Serikali yaanza kununua ARVs, kufufua kiwanda cha uzalishaji Arusha

Muktasari:
- Kwa kipindi kirefu, Tanzania ilitegemea dawa za ARVs kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).
Dodoma/Dar. Wizara ya Afya imeweka wazi kuwa tayari imeanza kununua dawa za ARVs za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU), na tayari Sh93 bilioni zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo na bidhaa za kifua kikuu na malaria Machi hadi Juni, 2025.
Wizara imeeleza hayo wakati ikiliomba Bunge kuidhinisha Sh1.61 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbe 10, ikiwamo kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Kwa kipindi kirefu, Tanzania ilitegemea dawa za ARVs kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Jumatatu, Juni 2, 2025, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema wametenga Sh202 bilioni zitakazotumika kukabiliana na mabadiliko hayo ya sera.
Mhagama amesema katika kukabiliana na athari hizo katika sekta ya afya, wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya tathmini ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Amesema wametenga Sh202 bilioni kwa ajili ya kutumika Machi hadi Juni, 2025.
“Kati ya fedha hizo, Sh93 bilioni tayari zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa za ARVs, bidhaa za kifua kikuu na malaria,” amesema Mhagama.
Pia, amesema Serikali imeongeza bajeti ya dawa kwa wizara hadi kufikia Sh300 bilioni kwa mwaka 2025/26 kutoka Sh200 bilioni za mwaka 2024/25 na kuwa ongezeko hilo litawezesha ununuzi wa ARVs pamoja na dawa nyingine muhimu.
“Naomba kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa, Serikali imejipanga katika kuhakikisha dawa hizo muhimu zinapatikana kwa walengwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kama kawaida,” amesema.
Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za tiba dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza na ya mlipuko, Sh173.94 bilioni zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali.
Afua hizo ni kufufua Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industry (TPI) kilichopo Arusha kuanza kuzalisha ARVs.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema mkakati wa Serkali katika kuelekea kuwa na hali ya kujitegemea ulianza muda mrefu hata kabla ya utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Profesa Aloyce Ndakidemi ameuliza ni nini mkakati wa Serikali katika kukabiliana na masharti magumu ya kuondoa misaada kwa nchi maskini kulikofanywa na Rais Donald Trump.
Waziri Nchemba amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza mapato ya ndani ili kuhakikisha sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa kwa kutumia mapato ya ndani.
"Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mahitaji ya kibajeti, Serikali itaendelea kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia njia mbadala ikiwamo ubia kati ya sekta ya umma na binafsi," amesema Dk Nchemba.
Waziri amesema mkakati huo utakwenda kusaidia kuipunguzia Serikali mzigo wa kukopa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa kibajeti, kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Akitoa maoni yake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Mugisha Nkoronko amesema wanaunga mkono jitihada hizo, kwa Serikali kuziba nakisi inayotokana na Marekani kujiondoa.
“Ni jambo la kupongeza na kujivunia imechukua jitihada zaidi kuhuisha kiwanda cha dawa, MAT tunaunga mkono, tunatamani kuwe na viwanda vingi zaidi tuzalishe vifaa tiba vyetu sisi wenyewe na tuuze masoko ya Afrika kwani tuna miundombinu ya bandari pia,” amesema Dk Mugisha.
Fedha zitakavyotumika
Akisoma bajeti ya wizara hiyo, Waziri Mhagama amesema kati ya fedha zinazoombwa Sh991.75 bilioni zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 61 ya bajeti inayoombwa.
Amesema Sh49.8 bilioni zitaimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini, kwa kuanza kugawa kadi za bima kwa makundi mbalimbali pamoja na, “kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote nchini, kwa kuanza kutoa kadi za bima ya afya kwa makundi mbalimbali.”
Mhagama amesema Sh166.01 bilioni zitatumika katika kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwamo ya milipuko, yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, yasiyoambukiza na huduma za lishe.
Amesema miongoni mwa afua ambazo fedha hizo zitatumika ni kuendelea kuimarisha huduma za afya mipakani kwa kujenga miundombinu ya kuwatenga wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza katika mipaka 16.
Kipaumbele kingine amesema ni kuimarisha upatikanaji bora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi Taifa, huku Sh309.51 bilioni zikitengwa kutekeleza afua mbalimbali.
Mhagama amezitaja miongoni mwa afua zitakazotekelezwa ni kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ikiwamo matumizi ya akili mnemba na kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya ya Jamii.
Pia, zitatumika katika kuimarisha Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuwa na hadhi ya Hospitali ya Taifa na kuanzisha kituo cha kimataifa cha upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kitakachoongoza kwa ukubwa katika ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara.
Pia, afua nyingine ni kuendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya (dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi) kwa kuboresha mifumo ya maoteo, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa dawa na bidhaa nyingine katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya.
“Kuendelea kufanya tafiti na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti hizo kwa maeneo ya kimkakati, Sh4.46 bilioni zitatekeleza afua mbalimbali,” amesema.
Amesema Sh76.57 bilioni zimetengwa kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Mhagama amesema Sh80.38 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalamu katika sekta ya afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi.
Pia, amesema katika kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi na tiba utalii nchini zimetengewa Sh123.93 bilioni.
Amesema tiba mbadala zimetengewa Sh937.29 milioni, afya ya akili, utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu zimetengwa Sh6.61 bilioni.
Matibabu mapya
Katika kuendelea kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, Mhagama amezitaja baadhi ya huduma hizo ni upandikizaji wa ini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kampasi ya Upanga na kuanzisha huduma bobezi za mfumo wa mkojo na uzazi kwa wanaumekatika Hospitali ya Taifa Muhimbili kampasi ya Mloganzila.
Ametaja huduma nyingine itakayoanzishwa ni upasuaji na ubadilishaji wa mabega na viwiko katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili.
Mhagama amesema kuendelea kutoa huduma ya upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo, nyonga na magoti kwa kutumia mfumo wa akili mnemba katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili.
Afua nyingine ni kuanzisha kiwanda cha kuzalisha viungo tiba na viungo saidizi Hospitali ya Kanda KCMC.
Hata hivyo,Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imesema kuwa Bohari ya Dawa (MSD) inaidai Serikali jumla ya Sh434.2 bilioni kutokana na huduma za ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma nchini.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo bungeni, Mwenyekiti wake, Elibariki Kingu amesema madeni hayo yamegawanyika katika makundi mawili.
Amelitaja kundi la kwanza ni zile dawa zilizotolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa matarajio ya kulipwa baadaye na la pili ni gharama za utunzaji na usambazaji wa bidhaa za miradi maalumu baada ya Serikali kukubali kuchangia.
“Hadi kufikia Machi 2025, vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoko chini ya Wizara ya Afya vinadaiwa Sh46.4 bilioni huku vile vilivyo chini ya Ofisi ya Rais – Tamisemi vikidaiwa Sh83.1 bilioni,” amesema Kingu.
Pia, Kamati imeishauri Serikali kukamilisha mchakato wa kuandaa sheria itakayosimamia huduma ya uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa chembechembe na viungo vya binadamu, ili kuweka msingi madhubuti wa utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Kingu amesema ni muhimu kwa Serikali kuweka mfumo wa kisheria utakaowezesha huduma hiyo kutolewa kwa ufanisi, usalama na kwa kuzingatia haki za binadamu.
Aidha, kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, kamati hiyo imeshauri Serikali kuongeza juhudi za kupambana nayo kwa kufanya tafiti za kina kubaini ukubwa wa tatizo, kutoa elimu kwa umma juu ya vyanzo na njia za kujikinga, huku ikisisitiza umuhimu wa lishe bora na mazoezi ya mwili.