Unene sio mzuri kwa watoto

Muktasari:
- Wazazi watambue kuwa unene sio afya, bali unaweza kuwa dalili ya maradhi mabaya kwa watoto wao.
Wazazi wengi huwapa watoto aina ya vyakula vya wanga kwa wingi, na kusahau kuwa ulaji bora ni ule uliokamilika na unaotakiwa kuzingatia mahitaji ya mwili.
Kwa watoto chini ya miezi sita, ni muhimu wapewe maziwa ya mama tu na sio zaidi. Watoto wenye miezi sita mpaka miaka miwili, wazazi wanashauriwa kuwapa maziwa ya mama na chakula mchanganyiko.
Kwa miaka miwili hadi mitano, wapewe angalau milo mitano kwa siku na maziwa yaendelee kuwa sehemu ya mlo wao na aina nyingine ya vyakula vyenye protini. Watoto wa umri wa miaka sita hadi tisa wapewa milo kamili mitatu, ila ni muhimu kwa wazazi kuepuka kuwapa protini aina ya nyama na mafuta kwa wingi, ili kuepusha unene usiotarajiwa. Wazazi wawazoeshe watoto wao kula mbogamboga za majani na matunda katika kila milo yao mikuu. Matunda iwe kama mlo wa kati.
Tabia ya wazazi kuwazoesha watoto kula vyakula vya mafuta mengi au vilivyokaangwa kwa mafuta mengi, sio nzuri kwa afya ya watoto pia ni rahisi kuleta tatizo la unene wa kupitiliza (obesity) katika umri mdogo. Huku ni kuwasababishia Kisukari aina ya pili.
Hata hivyo, kuna unene wa kurithi; hali hii kwa watoto sio nzuri. Kama katika familia kuna historia ya unene, mzazi anatakiwa kuwa makini katika malezi ya mtoto. Katika familia yenye asili ya unene, mzazi ajue makundi yote muhimu ya chakula na kazi zake katika mwili. Pia aanze kumpunguzia mtoto kiasi cha vyakula vya wanga.
Ni wajibu wa mzazi kuanza kumzoesha mtoto au kijana wa umri wa kubalehe kula protini kama vile maharage, kunde na angalau mara moja kwa wiki kula protini aina ya nyama. Mazoezi na michezo mbalimbali ya kuchangamsha mwili inamsaidia mtoto kutopata unene.
Tabia ya mzazi akitoka kazini au safarini na zawadi ya juisi, cholocate kwa watoto, inawaweka katika hatari.
Wazazi wengi wanaamini kuwa kunenepa kwa watoto wao ni jambo zuri na wanapima afya za watoto wao kwa unene wa miili yao.