Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawakili wa Lissu waja na jipya usikilizaji wa kesi

Muktasari:

  • Tundu Lissu anayeshtakiwa akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii anatarajiwa kufikishwa mahakamani Mei 19, 2025.

Dar es Salaam. Mawakili wa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu wanapanga kuiandikia barua Mahakama kuomba shauri likasikilizwe Chuo cha Sheria kilichopo wilayani Ubungo, Dar es Salaam.

Kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa kwa njia ya mtandao, sasa itasikilizwa katika Mahakama ya wazi ikipangwa kutajwa Mei 19, 2025.

Wakili Jebra Kambole mmoja wa wanajopo wanaomtetea Lissu, leo Jumatano Mei 14, 2025 katika mkutano na waandishi wa habari amesema wanalazimika kuomba kesi isikilizwe kwenye chuo hicho kwa kuwa ni eneo linalochukua watu wengi, kwani wanaotarajiwa kuhudhuria usikilizwaji wa shauri hilo ni wengi.

"Kwa miundombinu ya pale Kisutu tunaona eneo ni dogo, hivyo kila anayetaka kushiriki usikilizwaji huenda asiweze kushiriki vilivyo, ndiyo maana tunakusudia kuiandikia barua Mahakama kuiomba ihamishie kesi hiyo kusikilizwa Chuo cha Sheria ambacho kina miundombinu inayoruhusu," amesema.

Mbali ya hilo, ametoa wito kwa wanafunzi wanaosoma sheria na masuala ya haki za binadamu kuhudhuria ili kujifunza namna mawakili wanavyopingana kwa hoja, jambo litakalowasaidia kuifanya kazi hiyo watakapokuwa mawakili.

Ameshauri Mahakama kufunga spika nje ili watakaoshindwa kuingia kwenye ukumbi wa mahakama wafuatilie kwa kusikiliza wakiwa nje.

Wakili Jebra Kambole akizungumza na waandishi wa habari.

Pia kwa wanaosikiliza kupitia mtandao wahakikishe unapatikana wakati wote.

"Mahakama ya wazi maana yake kila mtu anaweza kwenda au kusikiliza, hivyo pasipotosha si lazima watu wote waingie chemba, wanaweza hata kukaa nje ya viunga vya mahakama. Tunasisitiza hili kwa kuwa tunataka kuona watu wakisikiliza na kuona haki inatendeka," amesema.


Taratibu za kufuata

Mbali ya hilo, amewataka watakaojitokeza kusikiliza kesi kufuata taratibu na sheria ili wasije kujikuta wanaingia matatizoni.

Ametaja taratibu hizo kuwa ni kufika kwa wakati mahakamani kuanzia saa mbili asubuhi kabla ya kesi kuanza, watapaswa kuvaa kwa heshima, staha na wanawake kuepuka kuvaa nguo za kubana.

"Wanapaswa kukaa kwa utaratibu kwani inawezekana wengine wakashindwa kuingia ndani," amesema.

Pia wametakiwa kuzingatia maelekezo ya viongozi muda wote, simu za mkononi wahakikishe zinakuwa katika hali ya mtetemo au kuzizima kabisa na kutobeba silaha ya aina yoyote wala kuanzisha vurugu.

Kwa wanaofuatilia kwa njia ya mtandao, wanapaswa kuzuia sauti na kutopiga muziki au kelele.

Lissu ambaye yupo rumande Gereza la Ukonga, anakabiliwa mashitaka matatu ya kutoa taarifa za uongo, kinyume cha sheria.

Mahakama ilishatoa amri kuwataka ndugu, jamaa, marafiki na wafuasi wa Chadema wanaokwenda kusikiliza kesi hiyo wasikilize kwa amani.

Uamuzi huo ulitolewa Mei 6, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Kwa mara ya kwanza Lissu alifikishwa Kisutu, Aprili 10, 2025, na kusomewa mashitaka hayo.

Dickson Matata, wakili mwingine wa Lissu amesema mteja wao anaendelea vizuri.

Katika salamu zake kwa wana- Chadema, Matata amesema kiongozi huyo amewataka kushikamana licha ya changamoto wanazokumbana nazo.