Nida yakomaa na wasiochukua vitambulisho

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Wilbert akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Yasisitiza kusitisha matumizi ya namba za wale walipokea ujumbe mfupi kwa njia ya simu unaowataka kwenda kuchukua vitambulisho vyao ndani ya muda uliolekezwa.
Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia siku 10 kabla ya utekelezaji wa kufungia namba za utambulisho wa uraia kwa wananchi ambao hawajachukua vitambulisho, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imesema haitaongeza muda na itasitisha matumizi ya namba hizo kwa watu wote walipokea ujumbe kwa njia ya simu unaowataka kwenda kuchukua vitambulisho vyao.
Uamuzi huo umekuja baada ya kusuasua kwa wananchi kwenda kuchukua vitambulisho vyao, licha ya kutumiwa ujumbe mfupi uliowataka kwenda kuvifuata kwenye ofisi za Nida za wilaya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Januari 21, 2025, Mkurugenzi wa NIDA, James Kaji, amesema wamefanya utafiti na kubaini wananchi hawafuati vitambulisho hivyo kwa sababu wana namba za utambulisho.
“Tunatuma ujumbe mfupi wa simu (SMS) ambao tumekuwa tukiwatumia wahusika wa vitambulisho ambavyo havijachukuliwa. Ujumbe huo unasomeka: ‘Asipofika kuchukua kitambulisho chake ndani ya muda ulioelekezwa, matumizi ya namba yake ya utambulisho wa taifa (NIN) yatasitishwa.’
"Tumefanya utafiti ni kwa nini wahusika hawajitokezi kuchukua vitambulisho vyao, tulibaini baadhi ya wananchi wanafanya makusudi kwa kuwa wana namba za utambulisho, yaani MINs, ambazo zinawasaidia kupata huduma sawa na mwenye kitambulisho."
"Sambamba na hilo, tumebaini baadhi ya wananchi wamehama kutoka sehemu walikokuwa wanaishi wakati wanajisajili, na vitambulisho vyao vimepelekwa sehemu nyingine. Pia, baadhi ya wananchi wamefariki," amesema.
Aidha, Kaji amesema kwa sasa vitambulisho vyote vitachukuliwa kwenye ofisi za wilaya, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo vilikuwa vikitolewa ngazi ya kata, vijiji, Serikali za mitaa na vitongoji, ambapo muitikio ulikuwa mdogo, uliosababisha zaidi ya vitambulisho milioni moja kubaki katika ofisi hizo kwa muda mrefu.
Uamuzi wa kuvipeleka vitambulisho wilayani umekuja baada ya wananchi kulalamika juu ya changamoto wanazokutana nazo kutoka ofisi hizo na wengine kushindwa kuvipata.
Wakati Nida ikieleza hivyo, baadhi ya wananchi wanalalamika kutopata vitambulisho vyao takribani miaka saba sasa tangu kujisajili.
“Nimefanya kazi ya kuambiwa njoo baada ya miezi miwili, iliisha, naenda tena naambiwa hivyo hivyo, hali ya wenzetu wa hivi karibuni wanavyo, huku baadhi ya fursa zinanipita,” amesema Juma Sultani.
Kwa upande wake, Kareem George amesema amefanya mchakato wote wa kubadili jina kwenye Nida yake hadi kwenda mahakamani na kupewa deedpol na kulipa hela, lakini hadi sasa hajapata kitambulisho chake.
“Nimekwenda mahakamani, nikapata deedpol na kulipa Sh15,000, nikaambiwa niende kwa mkuu wa mkoa, nikalipa Sh33,000, nikaambiwa niende kwa mkuu wa wilaya, nikalipa Sh10,000, nikambiwa nitume gazetini nikalipa Sh20,000, nikalipa na Nida Sh20,000. Nikamaliza, wakaniambia nikipata kitambulisho niende kubadili jina,” amesema George.