ACT yalalamikia hujuma uchaguzi, ZEC yajibu

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akionesha baadhi ya kura ambazo alidai zilipangwa kuingizwa kwenye vituo katika uchaguzi mdogo wa Mtambwe. Picha na Muhammed Khamis
Unguja. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amelalamikia hujuma katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Mtambwe, Pemba uliofanyika Oktoba 28, 2023, huku Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikieleza kushangazwa na madai hayo.
Kulingana na Zitto, hujuma kama hizo ndizo zilizo haribu uchaguzi wa mwaka 2020 na ndio maana wanatarajia kufanya kongamano Desemba 8 mwaka huu kutathmini mwenendo wa Serikali wa Umoja wa Kitaifa (SUK) ndani ya miaka mitatu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi amekanusha kuwepo kwa hujuma katika uchaguzi huo, akisema hawajapokea malalamiko kutoka kwenye chama hicho.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana katika ofisi za chama hicho, Vuga, Zitto aliorodhesha mambo 15 yaliyofanyika katika uchaguzi huo, ambayo wanaamini ni hujumu.
Mambo hayo ni njama ya kumtengenezea Mgombea wa ACT Wazalendo kitambulisho bandia cha ukaa (ZAN ID) ili kumuondolea sifa za kuwa mgombea na msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Mtambwe kufanya njama kumwengua mgombea huyo, kabla hajarejeshwa na Tume baada ya kukata rufaa.
Pia alisema daftari la wapigakura lilikuwa na mapandikizi wengi na wasimamizi wa uchaguzi waliwapatia kura zaidi ya moja.
Kiongozi huyo aliwashutum watendajji wa ZEC kuingia kwenye vituo wakiwa na kura mifukoni na kuzitumbukiza kwa nguvu kwenye masanduku ya kura wakati wa kusehabu kura.
“Karatasi za kura kuzagaa mikononi mwa makada wa CCM nje ya vituo, wasimamizi kuwaruhusu watu ambao si wapiga kura wa Jimbo la Mtambwe kupiga kura, kuharibu kura kwa makusudi kwa kuzitia wino, kuzichora au kutokugonga muhuri kwa karatasi ambazo mpigakura anaaminika anatoka ACT Wazalendo.”
Mambo mengine ni wasimamizi wa kura kukataa kuhakiki vishina vya kura katika vituo vyote vilivyolalamikiwa kuongezwa au idadi ya kura katika fomu au kuingizwa kura zisizo halali.
Wasimamizi wa kura wakati wa kujaza fomu za matokeo kuongeza idadi ya kura kwa mgombea wa CCM na kupunguza kura za mgombea wa ACT, baadhi ya kura za Mgombea wa ACT kupewa mgombea wa CCM wakati wa kuhesabu.
Akizungumzia mamamiko hayo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi alisema wakati uchaguzi huo unafanyika yeye na viongozi wote wa tume walikuwa Mtambwe na walipita kila kituo kuwahoji mawakala wa vyama vyote na hakuna aliyelalamika kuvurugwa kwa utaratibu.
“Sisi wenyewe tunashangazwa na haya yanayosemwa vyama vya siasa vinajua utaratibu ni vizuri kuufuata.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto alisema “huu ni unafiki kwa sababu unawezaje kuihusisha Serikali na mambo yote hayo na bado unakuwa sehemu ya mfumo unaokulipa mshahara?”
Alisema kama chama hicho hakiridhishwi, kinapaswa kujitoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa sababu hiyo haitakuwa mara ya kwanza.