Zanzibar: Ubakaji kinara matukio ukatili, udhalilishaji

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Atanas Paul; matukio ya ubakaji yameongoza kwa kuwa na idadi kubwa (3,073), yakifuatiwa na matukio 1,089 ya shambulio la mwili.
Unguja. Matukio 6,461 ya ukatili na udhalilishaji yameripotiwa kwa kipindi cha kuanzia 2017 hadi 2022, yakihusiana na ubakaji, ulawiti, utoroshwaji na mashambulio ama la kuudhuru mwili au lile la aibu, serikali imesema.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Atanas Paul; matukio ya ubakaji yameongoza kwa kuwa na idadi kubwa (3,073), yakifuatiwa na matukio 1,089 ya shambulio la mwili.
Aidha, matukio mengine na idadi yake katika mabano ni kama ifuatavyo; utoroshaji (805), kulawiti (728), shambulio la aibu (526) na kuingiliwa kinyume na maumblie (240).
Naibu Waziri huyo ameyasema hayo wakatia akijibu swali la Mwakilishi wa Mwera (CCM), Mihayo Juma Suleiman kuhusu matukio ya udhalilishaji.
"Kwa mwaka 2022, jumla ya matukio 1,360 yameripotiwa lakini waathirika wa matukio hayo walikuwa ni 1,361 wameripotiwa katika vituo vya polisi ambapo wanawake 185 sawa na asilimia 13.6, wanaume 3 sawa na asilimia 0.2," amesema na kuongeza
"Watoto walikuwa ni 1,173 kati ya hao wakike ni 889 sawa na asilimia 75.8 na watoto wa kiume ni 284 sawa na asilimia 24.2."
Naibu Wazir Anna ametoa wito wanawaume kuripoti matukio ya ukatii na udhalilishaji wanayofanyiwa kwani kuongezeka kwa uelewa kumesababisha wanaume pia kuathirika na kwamba serikali pia imeanza kukusanywa takwimu za wale wanaotoa taarifa.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa taarifa za kesi za udhalilishaji kwenye taasisi nyingine ingawa wizara ikishirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu tayari imetoa nyenzo za kukusanyia taarifa hizo kwa taasisi zinazohusiana na udhalilishaji.
Akijibu swali la mwakilishi wa Konde (CCM) Zawadi Amour Hassan aliyetaka kujua jinsi wizara zinavyoshirikiana kutoa taarifa hizo kwa madai zimekuwa zikitofautiana.
Anna amesema Wizara kwa kushirikiana na ofisi ya Mtakwimu Mkuu itatengeneza nyenjo na mfumo mzuri wa kukusanya taarifa hizo, na kwamba mchakato huo utajuimuisha taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya afya, jeshi la polisi, Mahakama na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka.