Zitto ataka timu ya Makamishina kuchunguza kifo tata Kokonko

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwenge mjini Kakonko Novemba 16, 2023 ambapo amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Cammilius Wambura kuunda kamati ya Makamishina wa Jeshi hilo kuchunguza kifo tata cha kijana Enos Elias kinachodaiwa kutoka akiwa mikononi mwa vyombo vya dola. Picha na Sunday George
Muktasari:
Kifo ha kijana Enos ambaye enzi za uhai wake alikuwa akijishughulisha na kilimo na ujasiriamali kimegubikwa na utata baada ya kutoweka kwa siku kadhaa kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa na watu wasiofahamika ndani ya pori la Kichacha Kijiji cha Chilambo kilometa kadhaa kutoka mjini Kakonko.
Kakonko. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazaledno, Zitto Kabwe amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura kuunda kamati ya Makamishina wa Polisi kutoka makao makuu kuchunguza kifo cha Enos Elias (20), mkazi wa Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko ambaye mwili wake ulikutwa umezikwa porini.
Kifo ha kijana Enos ambaye enzi za uhai wake alikuwa akijishughulisha na kilimo na ujasiriamali kimegubikwa na utata baada ya kutoweka kwa siku kadhaa kabla ya mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa na watu wasiofahamika ndani ya pori la Kichacha Kijiji cha Chilambo kilometa kadhaa kutoka mjini Kakonko.
Kabla ya kutoweka na baadaye mwili wake kufukuliwa porini, kijana huyo anadaiwa kuwapigia simu ndugu zake akiwajulisha kuwa yuko mikononi mwa maofisa wa Jeshi la Uhamiaji wilayani Kakonko na kuomba atumiwe namba ya utambulisho wa kitambulisho cha Taifa (Nida) ya mama yake mzazi, Juliet Joseph kuthibitisha uraia wake.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Kakonko leo Novemba 16, 2023, muda mfupi baada ya kutoka Kijiji cha Ilabilo alikoenda kuhani msiba na kuipa pole familia ya kijana Enos, Zitto ameshauri viongozi wa Serikali, watendaji na watumisha wa taasisi zinazotajwa kuhusika kwa njia moja au nyingine na kifo kuwekwa kuruhusu uchunguzi huru.
“DC (Mkuu wa Wilaya), OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) na Mkuu wa Uhamiaji wawajibike kwa kuondoka Kakonko kwa kutowasimamia vema watumishi walio chini yao wanaotuhumiwa kumshikilia Enos ambaye baadaye amekutwa amefariki,’’ amesema Zitto
Amesema wakati uchunguzi wa kifo hicho unaendelea, maofisa Uhamiaji waliohusika kwenye tukio la kumkamata kijana huyo kabla ya kukutwa na mauti wanapaswa kuwekwa chini ya ulinzi ili wasiharibu uchunguzi.
Zitto ambaye yuko kwenye ziara ya kichama katika majimbo yote ya uchaguzi Mkoa wa Kigoma amemshauri Kamishinda Jenerali wa Uhamiaji Dk Anna Makakala kufika Kakonko kuitembelea, kuipa pole na kuiomba radhi familia ya Enos anayedaiwa kutoweka akiwa mikononi mwa maofisa wa Uhamiaji.
‘’Katika hili, ACT-Wazalendo tutasimama na familia tunalitaka Jeshi la Polisi kutimize wajibu kwa kufuatilia mawasiliano ya simu ya marehemu kujua kilichotokea kabla hajatoweka na baadaye mwili wake kukutwa ukiwa umezikwa porini,’’ amesema Zitto
Kiongozi ambaye yuko kwenye ziara ya kichama katika majimbo ya uchaguzi Mkoa wa Kigoma ameisihi familia na wananchi wa Kijiji cha Ilabilo kuwa watulivu wakati uchunguzi wa kifo cha kijana Enos aliyezikwa juzi Novemba 14, 2023 katika makaburi ya umma Kijiji cha Ilabilo unaendelea.
Polisi, Kamati ya RC
Wito wa Zitto kwa IGP kuunda kamati ya Makamishina unatolewa huku tayari Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake, David Misime imetangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu kifo hicho na kuwataka wenye taarifa zitakazosaidia uchunguzi huo kukamilika wajitokeze.
Wakati Jeshi la Polisi likitangaza kuanzisha uchunguzi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mwanamvua Mrindoko ameunda kamati ya watu sita kuchunguza suala hilo na kuipa siku saba kukamilisha kazi hiyo
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Novemba 16, 2023, Ofisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Andrew Mrama amesema kamati hiyo ambayo tayari imeanza kazi imeundwa Novemba 15, 2023.
‘’Siwezi kumtaja mwenyekiti wala wajumbe wa kamati kwa sababu iko chini ya Kamati ya Usalama Mkoa…ninachoweza ni kuthibitisha kuwa ni kweli imeundwa na tayari imeanza kazi,’’ amesema Mrama
Kilio cha familia
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Juliet Joseph, mama mzazi wa kijana Enos amesema yeye, familia na jamii wanaamini kijana huyo amefikwa na mauti akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa vyombo na taasisi za Serikali.
Amesema mara ya mwisho kuwasiliana na familia, Enos alikuwa mikononi mwa watu aliowataja kuwa ni maofisa Uhamiaji waliomtuhumu kuwa hakuwa raia wa Tanzania, hivyo uchunguzi unapaswa kuanzia ndani ya Jeshi la Uhamiaji na Polisi alikohifadhiwa kwa siku moja kabla ya kukabidhiwa kwa maofisa Uhamiaji.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Angel Elias ambaye ni dada wa Enos akisema ndiye aliyezungumza naye kwa njia ya simu Jumamosi Oktoba 28, 2023 akimtaka kumtumia namba ya kitambulisho cha mama yao ili awathibitishe uraia wake kwa maofisa Uhamiaji waliokuwa wanamshikilia.
‘’Wakati nazungumza naye, mimi na mama tulikuwa shambani; na kwa sababu namba ile ilikuwa imeandikwa kwenye karatasi ambayo ilikuwa nyumbani kwa wakati huo, ilibidi mama arejee nyumbani kuichukua lakini tulishindwa kumtumia baada ya simu yake kutopatikana hewani,’’ amesema Angel
Kupotea, maiti kukutwa porini
Anasema kutokana na maelezo ya Enos kuwa alikuwa anashikiliwa na maofisa Uhamiaji, ndugu yao mwingine aliyemtaja kwa jina la Leopold Kisondoka alianza jitihada za kumtafuta kwa kwenda Kituo cha Polisi Kakonko na ofisi za Uhamiaji bila mafanikio.
‘’Jambo la kustaajabisha, wote Uhamiaji wanaodaiwa kumkamata na Jeshi la Polisi alikohifadhiwa usiku wa Ijumaa Oktoba 27, 2023 walikana kumshikilia wala kujua taarifa za kaka Enos,’’ anasema Angel
Amesema licha ya kuendelea kufuatilia aliko ndugu yao kuanzia Jumapili ya Oktoba 29, 2023 hadi Jumanne Oktoba 30, 2023, maofisa wa taasisi hizo mbili waliendelea kushikilia maelezo ya kutofahamu lolote kuhusu Enos hadi Ijumaa Novemba 3, 2023, walipopigiwa simu kukitakiwa kufika Kituo cha Polisi Kakonko ambako walitakiwa kwenda kufukua kaburi lililoonekana katika pori la Kichacha, umbali wa zaidi ya kilometa 25 kutoka Kakonko mjini.
‘’Tuliongozana na askari hadi porini na baada ya kaburi kufukuliwa na mwili kutolewa, mama aliutambua kuwa ni wa marehemu kaka Enos kutokana na alama iliyokuwa nayo kwenye meno,’’ amesema.
Familia yagomea maiti
Kutokana na utata wa kifo hicho, William Sabakwisi, baba mdogo wa marehemu Enos anasema familia iligoma kuchukua mwili wa Enos kushinikiza uchunguzi.
‘’Kwanza familia ilichukizwa jinsi polisi na uhamiaji ilivyowazungusha kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Enos; pili ilitaka Leopold Kisondoka aliyekamatwa na polisi kwa kuwa mtari wa mbele kufuatilia tukio hilo aachiwe huru bila masharti.
‘’Familia iliamini kitendo cha kumshikilia Leopold ambaye ndiye alikuwa kinara wa kumtafuta Enos ililenga kumbambikia kesi kuwalinda wauaji,’’ amesema Sabakwisi
Baada ya majadiliano, polisi walimwachia Leopold na familia ikakubali kuchukua mwili ambaye alizikwa katika makaburi ya umma Kijiji cha Ilabilo Novemba 14, 2023.