Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanayowasubiri mawaziri wanne wa Samia

Muktasari:

  • Mawaziri wapya Tanzania wanakabiliwa na changamoto kubwa katika wizara zao: Migogoro ya ardhi, mikopo na ajira kwa vijana, na masilahi ya vyombo vya habari ni miongoni mwa majukumu muhimu yanayowasubiri.

Dar es Salaam. Uteuzi ni jambo moja, lakini kuitumikia nafasi uliyoteuliwa ni jambo lingine.

Hiki ndicho kinachowasubiri mawaziri wanne wapya katika wizara mbalimbali walioteuliwa Julai 21, mwaka huu na kilichobaki ni kuapishwa na kuanza kuchapa kazi.

Ingawa uteuzi aghalabu ni faraja kwa mteuliwa, wadau wa sekta zitakazoongozwa na mawaziri hao wapya wameeleza kuwepo shughuli pevu zinazowasubiri wateule hao.

Wateule hao wapya ni Deogratius Ndejembi aliyetoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akimrithi Jerry Silaa.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo naye ni miongoni mwa wateule hao, aliyepewa uwaziri katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akimrithi Januari Makamba aliyetenguliwa. Kadhalika, Silaa aliyeondolewa Ardhi na sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, akimrithi Nape Nnauye ambaye pia uteuzi wake umetenguliwa.

Mwingine ni Ridhiwani Kikwete aliyetoka kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora anayeenda kuwa Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), akimrithi Ndejembi.


Migogoro ya Ardhi

Migogoro ya ardhi na ukiukwaji wa sheria ya ardhi ni machache kati ya mengi yaliyotajwa na wadau wa sekta ya ardhi kama kibarua kinachomsubiri Ndejembi katika wadhifa wake mpya.

Ndejembi katika wadhifa wake mpya anakabiliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi, ambayo imeonekana kuwasumbua mawaziri wengi waliopita katika wizara hiyo kama anavyofafanua, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Haki Ardhi, Cathbert Tomitho.

Kutokana na wingi wa migogoro hiyo, Tomitho amesema Silaa alijikuta anatumia muda mwingi kuisuluhisha, huku akiacha maeneo mengine yanayoihusu sekta hiyo, ikiwemo umilikishwaji.

 “Si kwamba alikosa kipaumbele isipokuwa sekta ya ardhi ndivyo ilivyo,” anaeleza.

Ukiachana na kibarua hicho, kwa mujibu wa Tomitho, Ndejembi pia ajiandae kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 ambayo kwa sehemu kubwa imekuwa ikikiukwa na ndiyo chanzo cha migogoro.

“Alipokuwa Silaa, alitembelea Bunju na maeneo mengine, malalamiko mengi ni viwanja kumilikishwa zaidi ya mara moja, tujiulize kwa nini manispaa na wizara yenyewe inamilikisha ardhi kwa zaidi ya mara moja, maana yake sheria haifuatwi,” anasema.

Uwajibishaji wa watendaji wa ngazi mbalimbali ndani ya wizara ni jambo lingine lililotajwa na Tomitho kama jukumu zito linalomkabili Ndejembi katika uwaziri wake wa ardhi.

“Kuna hati miliki feki za ardhi zinatoka na kuna watu ambao ni maofisa kwenye wizara wanahusishwa, nadhani waziri anapaswa kuangalia kwanza watendaji wake,” alieleza Tomitho.

Ndejembi huyohuyo, kwa mujibu wa Dk. Emmanuel Mchome, mwanazuoni wa Chuo Kikuu Ardhi, ajiandae kufanya utambuzi wa umiliki wa ardhi unaopaswa kufanyika wakati wa upimaji na ramani itakayopatikana ibandikwe kwenye ofisi ya kijiji au kitongoji kwa miezi mitatu.

Kwa mujibu wa Dk Mchome, ramani hiyo inapaswa kuwa na majina ya wamiliki wa kila ardhi na ukubwa wa eneo wanalolimiliki.

“Kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu, kila mmoja atakwenda kuangalia jina lake na ardhi yake, kama atatokea mwenye pingamizi atasema na utawekwa utaratibu wa kusikiliza na kutatua,” amesema.

Ameeleza hiyo itasaidia kujua wamiliki halali wa maeneo na hivyo kuepusha utapeli na uuzaji holela wa ardhi.


Changamoto za vijana

Wakati Ndejembi akitarajia kibarua hicho, Ridhiwani naye anatakiwa kuwa tayari kuweka sawa suala la mikopo na mitaji kwa vijana, bila kutekeleza mpango wa uundaji wa baraza la vijana nchini.

Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Youth Coalition (TYC), Lenin Kazoba amesema mitaji na mikopo kwa vijana ni moja ya majukumu ambayo hatima yake inamsubiri Ridhiwani katika nafasi yake mpya.

Kwa kuwa upatikanaji wa ajira ni changamoto nchini, Kazoba amesema wizara hiyo inapaswa kuweka mwongozo na mazingira mazuri ya kuwawezesha vijana kupitia mikopo.

Ingawa tayari Serikali imeshazindua mwongozo wa utoaji wa mikopo hiyo kwa makundi manne likiwemo la vijana, Kazoba alisisitiza umuhimu wa usimamizi kuhakikisha kundi hilo linanufaika.

“Kulikuwa na mikopo iliyokuwa inatolewa kupitia halmashauri, haikuwa na mwongozo, hatimaye haikuwanufaisha vijana, lakini Ridhiwani anapokwenda pale ahakikishe anaweka mazingira mazuri,” alieleza.

Ukamilishaji wa upatikanaji wa sera ya vijana ni jukumu lingine linalomsubiri waziri huyo katika wadhifa wake mpya.

Kwa mujibu wa Kazoba, hadi sasa sera hiyo haijaonekana katika ajenda za Serikali pamoja na umuhimu wake, hivyo matumaini ya vijana ni kuona Ridhiwani anakwenda kufanikisha hilo.

 Uanzishwaji wa baraza la vijana ni jambo lingine linalomsubiri waziri huyo, aliongeza.

“Kwenye hili changamoto imekuwa katika sheria ambayo hata vijana wenyewe hawaijui, kwa maana sheria ya baraza ya mwaka 2015,” alisema.

Kinachosababisha vijana wasiijue, amesema ni mazingira ya kupitishwa kwake ambayo hayakuwahusisha.


Silaa na Uchumi katika Vyombo vya Habari

Licha ya Jerry Silaa kuonekana rafiki wa vyombo vya habari katika nafasi zote za uongozi alizowahi kushika, anakabiliwa na kibarua cha kubadili urafiki huo na kuwa kichocheo cha uimara wa uchumi wa sekta kwa ujumla, kama inavyoelezwa na Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena.

 Urafiki wa Silaa na vyombo vya habari ulithibitika kwa kile kilichoelezwa na Meena kuwa, katika majukumu mengi tangu mwanasiasa huyo alipokuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, amekuwa akishirikiana na wanataaluma hiyo.

Mwanahabari huyo mwandamizi amesema anachopaswa kukifanya Silaa kwa sasa ni kuubadili urafiki aliokuwa nao kwa vyombo vya habari na aufanye kwa namna ya kupambania masilahi yao na hatimaye kuimarisha uchumi wa sekta husika.

“Vema kwa sasa urafiki wake (Silaa) uingie kwenye kubadilisha uchumi katika vyombo vya habari,” amesema.

Hata hivyo, mwanahabari huyo amesema hata waziri aliyeondolewa (Nape) amefanya mengi kwa masilahi ya taaluma ya habari, kadhalika yapo ambayo hakuyafanya pia.

“Uhalisia Nape alikuwa waziri wa habari alifanya kazi yake aliyotakiwa kuifanya na tunashukuru kwa kile alichokifanya, lakini kuna mambo mengi pia yalimshinda,” amesema.

 Kuhusu yaliyomshinda, amesema ni baadhi ya mambo aliyokuwa akijadiliana na kukubaliana na wadau wa sekta ya habari, ambayo utekelezwaji wake haukufanyika.

Lakini Nape huyohuyo, Meena amesema kuna wakati alifanya mambo yaliyowafurahisha wanataaluma ya habari, ikiwemo kusimamia mabadiliko ya sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016, ingawa hayajakamilika kama walivyotaka.

Kwa ujumla, amesema yapo maeneo ambayo Nape alifanya vema, lakini yapo ambayo wakati mwingine hayakuwafurahisha wanahabari.


Kombo na Hadhi Maalumu

Kwa upande wa Mahmoud Thabit Kombo aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anakabiliwa na kuhakikisha anakamilisha kile kilichoachwa na mtangulizi wake, Makamba.

Kwa mujibu wa Balozi wa zamani wa mataifa mbalimbali ikiwemo Italia na Ujerumani, Ali Karume alisema sera ya mambo ya nje na diplomasia ya uchumi ndiyo mwelekeo wa Serikali kwa sasa.

Kwa sababu hiyo, alieleza Balozi Kombo anapasa kuendeleza pale ambapo mtangulizi wake ameishia, huku asiache kufanikisha suala la utoaji wa hadhi maalumu kwa Watanzania waishia nje ya nchi.

Sambamba na yote, Balozi Karume amemtaka Kombo kuhakikisha anakuwa mwadilifu kwa kuwa nafasi aliyopewa ni tafsiri halisi ya kuwa msemaji wa mkuu wa nchi kimataifa.

“Lakini kwa kuwa Kombo alishakuwa balozi ameshajua mambo ya nje yanategemea mabalozi, hili jukumu halitamshinda,” amesema.

Ubora zaidi wa Kombo kwa mujibu wa Balozi Karume, ni kutoonyesha kwake malengo ya kisiasa zaidi ya nafasi aliyopewa, hivyo anaamini atatumikia vema.