Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Korti yatupilia mbali rufaa ya mhasibu dhidi ya jirani yake

Muktasari:

  • Mahakama ya Mwanzo Songea ilimtia hatiani mshtakiwa na kumuhukumu adhabu ya kutumikia huduma za kijamii kwa miezi sita na kumlipa jirani yake fidia ya Sh1.3 milioni.

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea, imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na Auleria Ngowi dhidi ya jirani yake, Pendo Lwema.

Mahakama ya Mwanzo Songea ilimtia hatiani Pendo na kumuhukumu adhabu ya kutumikia huduma za kijamii kwa miezi sita na kumlipa jirani yake (Auleria) fidia ya Sh1.3 milioni ndani ya mwezi mmoja katika kesi ya jinai ya mwaka 2024.

Rufaa ya Auleria inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Songea katika rufaa ya jinai iliyobatilisha hukumu dhidi ya Pendo na kufuta adhabu zilizotolewa kwake.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, James Karayemaha ametoa hukumu hiyo jana Mei 13, 2025 baada ya kusikiliza sababu za rufaa na kupitia mwenendo wa shauri.

Msingi wa rufaa

Katika Mahakama ya Mwanzo Songea, Pendo alishtakiwa kwa wizi akidaiwa kumwibia Auleria Sh1.3 milioni kinyume cha kifungu cha 258(1) na 265 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Alidaiwa kutenda kosa hilo Septemba 7, 2024, eneo la Ruhuwiko, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Katika kuthibitisha kesi, mlalamikaji aliita mashahidi watatu, mshtakiwa alijitetea yeye na alikuwa na shahidi mmoja.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Auleria na Pendo walikuwa majirani na kila usiku, Pendo alikwenda nyumbani kwa Auleria aliyekuwa mhasibu wa kikundi, ambako alimkuta akihesabu fedha.

Ilidaiwa Pendo alikuwa na tabia ya kuchukua mali za Auleria pasipo ridhaa yake, ukiwamo mkaa na kuvuna mboga kwenye bustani.

Siku ya tukio Auleria alidai alipigiwa simu saa saba mchana na shahidi wa kwanza aliyemweleza dirisha la nyumba yake lilikuwa wazi, huku grili likiwa limevunjwa.

Alieleza alipokwenda nyumbani kwake alifungua mlango kisha akakagua alipoweka Sh1.3 milioni na kugundua zimeibwa, hivyo akatoa taarifa Polisi.

Pendo alikamatwa na kufikishwa Mahakama ya Mwanzo Songea.


Kuhusu utetezi

Pendo aliileza Mahakama aliona dirisha la nyumba ya Aurelia likiwa katika hali ya kutiliwa shaka, akashuku kuwa limevunjwa, hivyo aliwafahamisha wazazi wa shahidi wa pili na majirani wengine.

Alieleza shahidi wa pili alimpigia Aurelia na kumtaka arudi nyumbani. Aliporejea na kuingia ndani Auleria alilalamika Sh800,000 zimeibwa na kwamba majirani wengine waliondoka yeye akabaki kumfariji.

Muda mfupi baadaye alisema aliondoka baada ya kuitwa na mumewe. Jioni Aurelia alimwambia anatakiwa kuripoti kituo cha polisi kwani yeye ni mshukiwa mkuu wa kosa hilo.

Mahakama ya Mwanzo baada ya kutathmini ushahidi wa pande zote mbili, ilieleza Auleria alithibitisha mashitaka pasipo kuacha shaka, hivyo ilimtia hatiani Pendo na kumuhukumu kutumikia huduma za kijamii kwa miezi sita na kumlipa fidia jirani yake Sh1.3 milioni.


Mahakama ya Wilaya

Pendo alikata rufaa Mahakama ya Wilaya Songea ambayo ilitengua hukumu ya Mahakama ya Mwanzo na kumfutia adhabu.

Mahakama hiyo ya kwanza ya rufaa iliridhika kwamba hukumu dhidi ya Pendo ilitokana na tuhuma na ushahidi wa tabia yake ya kumtembelea mrufani, na kuridhika kuwa Auleria alishindwa kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka yoyote.

Auleria alikata rufaa Mahakama Kuu akiwasilisha sababu tatu za rufaa.

Alidai Mahakama ya kwanza ya rufaa ilikosea kubatilisha uamuzi wa mahakama bila kuzingatia ushahidi wake, ilishindwa kuzingatia mazingira ya kesi na matumizi ya kanuni ya ushahidi uliothibitishwa na kushindwa kuzingatia kanuni ya kubatilisha mzigo wa ushahidi.

Auleria na Pendo hawakuwa na mawakili wa kuwawakilisha mahakamani. Rufaa ilisikilizwa kwa njia ya maandishi.

Mrufani Auleria aliibua hoja iwapo kosa la wizi lilithibitishwa kulingana na matakwa ya sheria na la pili, iwapo Mahakama ya kwanza ya rufaa ilijielekeza vibaya/ilikosea kisheria kwa kufuta uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo.

Hoja hiyo ililenga kubainisha vipande vya ushahidi wa kuunga mkono hoja kwamba alithibitisha shauri hilo pasipo kuacha shaka kwa mujibu wa matakwa yaliyoainishwa katika kifungu cha 3 (2) (a), kikisomwa pamoja na kifungu cha 8 na cha Sheria ya Ushahidi.

Alidai Pendo alihusishwa ipasavyo na kosa la wizi kupitia ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa tatu.

Alieleza matukio ya mlalamikiwa kuripoti tukio hilo kwa majirani kuwa dirisha lilivunjwa, kuingia kwenye nyumba ya mrufani na kuchota mkaa bila kibali kwa mujibu wa ushahidi wa tatu. Pia alidai Pendo alikuwa na tabia ya kukimbilia kwenye nyumba yake kuuliza masuala yake ya fedha kila anaporudi nyumbani kutoka kazini.

Alidai kwa ushahidi wa kimazingira unamuhusisha mlalamikiwa kutenda kosa hilo.

Alidai Mahakama ya kwanza ya rufaa ilifanya makosa kupuuza ushahidi wake kuwa siku moja kabla ya tukio, Pendo alikwenda kwake akamkuta akihesabu fedha, hivyo mahakama ilipaswa kumuamini.

Pendo kwa upande wake alieleza mrufani ameshindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake bila kuacha shaka.

Alitoa mfano wa kesi ya Magendo Paul na mwingine  dhidi ya Jamhuri (1993) TLR 2019, alikuwa na maoni kwamba ushahidi wa mrufani haukuwa na nguvu dhidi yake.

Kuhusu mwenendo wa kesi, alidai ushahidi uliotolewa ulikuwa wa madai tu na hauna uthibitisho wa moja kwa moja.

Akizungumzia ushahidi wa kimazingira, alieleza kitendo kwamba aliingia katika nyumba ya mtu siku iliyopita haimaanishi yeye ndiye aliiba pesa. Aliiomba Mahakama isikubaliane na rufaa hiyo.


Uamuzi wa jaji

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili Jaji amesema suala kuu la kuamuliwa ni iwapo mrufani alithibitisha mashitaka bila kuacha shaka yoyote.

Suala hilo alisema linaweza kushughulikiwa vyema ikiwa atarejea ushahidi wa mrufani.

Jaji alisema hakuna shahidi aliyemwona jambazi aliyevamia nyumba ya mrufani na kilichomuhusisha Pendo na kosa hilo ni kwa sababu alimtembelea Aurelia siku moja kabla ya wizi kutokea.

Alisema ushahidi hauelezi Pendo aliona mahali mrufani ameweka fedha hizo na kwamba, mrufani alitaja mazingira ambayo yalimsababisha kumuunganisha Pendo na kosa hilo, ikiwamo kumkimbilia nyumbani kwake kuuliza masuala yake ya kifedha pindi anapotoka kazini.

Jaji Karayemaha alisema kwa aina yoyote, ushahidi wa mrufani juu ya mazingira yanayozunguka una tafsiri nyingi kwa sababu suala la mjibu rufaa kuchota mkaa bila kibali, kumchunguza kuhusu masuala ya fedha haimaanishi yeye ndiye aliyevunja dirisha na hatimaye kuiba fedha hizo.

Baada ya kujadili sababu zote Jaji alisema anaungana na mahakama ya kwanza ya rufaa na kushikilia kuwa mrufani alishindwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka.

“Mahakama ya kwanza ya rufaa haikujielekeza vibaya katika kubatilisha uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo, natupilia mbali rufaa hii,” alisema jaji.