Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yatoa amri tano kesi ya Lissu

Mawakili wa utetezi kesi ya Uhaini na kuchapisha taarifa ya uongo,zinazomkabili mwenyekiti Chadema, Tundu Lissu wakifurahi baada ya Mahakama kukubali ombi la mshitakiwa kuletwa mahakamani. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Lissu anakabiliwa na mashitaka matatu katika kesi ya jinai ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii, kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  imetoa amri tano ikiwamo kuridhia, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu apelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi yake ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa Youtube.

Lissu ambaye yupo rumande Gereza la Ukonga, anakabiliwa mashitaka matatu ya kutoa taarifa za uongo, kinyume cha sheria.

Amri nyingine zilizotolewa na Mahakama hiyo ni kesi yake kusikilizwa mahakama ya wazi ili kila mmoja aweze kupata fursa ya kuhudhuria na kusikiliza kesi hiyo.

Pia, mshtakiwa huyo apelekwe mahakamani hapo Mei 19, 2025 kwa ajili kusikiliza hoja za awali ambazo zitasomwa na upande wa mashitaka.

Vilevile, amri nyingine iliyotolewa na mahakama hiyo ni kuwataka ndugu, jamaa, marafiki na wafuasi wa chama hicho wanaokwenda kusikiliza kesi hiyo wasikilize kwa amani na watunze ndani na nje ya Mahakama.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Mei 6, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa kutolewa uamuzi iwapo mwenendo wa kesi hiyo usikilizwe kwa njia ya mtandao au mshtakiwa apelekwe mahakamani hapo.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mhini amesema kilichofanywa na Mahakama cha kuamuru kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao ilikuwa ni sahihi na kanuni zilizotengenezwa na Jaji Mkuu zilikuwa hazijakiuka chochote.

Askari Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam leo Jumane, Mei 6, 2025.

"Baada ya kupitia hoja za pande zote, Mahakama imeamuru kesi itasikilizwa kwa njia ya kawaida na mshtakiwa anatakiwa aletwe mahakamani kusikiliza kesi yake" amesema Hakimu Mhini.

Amesema mshtakiwa huyo anapaswa kuwepo mahakamani hapo ili aweze kusikiliza kesi yake na  kusaini nyaraka kuhusiana na hoja zinazokubalika na zile zinazobishaniwa.

Pia hakimu Mhini, ameelekeza mkuu wa gereza husika kuhakikisha anampeleka mshtakiwa huyo mahakamani hapo siku ya tarehe tajwa.

Vilevile, watu na wafuasi wanaotaka kusikiliza kesi hiyo wanatakiwa kuzingatia na kusikiliza kwa utulivu na amani bila kuleta vurugu yoyote.

Amesema kwa kuzingatia ibara ya 13(6) A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mazingira ambayo mshtakiwa amekuwa akikataa kushiriki kesi hiyo kwa njia ya mtandao.

"Kwa misingi ya utoaji haki, naelekeza mshtakiwa huyu tarehe ijayo, aletwe Mahakama ya Kisutu ili aweze kusikiliza kesi yake kwa njia ya kawaida," amesema hakimu Mhini wakati akitoa uamuzi.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawab Issa amedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya uamuzi na upande wa mashitaka wapo tayari kusikiliza.

Wakili Tawab amesema hawamuoni mshtakiwa hivyo wanaomba kujua alipo.

Tawab baada ya kutoa taarifa hiyo, Mrakibu wa Magereza, Juma Kapilima ameieleza Mahakama mtuhumiwa alijulishwa aende katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kusikiliza kesi yake kwa njia mtandao, lakini amesema hawezi kwenda kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao.

Kutokana na majibu hayo hakimu Mhini aliuliza mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Mpare Mpoki iwapo wapo tayari kusikiliza uamuzi huo nao walijibu wako tayari na kisha kutoa uamuzi.

Kwa mara ya kwanza Lissu alifikishwa Kisutu, Aprili 10, 2025, na kusomewa mashitaka matatu ya kutoa taarifa za uongo.


Walichokisema mawakili

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala amesema kwa hatua ambayo kesi hiyo ilifikia kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, ilitakiwa mhusika awepo mahakamani na kusaini nyaraka zinazohitajika.

Dk Nshala amesema upande wa mashitaka umesema kesi hiyo inaweza kusikilizwa mshtakiwa akiwa ndani kwa mantiki hiyo Mahakama haikukosea kwa uamuzi huo.

"Hizi ni hoja ambazo zilikuwa zinabishaniwa na upande wa utetezi uliwasilisha hoja nyingi sana ikiwemo haki ya mshtakiwa kuonana na mawakili wake, umma kushiriki kwenye kesi, kitu ambacho magereza waliwazuia mawakili wa mshtakiwa kumuona akiwa mahabusu," amesema Dk Nshala.

Naye Wakili Peter Kibatala amesema wamefurahia uamuzi wa Mahakama hiyo akitaja sababu kubwa ni kutokana na uamuzi uliohitaji ushujaa wa chombo hicho.

"Katika hoja zetu tunashukuru Mahakama imetusikiliza na tunaamini imejijengea heshima yakipekee siku hii ya leo, kikubwa tunaishukuru Mahakama kwa ujasiri," amesema Kibatala

Kulingana na Wakili Kibatala kesi hiyo inafuatiliwa na watu wote nchini na nje ya Tanzania na mahakama imejijengea heshima hadi nje kwani tangu Lissu kuwekwa gerezani kumekuwa na waangalizi wa kimataifa.

"Wapo mabalozi na wale wote wanabeba picha ya Mahakama zetu zinaweza kuwa na ujasiri. Tuendelee kutoa wito kwa wale tuliowakemea hivi karibuni wana kawaida ya kuongea barabarani basi wajionye na wajionye kwani tabia hiyo inaweza kuleta madhara kwa kesi," amesema.

Amesema ni muhimu kuiacha Mahakama ifanye shughuli zake kwa uhuru bila kuingiliwa na majibu yakishatolewa wanaweza kwenda kuzungumzia barabarani.

"Tulitoa ahadi tutapigania haki ya umma kusikiliza kesi hii na tunafurahi tumetimiza ahadi yetu na hatuna deni," amesema

Wakili huyo amesema kunapokuwa na haki lazima kuwepo na wajibu na Mahakama imewataka wanaohitaji kusikiliza basi wanapaswa kuzingatia nidhamu.

Pia alisisitiza kuzingatia jambo hilo kulingana na kazi iliyofanywa hadi kufanikiwa kwao kusikiliza.

"Wakija kusikiliza Mei 19, 2025 wawe watulivu na wasiwe na visingizio. Wajitahidi waje kwa wingi kadri wawezavyo na wajitahidi kuzingatia nidhamu na wasije kutuangusha mawakili tuliofanya kazi kubwa katika mazingira magumu," amesema Wakili Kibatala.


Imeandikwa na Hadija Jumane, Baraka Loshilaa na Tuzo Mapunda