye amekuwa akihamishwa mara kwa mara na ambaye rekodi zake haziridhishi.

"Sisi watumishi msimamo wetu ni kutofanya naye kazi. Hatukubaliani na uamuzi huu na tuko tayari kuacha kazi," amesema Mwakasambo.