Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Nape, Makamba kuenguliwa uwaziri

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (kulia) na aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati wa mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Juni 6, 2024. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Jana Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, huku akiwaweka kando mawaziri hao waandamizi.

Dar es Salaam. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wameeleza sababu ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaengua January Makamba na Nape Nnauye katika wadhifa wa uwaziri, kuwa ni pamoja na kushindwa kufikia matarajio yake.

January kabla ya mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia juzi katika baraza la mawaziri alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku Nape akiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Akizungumzia mabadiliko yaliyofanywa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Deus Kibamba ambaye ni mhadhiri katika Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahemd Salim (zamani Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam), amesema wizara hiyo ni ngumu ndiyo maana imepitia mabadiliko ya mawaziri wanne ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia.

Rais Samia alipoingia madarakani Machi 2021 alimkuta Profesa Palamagamba Kabudi akiwa waziri hapo.

Alitengua uteuzi wake na nafasi kushikwa na Balozi Liberata Mulamula, ambaye pia alitenguliwa na kuteuliwa Dk Stergomena Tax, ambaye sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Septemba Mosi, 2023 Rais Samia alimteua January kuongoza wizara hiyo akitokea Wizara ya Nishati.

Kibamba amesema wizara hiyo ni ngumu siyo kwa Tanzania pekee, bali hata nchi nyingine na huenda kikawa chanzo cha kufanyika mabadiliko ya mara kwa mara.

“Eneo moja ambalo limekuwa shida kwa mawaziri wa mambo ya nje kwa nchi zetu za Afrika, ni kutafuta safari za nje,” amesema Kibamba.

“Ningekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ningesafiri safari moja nje ya nchi kwa mwaka mzima, kwa sababu kuna mengi ya kufanyika kupitia teknolojia, ningekuwa waziri wa Zoom, ningekuwa wa video conferencing (mikutano kwa njia ya video). Ningekuwa naita maofisa wangu kwenye ukumbi wa mikutano wizarani kwangu waangalie mkutano kule kwenye video, wakati balozi wetu wanahudhuria kule,” amesema.

Kibamba amesema waziri katika wizara hiyo ndio kila kitu kinachohusu uhusiano wa kimataifa.

“Safari iwe ni safari ya Wizara ya Kilimo au nyingine, ujue inatengenezwa na Wizara ya Mambo ya Nje. Ndiyo maana Magufuli (Dk John, Rais wa awamu ya tano) aligombana na baadhi ya mawaziri wa wizara hiyo,” amesema.

“Ni kweli Rais ana mkono wa kusema hapana, kufanya tathmini za faida na hasara, lakini anapomteua waziri anakuwa ameshamwamini,” amesema.

Mhadhiri huyo anasema matarajio ya wananchi ni kuona faida ya ziara za viongozi wa Serikali zinazoratibiwa na wizara hiyo.

“Wasingetaka wizara iwe ya kukimbilia mataifa mengine kukopa tu, wangetaka itafute suluhu ya maparachini yaliyopo Kilolo yatapataje soko huko duniani? Korosho inayolimwa nchini inawanufaishaje huko nje,” amesema.

Hata hivyo, Kibamba amesema kuondoka kwa January kunaweza kusiwe suluhisho, bali Rais Samia anapaswa kukuna kichwa kupata mtu sahihi atakayekwenda na kasi yake.

“Suala siyo kukopa tu, maana hivi karibuni, tunasikia nchi imekopa. Nadhani hata Rais anasikiliza na kujiuliza, hivi ni kukopa tu, hakuna mikakati mingine? Hakuna uwekezaji unaoweza kuja kutoka nje ya nchi?” amesema.

“Katika dunia ya sasa unahitaji waziri anayejifikirisha na anatakiwa kutuliza miguu nyumbani, mara chache tu asafiri, kwa sababu kuna timu kubwa ya wataalamu iliyopo kwenye balozi,” amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema mabadiliko katika wizara hiyo ni ya kawaida.

“Nadhan bado Rais hajapata mtu sahihi kwa wizara hii. Utakumbuka amekuwa akifanya mabadiliko kwenye wizara hii zaidi ya mara nne sasa. Yawezekana walioteuliwa kwa nafasi hii bado hawajatafsiri ndoto za Rais,” amesema.


Wizara ya Habari

Kuhusu Nape baadhi ya wachambuzi wanahusisha kutenguliwa kwake na kauli aliyoitoa Julai 15, 2024 akiwa mkoani Kagera.

Nape alikaririwa akisema: “Matokeo ya kura siyo lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi mkishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe.”

Kauli hiyo ilizua mjadala mitandaoni, huku Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla akisema si msimamo wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Dk Kabobe, kauli hiyo lilikuwa kosa kubwa kwa Nape.

“Yalikuwa makosa makubwa kwa kiongozi mwandamizi kama Nape kutoa kauli kama hizo zenye kukichafua chama (CCM) na Serikali juu ya uchaguzi,” amesema.

“Kauli yake inaweza kuwa imechukuliwa kama uthibitisho kwa wapinzani ambao mara zote wamekuwa wakilalamika kuibiwa kura,” ameeleza.

“Ukizingatia kuwa Rais anatekeleza vizuri falsafa yake ya 4R, vitendo kama hivi vya kumrudisha nyuma lazima avikemee na kulinda chama na Serikali yake kwa wivu mkubwa. Nadhani hiki ndicho alichofanya,” amesema.

Kuhusu uteuzi wa Jerry Silaa, kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, mwanahabari mkongwe, Absalom Kibanda amesema anaingia katika wizara hiyo akikuta mtangulizi wake Nape amefanya kazi kubwa inayoonekana kwenye taarifa ya hali ya vyombo vya habari aliyokabidhi kwa Rais Samia hivi karibuni.


Uteuzi  wa watu walewale

Kwa mtazamo wa mwanazuoni wa sayansi ya siasa, Profesa Ernest Mallya yapo yaliyojificha nyuma ya uamuzi wa mamlaka ya uteuzi kumtengua mteule wake.

Ingawa wapo wanaodhani kutenguliwa ni adhabu, Profesa Mallya amesema wakati mwingine kiongozi anahitaji kupanga safu anayoihitaji.

Kwa sababu kutenguliwa si adhabu, mwanazuoni huyo aliyewahi kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema si ajabu kuona aliyetenguliwa akiteuliwa wakati mwingine kwa nafasi ileile au nyingine.

“Hapo inategemea na wewe umetafsiri vipi uamuzi wa mtu kutenguliwa. Wakati mwingine mtu anaondolewa kwenye nafasi yake si eti adhabu kama wengi wanavyodhani,” amesema.

Kuhusu hilo, Kibanda amesema mabadiliko hayo yanaonyesha Rais Samia anachojali ni utekelezaji wa majukumu aliyowapa watendaji wake, siyo vinginevyo.

“Rais anatuelezea kupitia wasaidizi wake wa Ikulu, washauri wake wa siasa, watendaji wa Serikali za mitaa, mawaziri, naibu waziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, ma-RAS, ma-DAS, kwamba akiona ndivyo sivyo, hata awe amefanya mabadiliko mara ngapi, haimpi shida, kwa hiyo anasimamia maneno yake,” amesema Kibanda.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema yapo mambo matatu yanayosababisha mamlaka ya uteuzi kuishia kuwateua watu walewale kila wakati.

Dk Masabo anasema ni uwepo wa changamoto ya maandalizi ya viongozi inayoikabili Tanzania kwa sasa.

Changamoto hiyo amesema inasababisha kuwapo kasumba kwamba kuna watu fulani ndio wanaoweza kuongoza.