Nida kutoa namba kwa watoto na wageni, kuzifuta hizi…

Muktasari:
- Kuanzia Mei mosi, 2025, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetangaza kufungia namba zote ambazo vitambulisho vimetelekezwa ndani ya mamlaka hiyo.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imetangaza mpango wa utambuzi na usajili wa watu wote chini ya miaka 18 na raia wa kigeni wanaoingia nchini na kukaa zaidi ya miezi sita kuanza kupatiwa jamii namba.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, usajili wa watu wenye umri chini ya miaka 18 utaanza kwa majaribio katika wilaya tatu ambazo ni Kusini-Kusini Unguja, Kilolo-Iringa, na Rungwe-Mbeya na watu 335,826 watafikiwa kwa kipindi cha miezi miwili.
Pia, mamlaka hiyo imetangaza kuwa hadi Mei mosi 2025 watazifungia namba za Nida kwa watu wote ambao hawakwenda kuchukua vitambulisho vyao kwenye mamlaka hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 14, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji amesema hatua ya utambuzi wa watoto ni hitaji la Rais Samia Suluhu Hassan aliyeitaka mamlaka hiyo kuongeza wigo wa usajili na utambuzi kuanzia mtoto anapozaliwa.
"Azma ya Rais Samia ni kuondoa usumbufu kwa wananchi wakati wa kutafutiwa huduma, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa taasisi za umma na binafsi na kuwepo na utambulisho mmoja kwa mtu mahali popote," amesema.
Kauli ya Rais Samia ni ile aliyoitoa Agosti 11, 2023 wakati akizindua mkongo wa baharini wa mawasiliano ya internet wa Airtel 2Africa Dar es Salaam ambapo alielekeza watu wote wanaoishi nchini watambulike kupitia namba ya kipekee ya Taifa ya utambulisho.
Kuhusu raia wa kigeni, Kaji amesema watakaotambuliwa na kupewa jamii namba pekee ni wale waliokaa nchini kwa zaidi ya miezi sita na wenye vibali vya makazi.
Akizungumzia ufungaji wa namba za Nida, Kaji amesema kwa watu waliotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kufuata vitambulisho na kupuuza wito huo, namba zitafungiwa hadi watii angizo.
"Kwa kuzingatia tulishawatumia ujumbe kwa watu wote ambao vitambulisho vyao vilikusanywa, tutafunga matumizi ya NIN kwa wale ambao tumeshazalisha vitambulisho vyao," amesema.
Kaji amesema tangu Machi 23, 2025 wananchi milioni 1.88, sawa na asilimia 157 ya watu wote waliokuwa hawajachukua vitambulisho vyao wametumiwa ujumbe mfupi (SMS).
Mbali na hayo, Kaji amesema Nida imeunganisha mfumo wake na taasisi 128, kati ya hizo 71 taasisi binafsi, 57 taasisi za umma, lengo kuboresha huduma kwa wananchi na kuwezesha kila mtu atambulike kwa taarifa zake za utambulisho.
"Tumepokea maombi ya taasisi 56 yamepokelewa kuanzia Januari hadi Aprili 12, tunataraji hadi Desemba 2025 kutakuwa na taasisi 200 zilizounganisha mifumo yake na mifumo ya NIDA," amesema.
Aprili 3, 2023, Rais Samia aliagiza ifikapo Desemba 2024 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ahakikishe mifumo yote ndani ya Serikali inasomana.
Hiyo ilikuwa si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutoa maelekezo hayo, kwani aliwahi kufanya hivyo Juni 9, 2023 katika Baraza la Biashara Dar es Salaam, akitaka kuharakishwa kwa maboresho yatakayofanya mifumo ya taasisi za umma isomane.
Agizo kama hilo alilitoa tena Agosti 11, 2023 kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuhakikisha mifumo yote ya Tehama inayotumika ndani ya Serikali inasomana.
Katika maelekezo hayo, alitaka hilo likamilike ifikapo Desemba, 2024 na aliwataka makatibu wakuu wa wizara kuhakikisha wanasimamia utekelezwaji wake.
Wanachosema wananchi
Sophia James, mkazi wa Kinondoi-Manyanya, Dar es Salaam amesema mpango wa kuanza kuwatambua watoto kupitia Nida utaondoa mkanganyo wa taarifa za kuzaliwa na majina ya watoto.
"Mfumo huu utaondoa mkanganyiko wa taarifa za mtoto, utakuta mtoto kwenye cheti cha kuzaliwa ana jina lingine kwenye Nida akiwa mkubwa anaandika jina lingine, sasa huu utaratibu utaleta suluhu maana mtoto taarifa zake zitatunzwa kwenye mfumo," amesema.
Naye Gibson Peter, mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam amesema Nida inapaswa kuwapa wananchi elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na kitambulisho hicho, kwani wananchi hutafuta vitambulisho wanapotafuta ajira au kusafiri nje ya nchi.