ATF yafundwa kupata fedha za afua za Ukimwi

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi akizungunza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF)
Muktasari:
- Baada ya Serikali kuanzisha tozo kwa ajili ya kugharamia afya za Ukimwi na Bima ya Afya kwa Wote, imeitaka Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF), kubuni vyanzo vingine vya mapato.
Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi ameielekeza Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF) kubuni mbinu za ndani za kutafuta fedha za kugharamia afua za Ukimwi, kufuatia kupungua kwa misaada ya wahisani kwa takriban asilimia 40.
Amesisitiza umuhimu wa kujitegemea kifedha ili kuhakikisha uendelevu wa mapambano dhidi ya Ukimwi nchini.
Kupungua kwa misaada hiyo kunatokana na uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa kupunguza msaada wa kibajeti kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, hatua ambayo imeathiri ufadhili wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo afua za Ukimwi.
Akizungumza leo Juni 26, 2025 wakati akizindua bodi ya mfuko huo, Lukuvi amesema katika kuimarisha uendelevu wa mfuko huo, bodi inapaswa kuwa na dira pana na mkakati wa muda mrefu wa kuhakikisha mfuko huo unakuwa thabiti.
“Ni muhimu kuwa Mpango Mkakati wa Uendelevu wa ATF unaoendana na Dira mpya ya Maendeleo ya 2050 ambao utaongoza juhudi za kizazi kipya cha mapambano dhidi ya VVU (virusi vya Ukimwi na Ukimwi nchini,”amesema.
Lukuvi amesema kampeni za kitaifa za uhamasishaji wa kuchangia mfuko huo zinaweza kuanzishwa kwa ubunifu mkubwa.
Amesema bodi inayo nafasi ya kuchukua hatua madhubuti za kuhamasisha kuvutia raslimali za ndani kwa kushirikisha sekta binafsi, diaspora, taasisi za fedha na makundi mengine ambayo bado hayajatumika vya kutosha.
“Vilevile ni muhimu kufanya mapitio ya mifumo ya sasa ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha ili kuhakikisha mifumo thabiti, shirikishi, yenye uwazi na inayozingatia viwango vya juu vya uwajibikaji,” amesema.
Lukuvi amesema bodi hiyo pia inapaswa kuweka utaratibu wa mara kwa mara wa kujitathimini kwa kutumia viashiria vya Taifa vya Uendelevu wa Ukimwi ambavyo vitasaidia kubaini maeneo yenye mafanikio na yale yanayohitaji maboresho ya haraka.
Amesema kampeni za kitaifa za uhamasishaji wa kuchangia mfuko huo zinaweza kuanzishwa kwa ubunifu mkubwa.
“Sambamaba na hayo ni muhimu bodi ikachunguza na kufungua milango ya ubunifu mpya wa raslimali kupitia mifumo kama Blended Financing), ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi pamoja na uvumbuzi wa kifedha kama Health Bonds au Impact investiments Fund ambazo tayari nchi nyingine zimeanza kutumia kwa mafanikio makubwa,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk James Kilabo amesema kupitia bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2025/26, Serikali imeanzisha tozo ya uwajibikaji wa Ukimwi (HIV response Levy (HRL).
Amesema tozo hiyo itatozwa kupitia vyanzo vya kodi nane na kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kuwa tozo hiyo pekee haitoshi kugharamia mahitaji ya mwitikio wa Ukimwi nchini.
“Bodi mpya ina dhamana kubwa ya kuongoza mchakato wa kuongeza wigo wa vyanzo vya raslimali za ndani kwa ubunifu, ushirikiano mpana na kwa ufanisi wa hali ya juu,” amesema Dk Kilabo.
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDs), Dk Catherine Joachim amesema athari za kutegemea kwa kiwango kikubwa misaada kutoka kwa wafadhili wa nje ya nchi zimeanza kujitokeza ambapo Serikali ya Marekani imesitisha kutoa baadhi ya misaa iliyokuwa imepanga kutoa nchini.
“Aidha, Global Fund pia imesitisha ufadhili wao kwenye baadhi ya shughuli ambazo zilipangwa kutekelezwa nchini. Baadhi ya maeneo ambayo yanakwenda kuathirika baada ya wafadhili hawa wakubwa kubadili sera yao ya misaada ni pamoja na tiba, kinga, matunzo na utengamano,” amesema.
Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto ya utegemezi mkubwa wa raslimali za nje katika kutekeleza afua za ukimwi nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya ATF, Sabasaba Moshingi amesema kwa pamoja wamepokea majukumu, maelekezo na changamoto ambapo walimhakikishia kuwa watajitahidi kadri ya uwezo na weledi wao kusimamia na kuongoza bodi hiyo.
Katika bajeti ya mwaka 2025/26, Serikali ilipitisha tozo za kugharamia shughuli hizo na Bima ya Afya kwa Wote kutoka katika ushuru wa bidhaa za vinywaji vya kilevi, huduma za mawasiliano ya kieletroniki,mafuta ya petrol, dizeli na taa.
Maeneo mengine ni kwenye madini, michezo ya kubahatisha, magari na mashine zinazoagizwa kutoka nje ya nchi pamoja na Sh500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji wa njia ya treni na Sh100 kwa usafiri wa njia ya anga.