Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabadiliko  homoni yanavyoathiri  sukari kwa wanawake

Muktasari:

  • Homoni ni vichocheo vya mwili vinavyosaidia kudhibiti kazi nyingi mwilini, ikiwemo jinsi ya kutumia na kuhifadhi sukari mwilini.

Wanawake wenye kisukari hupata changamoto kwenye miili yao kutokana na mabadiliko ya homoni yanayotokea katika hatua mbalimbali za maisha yao.

Homoni ni vichocheo vya mwili vinavyosaidia kudhibiti kazi nyingi mwilini, ikiwemo jinsi ya kutumia na kuhifadhi sukari mwilini.

 Kwa wanawake, mabadiliko ya homoni hutokea wakati wa mzunguko wa hedhi, ujauzito, kunyonyesha, na wakati wa kukoma hedhi. Hali hizi zinaweza kuwa na athari kubwa kwa udhibiti wa viwango vya sukari.

Kipindi cha mzunguko wa hedhi, viwango vya homoni kama vile ‘estrogen’ na ‘progesterone’ hubadilika. Kabla ya hedhi kuanza, homoni ya ‘progesterone’ huongezeka na hufanya mwili kushindwa kutumia insulin, hali inayosababisha sukari kupanda sana.

Wanawake wenye kisukari viwango vyao vya sukari hupanda sana siku chache kabla ya hedhi, na kushuka ghafla baada ya hedhi kuanza. Hivyo ni muhimu kwa mwanamke kufuatilia mzunguko wa hedhi na kupima kila mara viwango vya sukari,  kipindi hicho ili kujua jinsi gani anaweza kudhibiti hali hiyo.

Wakati wa ujauzito huwa kuna mabadiliko ya homoni ambazo huongezeka zaidi ili kusaidia ukuaji wa mtoto tumboni.

Homoni hizi, kama vile ‘human placental lactogen’, husababisha mwili kushindwa kutumia insulin, hivyo  kwa wajawazito wenye kisukari hali hii inahitaji uangalizi wa karibu  ili kuhakikisha mtoto anakua salama na mama hapati matatizo ya kiafya.

Mabadiliko haya pia hufanya wanawake wasio na kisukari kugundulika kwa mara ya kwanza wakati wa ujauzito. Kisukari kipindi cha ujauzito kinachotwa ‘gestational diabetes’ huongezeka kwa sababu ya mabadiliko haya ya homoni.

Baada ya kujifungua na wakati wa kunyonyesha, homoni ya ‘oxytocin’ huongezeka na mara nyingine huchangia kushuka kwa sukari.

Kunyonyesha kunatumia nishati nyingi mwilini, kama mama hatakula vya kutosha, anaweza kupata ‘hypoglycemia’ ambayo ni hali ya kushuka sana kwa sukari mwilini.

 Ni muhimu kwa mama anayenyonyesha kuhakikisha anakula milo midogo mara kwa mara na kupima sukari yake kabla na baada ya kunyonyesha.

Kipindi cha kukoma hedhi nacho huambatana na mabadiliko ya viwango vya homoni, hasa kupungua kwa ‘estrogen’.

Upungufu huu huweza kuongeza hatari ya kupanda kwa viwango vya sukari na pia kupunguza uwezo wa mwili kutumia insulini ipasavyo.

Wanawake walio katika kipindi hiki wanaweza pia kupata usumbufu wa usingizi, mabadiliko ya hisia, na kuongeza uzito mambo ambayo yote yanaweza kuathiri viwango vya sukari.

Kwa ujumla, ni muhimu kwa wanawake wanaoishi na kisukari kuwa na uelewa mzuri wa mabadiliko haya ya homoni na namna yanavyoathiri sukari mwilini.

Ni muhimu kufuatilia mzunguko wa hedhi, kufanya mazoezi, kula mlo kamili, kupima sukari mara kwa mara na kutumia dawa kama daktari anavyoshauri.