Dhibiti hivi kisukari unapougua malaria

Wagonjwa wa kisukari wanakumbana na changamoto mbalimbali katika kudhibiti afya zao, na hali huwa ngumu zaidi pale wanapougua magonjwa mengine kama vile malaria.
Malaria ni ugonjwa unaoambatana na homa kali, kutetemeka, maumivu ya mwili na kichefuchefu, dalili ambazo pia zinaweza kufanana na zile za kupanda kwa sukari.
Kwa hali hiyo, ni muhimu sana kuelewa jinsi ya kutofautisha dalili hizo na namna ya kudhibiti kiwango cha sukari wakati wa malaria.
Dalili za kawaida za malaria ni pamoja na homa ya ghafla, kutetemeka kwa mwili, maumivu ya kichwa, kichefuchefu, kutapika, maumivu ya viungo, na uchovu mkubwa.
Kwa upande mwingine, dalili za kupanda kwa sukari hujumuisha kiu ya kupitiliza, kukojoa mara kwa mara, kichefuchefu, kizunguzungu, macho kuona ukungu na uchovu.
Ingawa baadhi ya dalili zinakaribiana, kuna nyingine kama kukojoa mara kwa mara na kiu kali ya maji, hivyo ni viashiria vya sukari kuwa juu na siyo malaria.
Mgonjwa mwenye kisukari anapopata malaria, mwili huingia kwenye hali ya msongo, na homoni za msongo husababisha kupanda kwa kiwango cha sukari mwilini.
Pia, iwapo mgonjwa atapoteza hamu ya kula au atatapika, kuna uwezekano wa kushuka kwa sukari.
Iwapo atatumia insulini au dawa nyingine ya kudhibiti viwango vya sukari bila kula chakula cha kutosha, itasababisha sukari kuzidi kushuka, hivyo usimamizi wa hali hii unahitaji uangalizi wa karibu.
Jambo la msingi ni kuhakikisha mgonjwa anapima viwango vya sukari mara kwa mara angalau mara nne kwa siku.
Hii itasaidia kugundua iwapo sukari inapanda sana au inashuka, na hivyo kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
Ikiwa mgonjwa hatumii kifaa cha kupimia sukari nyumbani, ni vyema kufika kituo cha afya kilicho karibu kwa ajili ya usimamizi wa karibu.
Wakati wa matibabu ya malaria, baadhi ya dawa za malaria zinaweza pia kuathiri kiwango cha sukari, hivyo ni muhimu kumjulisha daktari kwamba mgonjwa ana kisukari ili aweze kutoa mwelekeo sahihi wa matibabu.
Kwa wagonjwa wanaotumia insulini, kuna uwezekano wa kuhitaji kurekebisha dozi kulingana na kiwango cha sukari kinavyoonekana.
Lishe ni jambo muhimu la kuzingatia, hata kama malaria imesababisha mgonjwa kupoteza hamu ya kula basi apewe vinywaji vya nishati kama uji wa lishe, juisi halisi au supu yenye virutubisho.
Ulaji wa vyakula vya wanga na unywaji wa maji kwa wingi, husaidia kuimarisha kiwango cha sukari, kwani mwili unapoteza maji mengi wakati wa homa na kutapika.
Wagonjwa wa kisukari wanapohisi kuwa wana malaria wasianze kutumia dawa kabla ya kwenda kwa daktari na kufanya vipimo. Na wakipewa dawa za malaria ni muhimu kumaliza dozi pasipo kuruka au kuacha.