Hatari ya kifafa kwa wagonjwa wa kisukari

Muktasari:
- Familia zinapaswa kuvunja mitazamo hii kwa kujielimisha kuwa kifafa cha kisukari ni suala la kitabibu linaloweza kudhibitiwa kwa msaada wa haraka na maandalizi sahihi.
Kisukari ni ugonjwa sugu unaohitaji ufuatiliaji wa karibu kila siku. Mojawapo ya hatari kwa watu wenye kisukari ni kushuka kwa sukari kupita kiasi hali inayojulikana kwa jina la ‘hypoglycemia’.
Ikiwa haitatibiwa mapema, ‘hypoglycemia’ inaweza kusababisha kifafa, kupoteza fahamu, au hata kifo. Hali hii ni hatari zaidi kwa watoto, hasa wale wanaotumia insulini mara kwa mara.
Kushuka kwa sukari husababisha ubongo kushindwa kufanya kazi zake kwa kawaida. Dalili za awali ni pamoja na kutetemeka, jasho jingi, mapigo ya moyo kwenda kasi, kizunguzungu na njaa kali.
Ikiwa hatua ya haraka haichukuliwi, mtu anaweza kuanza kuchanganyikiwa, kupoteza fahamu au kupata kifafa.
Hali hii inaweza kutokea muda wowote, lakini kuna nyakati hatarishi zaidi. Mosi, baada ya kutumia insulini bila kula chakula cha kutosha. Pili, wakati wa kufanya mazoezi makali bila kula chakula au kupunguza dozi ya insulini. Vilevile, sukari inaweza kushuka sana ikiwa mgonjwa anakula chakula chenye wanga kidogo kupita kiasi au anakunywa pombe bila kula. Hatari pia huongezeka wakati wa usiku katikati ya usingizi mzito ambapo ni vigumu kugundua dalili.
Pindi dalili za kushuka kwa sukari zinapojitokeza, hatua ya haraka ni kumpa mgonjwa kitu chenye sukari, kama asali au glukosi.
Lengo ni kuhakikish kuwa kiwango cha sukari mwilini kinakuwa sawa. Ikiwa mgonjwa amepoteza fahamu au amepata kifafa, usimpe kitu cha kumeza kwani anaweza kupaliwa. Badala yake, apewe sindano ya glukagon kama ipo, au akimbizwe hospitalini kwa matibabu ya haraka.
Ili kuzuia hali hii, kuna hatua rahisi za kufuata. Kwanza, kula kwa wakati ni muhimu sana. Watoto wenye kisukari wanapaswa kuwa na ratiba ya kula na kuzingatia dozi ya insulini. Pili, kupima sukari mara kwa mara kunasaidia kugundua hali ya hatari kabla haijatokea. Tatu, ni muhimu kujifunza na kuzijua dalili zake za mwanzo za kushuka kwa sukari.
Kwa watoto shuleni, walimu wanapaswa kufahamu hali zao na kuwa na juisi au pipi kwa dharura. Familia nazo zinatakiwa kujifunza na kuwa elimu ya kutosha ili kusaidia watoto wao anapopata dalili. Kuweka chakula au pipi kila mara kwenye begi la shule ni hatua rahisi inayoweza kuokoa maisha.
Familia zenye watoto wanaoishi na ugonjwa wa kisukari, baadhi yao zina imani potofu kwamba kifafa ni matokeo ya laana, kurogwa au mapepo. Hali hii imekuwa kikwazo kikubwa katika kuwahi kutoa msaada.
Familia zinapaswa kuvunja mitazamo hii kwa kujielimisha kuwa kifafa cha kisukari ni suala la kitabibu linaloweza kudhibitiwa kwa msaada wa haraka na maandalizi sahihi.
Kupitia elimu, ufuatiliaji wa karibu, na msaada wa haraka, tunaweza kuokoa maisha ya watoto wenye kisukari.