Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walichokubaliana Rais Samia, Stubb wa Finland

Muktasari:

  • Rais Stubb wa Finland amewasili Tanzania kwa ziara ya siku tatu ya kiserikali kuanzia leo Jumatano. Amefanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Serikali za Tanzania na Finland zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika maeneo mbalimbali huku zikiibua ushirikiano kwenye maeneo mapya kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Mei 14, 2025 Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake, Rais wa Finland, Alenxander Stubb ambaye yuko nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu.

Rais Stubb amewasili nchini leo Jumatano Mei 14,2025 na kufika Ikulu ambako alipewa heshima ya gwaride lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na kupigiwa mizinga 21.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania akimpokea Rais wa Finland, Alexander Stubb, Ikulu leo Mei 14, 2025. Picha na Ikulu.

Baada ya heshima hizo, wawili hao walikwenda kwenye mazungumzo na baadaye walizungumza na vyombo vya habari kuhusu mambo waliyojadiliana,  ikiwemo kuongeza ushirikiano baina yao ambao umedumu kwa miaka 60 sasa.

Akizungumzia ushirikiano huo, Rais Samia amesema wamekubaliana kuongeza uhusiano wao katika maeneo wanayofanya kazi kwa pamoja, ambayo ni sekta za misitu, biashara, uwekezaji, madini, utalii, elimu, uwezeshaji wanawake, Tehama na uhamilishaji wa teknolojia.

“Sote tulikubaliana kuwa kuna fursa ya kukuza ushirikiano katika maeneo hayo na tukaeleza utayari wetu kutumia fursa hizi kwa manufaa ya mataifa yetu,” amesema Rais Samia wakati wa mkutano wao na vyombo vya habari.

Katika sekta ya misitu, amesema Finland imekuwa ikiisaidia Tanzania katika utunzaji wa misitu na katika ziara hii, Rais Stubb kesho atazindua mpango unaolenga kuzijengea uwezo taasisi za mafunzo kwenye sekta hiyo  nchini.

Rais wa Finland, Alexander Stubb (suti nyeusi) akisindikizwa kukagua gwaride na Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Jacob Mkunda. Picha na IKULU. 

Amesema ameikaribisha Serikali ya Finland kushirikiana na Tanzania katika mkakati wake wa nishati safi ya kupikia, ili kuhakikisha inafikia malengo yake ya kufanya asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati hiyo ifikapo mwaka 2030.

“Vilevile, tumeikaribisha sekta binafsi ya Finland, tushirikiane kwenye kuongeza thamani kwenye madini yanayopatikana nchini ili tuongeze thamani kwa ajili ya masoko ya nje,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amebainisha kwamba kwenye mazungumzo yao walikubaliana kuongeza maeneo mengine ya ushirikiano hasa yale  muhimu kama vile uchumi wa buluu, nishati na elimu kwa manufaa ya watu wao.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania (Kulia) akiwa amesimama na Rais wa Finland, Alexander Stubb (Kushoto) wakati wa kuimba nyimbo za mataifa hayo. Picha na Ikulu.


Kisiasa, Rais Samia amesema Tanzania iliwasilisha pendekezo la kuanzisha uhusiano wa kibunge ili kuwa na jukwaa la kuzungumzia yanayotokea kwenye nchi zao. Pia, wamekubaliana kuendelea na mashauriano ya kidiplomasia na kuratibu ziara za biashara za wadau wa sekta binafsi.

“Katika kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji, tumekubaliana kuchochea ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina yetu na ndani ya Afrika,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amemweleza mgeni wake nia ya Tanzania kutaka kuongeza idadi ya watalii kutoka Finland, mwaka jana kulikuwa na watalii 5,067 na robo ya kwanza ya mwaka huu kuna watalii 1,276, hivyo ameomba washirikiane katika kukuza utalii.

Rais wa Finland, Alexander Stubb akisaini kitabu cha wageni Ikulu ya Tanzania jijini Dar es Salaam. Pembeni yake ni Rais Samia Suluhu Hassan. Picha na Ikulu. 

“Nimemshukuru Rais Stubb kwa msaada ambao Finland imekuwa inatoa katika sekta ya elimu, hususan katika eneo la ufundi stadi wa kidijitali na kuwajengea uwezo walimu. Tumeomba kuimarisha ushirikiano katika sekta hii na kuangalia pia njia za ziada za kubadilishana ujuzi,” amesema.

Kwenye eneo la teknolojia, Rais Samia amesema: “Tumewakaribisha katika kuongeza ushirikiano kwenye eneo la kidijitali kwenye vituo atamizi, kwa ajili ya kampuni changa, kuimarisha huduma za Serikali mtandao na usalama wa mtandao kwa ujumla.”

Kwa upande wake, Rais Stubb amesema wamekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Tanzania na ziara yake inalenga kuimarisha ushirikiano huo kwa pande zote mbili hasa kwenye masuala ya maendeleo.

Amesema wanaamini katika usawa, ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na Tanzania imekuwa na sehemu kubwa kwenye mioyo ya raia wa Finland.

Rais huyo ambaye aliwahi kuja Tanzania miaka 22 iliyopita, akiwa Waziri wa Biashara, amesema barani Ulaya wana vita moja kati ya Ukraine na Russia ambapo nchi moja inajaribu kuikosesha nchi nyingine uhuru wake kama dola.

“Tumekuwa na uzoefu wa vita ya pili ya dunia (WWII) ndiyo maana tunafanya jitihada kuhakikisha sheria za kimataifa zinaheshimiwa, kwamba Ukraine inashinda vita na kupata amani ya muda mrefu,” amesema.

Amesema wamezungumzia suala la amani ya kikanda, mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kijinsia na maeneo mengine ya ushirikiano.

“Katika mazungumzo yetu tulikubaliana kwamba malengo yetu si tu kuwa na uhusiano mzuri, bali kufanya kazi pamoja kudumisha sheria za kimataifa. Lengo letu ni jambo hilo kuakisi Afrika nzima,” amesema.