Hofu yatanda; hospitali, zahanati zilivyoshindwa kudhibiti taka hatari

Uchafu wa hospitali uliotupwa kwenye eneo la wazi. Uchafu huu usippdhibitiwa huweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza. Picha na Maktaba.
Muktasari:
- Utupaji wa taka ovyo ni hatari lakini taka hatari zaidi ni zile za hospitali ambazo zinaweza kuambukiza magonjwa hata yale yasiyotibika kama Ukimwi na Homa ya ini endapo hazitadhibitiwa.
Unapita karibu na hospitali kubwa hapa nchini, unakutana na jaa lililojaa sindano zilizotumika, bandeji, plasta, pamba zenye damu na glasi za kupimia malaria.
Huu unaitwa uchafu wa hospitali na unafafanuliwa na Wakala wa Utunzaji wa Mazingira kama chochote kile ambacho kinagusana na majimaji ya mwilini, kama vile mipira ya mikono, sindano, visu vya kufanyia upasuaji, cannula (sindano ama kibomba cha kuingiza katika mshipa wa damu kwa ajili ya kuingizia dawa na maji ya dripu) na bandeji zenye damu.
Uchafu wa hospitali waweza kupatikana kutoka hospitali, zahanati, kliniki na maabara au maeneo ya kufanyia tafiti za kimaabara.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Taasisi ya Afya ya Ifakara, (IHI) inaeleza kuwa, hospitali nyingi hazikuwa na maeneo maalum ya kutupa au kuharibu taka hatarishi ambazo zinaweza kusababisha maradhi ya kuambukiza.
Ilibainika kuwa asilimia 11 tu ya hospitali nchini zilikuwa na maeneo salama ya kutupa taka zinazoweza kuambukiza.
Zahanati na hospitali nyingi hazikuwa na jaa la kutupa vifaa vyenye ncha kali vilivyotumika, wala vyombo maalum vya kuchemshia vifaa.
“Zaidi ya robo tatu ya hospitali na zahanati hazikuwa na maski, magauni maalum yanayovaliwa wakati wa upasuaji, wala vifaa vya kuyakinga macho wakati wa shughuli muhimu zinazoweza kusababisha madhara” ilisema sehemu ya ripoti hiyo
Dk Larama Rongo, mtaalamu wa Mazingira na afya katika Chuo Kikuu cha Muhimbili anasema zipo kesi ambazo zinaonyesha wazi watu waliopata maradhi ya homa ya ini kwa kutumia sindano zilizotumika hospitali.
Hatari hiyo si kwa matumizi ya sindano tu bali imebainika kuwa uchafu mwingi hutupwa maeneo ya wazi ambapo watoto huweza kufika na kuchezea vifaa tiba vilivyotumika.
“Watoto wakikuta mabomba ya sindano au zile glasi za kupimia malaria hawawezi kuacha kuchezea, utakaposhtuka mtoto kashapata maradhi ya ajabu” anasema Selina Makonde, mkazi wa Kimara, Dar es Salaam.
Imebainika kuwa baadhi ya uchafu hutupwa baharini ambako kunatajwa kuwa na hatari zaidi kwa watu wanaoogelea. Kwa mfano, vitu vyenye ncha kali kama sindano za dawa au za kutolea damu ya malaria, huweza kusababisha maambukizi endapo vitatupwa kwenye maji.
Uchafu mwingine wa hospitali hasa vifaa vyenye ncha kali vinapotupwa baharini vinaweza kuwachoma watu wenye VVU au hata homa ya ini(hepatitis B) na kuwaambukiza wengine kwa urahisi. Kwa mfano uogeleaji wa watoto Tanzania hasa maeno ya fukwe za wazi.
Si hivyo tu, uchafu wa hospitali unasababisha kuzagaa kwa sumu na hatimaye kuathiriwa kwa viumbe vya baharini kama samaki na mimea ya baharini. Wataalamu wa afya wanasema kuwa uchafu wa hospitali wenye sumu huweza kuathiri mzunguko wa chakula baharini na kuathiri viumbe wote.
IHI katika ripoti yao walibaini kuwa ni asilimia 50 tu ya zahanati na 56 ya hospitali ndizo zilizokuwa na sabuni na maji jambo ambalo linaonyesha kuna uzingatiaji hafifu wa kuzuia maambukizi ya magonjwa.
Ina maana kuwa, kwa mfano daktari ametoka kumchunguza mgonjwa lakini hanawi mikono yake au ananawa bila kutumia sabuni na dawa maalum ya kuua vimelea na kisha anakwenda kumchunguza mgonjwa mwingine.
Dk Innocent Mosha wa kitengo cha uchunguzi wa magonjwa(Patholojia) Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alisema kuwa uchafu wa hospitali ni wa hatari mno na unaweza kusababisha maambukizi ya maradhi hatari.
“Kwa kawaida kuna mashine maalum ya kuteketeza uchafu wa hospitali, kuna mashine iitwayo ‘incinirator’ ambayo huuchoma uchafu na kuuteketeza kabisa” alisema
Alisema uchafu wa hospitali hautakiwi kutupwa kama utupwavyo uchafu wa nyumbani kwani ni wa hatari.
“Haiwezekani ukatupa uchafu wa hospitali kama unavyotupa kabichi nyumbani. Huu uchafu niwa hatari” alisema
Utafiti mwingine kama huu ulifanyika nchini mwaka 2003 hadi 2005 kuangali mfumo wa namna ya utunzaji wa uchafu wa hospitali.
Katika utafiti huo ilibainika kuwa udhibiti wa uchafu upo kwa kiwango cha chini katika hospitali nyingi nchini.
Pia wahudumu wengi wa afya hawakuwa na uelewa wa namna ya utunzaji wa taka za hospitali.
Tafiti nyinigine
Katika tafiti nyingine zilizowahi kufanywa nchini kuhusu udhibiti wa uchafu ilibainika kuwa ni asilimia nne tu ya vituo vya afya zilikuwa na miongozo au zilifuata miongozo ya udhibiti wa taka kutoka Wizara ya Afya.
Jambo jingine linaloonyesha udhaifu mkubwa kwa wahudumu wa afya, ambalo lilionekana kwenye ripoti hiyo ya afya ni jinsi wahudumu walivyofanya kazi bila vifaa muhimu vya kujilinda wasipate maanmbukizi.
Kwa mfano wahudumu wengi walikuwa wamevaa nguo za kawaida na si sare za kazi, (asilimia 79) hawakuwa na eproni, maski, mabuti na wakati mwingine hawakuvaa mipira ya mikono.
Vilevile vichoma taka vingi vilivyokaguliwa kwenye hospital vilibainika kuwa havina ubora wa kuziharibu taka hatarishi kama sindano na glasi za kuchota damu.
Dk Herman Syabuka wa Zahanati ya Tabata anasema, hata udhibiti wa mipira ya kiume iliyotumika kwenye maeneo ya nyumba za wageni bado ni hafifu kwa watanzania.
“Niliwahi kuwakuta watoto wakipuliza mipira ya kiume iliyotumika karibu na nyumba moja ya wageni. Niliwagombeza lakini nani anajua, kuna maradhi mengine ya ngozi au ya zinaa huenda yakawapata midomoni” anasema.