Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nida yakunjua makucha vitambulisho feki, wamiliki wa steshenari watajwa

Muktasari:

  • Nida imesema Aprili 23, 2025 kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walimkamata mkazi wa Chalinze mkoani Pwani anayetuhumiwa kutengeneza na kuchapisha vitambulisho bandia vya Taifa.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imewaonya wamiliki na watoa huduma wa ‘steshenari’ wanaotengeneza na kuchapisha Vitambulisho vya Taifa ikieleza kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Nida, Geofrey Tengeneza kumekuwa na ongezeko la watu wenye namba za utambulisho (NIN) kutengenezewa vitambulisho bandia, ambavyo imebainika katika uchunguzi hutengenezwa kwenye steshenari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2025 jijini Dar es Salaam, Tengeneza amesema Aprili 23, 2025 Nida kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walimkamata mkazi wa Chalinze, Danford Mathias aliyetuhumiwa kutengeneza na kuchapisha vitambulisho bandia vya Taifa.

Baadhi ya vitambulisho vua Nida vikiwa kwenye box, tayari kuchukuliwa na wananchi. Picha na Mtandao

Kukamatwa wa mtuhumiwa huyo amesema ni sehemu ya operesheni inayoendelea kwa sasa nchi nzima chini ya Nida dhidi ya watu wanaohadaa umma kuwa wanatengeneza vitambulisho hivyo ambavyo ni nyaraka za Serikali.

Nida wakieleza hayo, mwaka jana (2024) Mwananchi katika ufuatiliaji wake jijini Dar es Salaam ilibaini uwepo wa watu wanaotengeneza nakala za vitambulisho hivyo kwenye steshenari.

Wanaofanya hivyo huwatoza wateja wao bei tofauti kwa kazi hiyo kulingana na nakala za vitambulisho mteja anazohitaji zikiwamo tete (soft copy) na ngumu (hard copy).

"Karibu nikutengenezee kitambulisho cha Taifa, Sh15,000 soft copy na Sh25,000 hard copy, karibu inbox tuzungumze," ni moja ya tangazo la mtengenezaji wa vitambulisho hivyo alilokuwa amelichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa Whatsapp kupitia 'Status'.

Katika ufuatiliaji Mwananchi ilibaini wanaotengeneza vitambulisho hivyo hutumia taarifa za mtandaoni zilizowekwa na Nida.

Katika eneo la Tabata mmoja wa wanaofanya kazi hiyo ilibainika taarifa za mteja huzitafuta kupitia namba ya muhusika katika tovuti ya Nida, baada ya hapo hutumia nakala tete kuchapisha kitambulisho, kazi anayoifanya ndani ya dakika 30 kabla ya kumkabidhi mteja kitambulisho.

Ilibainika wateja wengi ni madereva wa bodaboda na watu wanaokwenda kukopa kwenye vikundi.

Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Geofrey Tengeneza akizungumza na waandishi wa habari jjjini Dar es Salaam leo Ijumaa Mei 2, 2025. Picha na Sunday George

Katika eneo la Buguruni ilibainika kwa siku mtengenezaji aliweza kuhudumia watu kati ya watatu na watano.

"Nimeshachoka kuhangaikia kitambulisho, kwanza sijui nikakichukue wapi maana nilijiandikisha kwenye maonyesho yalifanyika viwanja vya Mbagala Rangi Tatu mwaka 2019 hadi leo (mwaka 2024)," alisema mkazi wa Mbagala akieleza sababu za kutafuta kitambulisho kwenye steshenari.

Tengeneza katika mkutano na waandishi wa habari amesema mtuhumiwa Mathias alikuwa akitoa huduma hiyo kwenye steshenari kwa gharama ya kati ya Sh6,000 na Sh10,000.

Amesema mtuhumiwa alikamatwa akiwa na vifaa vyake vya kazi baada ya kuwekewa mtego wa mtu aliyehitaji huduma hiyo ambaye alimtengenezea kitambulisho kwa Sh10,000.

“Katika kutengeneza na kuchapisha vitambulisho hivyo feki, mtuhumiwa huyu hutumia kitambulisho chake halali cha Nida na kuki-scan kisha kukiingiza kwenye mfumo wa Adobe na kufuta taarifa zake, kisha kubandika taarifa za mteja. Baada ya hapo hukichapisha kitambulisho hicho bandia na kumkabidhi mteja.

“Wamiliki wa maduka ya steshenari wanapaswa kutambua kuwa utengenezaji au uchapishaji wa vitambulisho feki vya Taifa ni kosa la jinai na ni kinyume cha Sheria ya Usajili na Utambuzi Sura ya 36 ya Mwaka 2012, Kanuni ya Usajili na Utambuzi wa Watu ya Mwaka 2014 na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura Na. 16 Rejeo la mwaka 2022,” amesema.

Tengeneza amewatahadharisha wananchi wanaokwenda kutengeneza vitambulisho hivyo steshenari, akisisitiza kitambulisho halisi ni kile kinachotengenezwa na kuchapishwa na

Nida, ambacho mara ya kwanza hutolewa bure bila malipo.

“Kwa wale wanaokwenda steshenari kwa lengo la kutengenezewa Vitambulisho vya Taifa kwanza, wafahamu kuwa vitambulisho hivyo ni feki hivyo, kumiliki kitambulisho cha namna hiyo ni kosa na utakapokamatwa nacho utafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Wale wenye namba za utambulisho wawe wavumilivu, wanapopewa muda wa siku chache kusubiri vitambulisho vyao kuzalishwa kwani, kwa sasa huchukua majuma mawili mpaka matatu tu kuzalishwa baada ya kukamilisha usajili,” amesema.

Nida ikieleza hayo, Mwananchi imezungumza na baadhi ya wananchi ambao wameeleza kinachosababisha watu kukimbilia kutengeneza vitambulisho kwenye steshenari ni usumbufu wanaopata kutoka mamlaka hiyo.

Muonekano wa kitambulisho cha Nida. Picha na Mtandao

Theodora Mrema, mkazi wa Tabata amesema urasimu ndiyo unafanya watu watafute njia za mkato za kupata vitambulisho hivyo kuliko kusubiri vinavyotolewa bure.

“Kwanza kwenye hivyo vituo ni foleni kila siku, haya ukifanikiwa kuandikisha kuja kukipata kitambulisho bado utaenda tena kupoteza siku nzima, mtu anaona kama ana namba ni heri akalipe fedha atengeneze huko steshenari kuliko usumbufu huo,” amesema.

Kwa upande wake, Jumanne Mayanja mkazi wa Kinondoni amesema Nida inapaswa kurahisisha mchakato wa utoaji vitambulisho ikiwemo kupunguza muda wa ufuatiliaji.

“Haya mambo yote yanatokea kwa sababu kitambulisho hiki ni muhimu lakini upatikanaji wake umekuwa mgumu kidogo, ukitaka kupata kitambulisho cha Nida uache kazi ufanye kazi, sasa kama una shida ya haraka ndiyo hivyo unaona bora usogee steshenari,” amesema.

Akizungumzia maoni hayo, Tengeneza amesema kama mwananchi anahitaji kupata kitambulisho kwa haraka kabla ya muda uliowekwa anapaswa kufika kwenye ofisi za Nida kueleza uhitaji wake ili kupata huduma sahihi badala ya kutumia njia za mkato ambazo huishia kutapeliwa.


Wasiochukua vitambulisho

Katika hatua nyingine, Nida imesitisha matumizi ya namba za utambulisho kwa watu ambao vitambulisho vyao vimetengenezwa lakini hawajavichukua hadi sasa.

Tengeneza amesema matumizi ya namba hizo yamesitishwa Mei Mosi, 2025 kama ilivyotangazwa hivyo kuanzia Mei 2 namba hizo hazitaweza kutumika kwa shughuli zozote za utambuzi hadi wahusika watakapofuata vitambulisho vyao.

“Baada ya kufunga tumepokea simu nyingi watu wakiuliza sasa itakuwaje, ndiyo basi tena Nida zetu zimefungiwa tutakosa huduma. Nitumie fursa hii kuwafahamisha wananchi kuwa namba inapofungwa haina maana kwamba ndiyo basi utambulisho wako umefutwa, hapana ni kwamba utakapokuja kuchukua kitambulisho chako namba yako inahuishwa (activated) na kuanza kutumika tena,” amesema.

Januari 21, 2025, Mkurugenzi wa Nida, James Kaji alisema wamefanya utafiti na kubaini wananchi hawafuati vitambulisho hivyo kwa sababu wana namba za utambulisho.

“Tunatuma ujumbe mfupi wa simu (SMS) ambao tumekuwa tukiwatumia wahusika wa vitambulisho ambavyo havijachukuliwa. Ujumbe huo unasomeka: ‘Asipofika kuchukua kitambulisho chake ndani ya muda ulioelekezwa, matumizi ya namba yake ya utambulisho wa Taifa (NIN) yatasitishwa.’

"Tumefanya utafiti ni kwa nini wahusika hawajitokezi kuchukua vitambulisho vyao, tulibaini baadhi ya wananchi wanafanya makusudi kwa kuwa wana namba za utambulisho, yaani MINs, ambazo zinawasaidia kupata huduma sawa na mwenye kitambulisho," alisema na kuongeza:

"Sambamba na hilo, tumebaini baadhi ya wananchi wamehama kutoka sehemu walikokuwa wanaishi wakati wanajisajili na vitambulisho vyao vimepelekwa sehemu nyingine. Pia, baadhi ya wananchi wamefariki dunia."

Kaji alisema kwa sasa vitambulisho vyote vitachukuliwa kwenye ofisi za wilaya, tofauti na ilivyokuwa awali vilikuwa vikitolewa ngazi ya kata, vijiji, serikali za mitaa na vitongoji, ambako muitikio ulikuwa mdogo, uliosababisha zaidi ya vitambulisho milioni moja kubaki katika ofisi hizo kwa muda mrefu.

Uamuzi wa kuvipeleka vitambulisho wilayani umechukuliwa baada ya wananchi kulalamika juu ya changamoto wanazokutana nazo kutoka ofisi hizo na wengine kushindwa kuvipata.