Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dawa kuzuia maambukizi VVU sasa rasmi

Muktasari:

  • Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) imeidhinisha sindano ya lenacapavir kwa ajili ya kinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) imeidhinisha sindano ya lenacapavir kwa ajili ya kinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), hatua ambayo imepongezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hatua ya FDA inafuatia matokeo yaliyoonyesha matumaini katika majaribio mawili ya awali (Purpose 1 na 2) yaliyofanyika mwaka 2024.  

Majaribio hayo yalionyesha usalama na ufanisi wa lenacapavir katika makundi mbalimbali ya watu na mazingira tofauti.

Jaribio la kwanza (Purpose 1) lilishirikisha wasichana wa  rika balehe na wanawake 5,345 wenye umri wa miaka 16 hadi 26 katika vituo 25 nchini Afrika Kusini na vitatu Uganda. Umri wa wastani wa washiriki ulikuwa miaka 21.

Jaribio la pili (Purpose 2) liliwashirikisha washiriki 3,267 wakiwamo wanaume na wale waliobadili jinsia (wanawake na wanaume) wenye umri wa miaka 16 na kuendelea, wanaojihusisha na ngono. Jaribio hilo lilifanyika katika vituo 88 nchini Argentina, Brazil, Mexico, Peru, Afrika Kusini, Thailand na Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa leo Juni 19, 2025 na tovuti ya WHO, chanjo ya lenacapavir huchomwa mara mbili kwa mwaka na hutoa kinga ya muda mrefu, hivyo kuongeza wigo wa chaguo za kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.

WHO kwa sasa inapendekeza dawa ya kumeza ya PrEP, pete ya ukeni ya dapivirine na sindano ya muda mrefu ya cabotegravir (CAB-LA) kama chaguo la kuzuia maambukizi ya VVU kabla ya kujamiiana (PrEP).

Lenacapavir, ikiwa na mfumo wa siri na wa muda mrefu wa kuchomwa sindano, inaweza kusaidia kuondoa changamoto kuu kama vile mzigo wa kumeza dawa kila siku, kutembelea kliniki mara kwa mara na unyanyapaa unaohusishwa na kinga dhidi ya VVU.

"Hatua hii ya kisheria inatufanya kusogea karibu zaidi na kupanua upatikanaji wa chaguo jipya la ubunifu katika kinga dhidi ya VVU kupitia Lenacapavir," amesema Dk Meg Doherty, mkurugenzi wa Mpango wa kimataifa wa WHO wa VVU, homa ya ini na magonjwa ya zinaa.

Amesema: "WHO ina jukumu muhimu katika kusaidia nchi kupitia uandaaji wa miongozo, upangaji wa ubora na michakato ya udhibiti. Tunafanya kazi na washirika na mamlaka za kitaifa kuhakikisha lenacapavir inawafikia wale wanaoihitaji zaidi kwa haraka, usalama na kwa usawa."

WHO imesema miongozo kuhusu matumizi ya lenacapavir kwa sindano itatolewa Julai 14, 2025 wakati wa mkutano wa kimataifa wa Ukimwi, utakaofanyika Kigali, nchini Rwanda.

Mbali ya hayo, uidhinishaji uliofanywa na FDA pia unafungua njia kwa upangaji wa ubora wa WHO, hatua inayoweza kuharakisha uidhinishaji wa kitaifa, baada ya kuidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti (SRA) na kununuliwa na mashirika wafadhili kama Global Fund.

Sambamba na hilo, WHO inashirikiana na Wakala wa Dawa wa Ulaya (EMA) kusaidia mpango wa dawa kwa wote (Medicines 4 All -M4All), ambao hurahisisha njia za udhibiti kwa nchi zinazopitisha matumizi ya lenacapavir.


Maoni ya wadau

Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi akizungumza na Mwananchi leo Juni 19, 2025 amesema ili dawa iweze kuingia nchini kuna utaratibu maalumu unaotumika.

Amesema kuna kamati ya tiba na dawa ya kitaifa, pia kampuni ambazo ndizo huzisajili na kuziingiza nchini, akieleza hivi sasa dawa nyingi za VVU/Ukimwi Taifa zinategemea misaada, kwa hiyo kama WHO imeidhinisha na Global Fund wakaipitisha, itaingia nchini na itatumika.

"Lakini kama haitaingia kwa utaratibu huo, tuna utaratibu wetu wa ndani ambao mtu anaisajili, kamati inakaa inaangalia gharama, uwezo wa nchi na zikiingia zinaingizwa kwenye mwongozo wa matibabu, kisha zinaanza kutumia," amesema.

Dk Isaac Maro, mtaalamu wa masuala ya afya aliyefanya tafiti kadhaa katika masuala ya VVU na Ukimwi, amesema kwa mwaka huu pengine hiyo ndiyo taarifa njema zaidi kwenye mapambano ya kusaka dawa, akisema ni mwelekeo mzuri.

Daktari bingwa wa mifupa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Shadrack Mwaibambe amesema WHO kuipitisha dawa hiyo ni ishara nzuri kwamba dunia bila VVU inawezekana.

Amesema anaamini jitihada nyingi zilizopo itafikia hatua hata walio na maambukizi watapatiwa dawa.

"Sisi madaktari tungeiomba Wizara ya Afya na taasisi inayohusika waharakishe taratibu ili dawa hii iingie nchini ili Tanzania iweze kutumia kwa uharaka," amesema.

Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema dawa hiyo imekuwa ikifanyiwa utafiti kwa kipindi kirefu, hivyo kuanza kutumika ni hatua kubwa katika sekta ya afya.

"Dawa hii ya sindano itawaondolewa wagonjwa kumeza dawa kila siku, inakaa kwa muda unachoma nyingine, vidonge baadhi ya watu viliwapa usugu, sasa hii itashusha kiwango cha maambukizi nchini," amesema.