Yaliyomo yamo ripoti ajali ya ndege

Muktasari:

  • Msemo wa Waswahili kuwa “Yaliyomo yamo” unafaa kueleza maudhui yaliyomo katika ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyowasilishwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ukilinganisha na ile iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii siku mbili zilizopita.

Dar es Salaam. Msemo wa Waswahili kuwa “Yaliyomo yamo” unafaa kueleza maudhui yaliyomo katika ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyowasilishwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ukilinganisha na ile iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii siku mbili zilizopita.

Baada ya kusambaa kwa ripoti hiyo juzi na kuripotiwa na vyombo vya habari vya ndani na vya nje, likiwemo gazeti hili, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliutaka umma uipuuze akisema, “Angalizo. Serikali bado haijatoa taarifa ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya kampuni ya Precision Air. Taarifa inayosambaa mitandaoni ipuuzwe kwa kuwa haijatoka katika mamlaka rasmi za Serikali.”

Juzi, Mwananchi iliandika kile kilichoandikwa katika ripoti hiyo iliyosambaa mitandaoni yenye kurasa saba ambayo maudhui yake hayana tofauti na maudhui yaliyoelezwa na waziri jana.

Jana, Msigwa akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari akitoa onyo akisema, “mimi nikiwa msajili wa magazeti pia nimesikitishwa sana kuona vyombo vya habari vya magazeti vinachapisha taarifa kuhusu ajali ya ndege kutoka kwenye vyanzo visivyokuwa sahihi, ni kitu ambacho si cha kiweledi.”

Wakati suala hilo likiwa bado linagonga mijadala, waziri mwenye dhamana ya usafiri wa anga, jana saa moja jioni jana alijitokeza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kutoa ripoti yaawali ya Serikali juu ya uchunguzi wa ajali hiyo.

Huku akisisitiza kanuni namba 18 (1) ya uchunguzi wa ajali za ndege, Waziri alisema inamtaka waziri kutoa taarifa baada ya miezi 12 na kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa taarifa mara kwa mara na si mwingine.

Alisema taarifa hiyo ni ya awali inayopaswa kutolewa ndani ya siku 14 baada ya tukio la ajali kutokea na kwamba nyingine zitaendelea kutolewa baada ya siku 30 na nyingine baada ya miezi 12.

Waziri huyo alisema, timu tatu za uchunguzi za wizara hiyo, Precision Air pamoja na wataalamu wa kampuni ya ATR watengenezaji wa ndege hiyo wote wapo nchini Ufaransa wakiendelea na uchunguzi.

Miongoni mwa mambo ambayo Waziri Mbarawa alieleza kuhusu ajali hiyo iliyotokea Novemba 6 mwaka huu katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 kunusurika, ni kuhusu nani aliyefungua mlango wa ndege.

Kama ambavyo gazeti hili liliripoti kutoka kwenye ripoti ya juzi kuwa aliyefungua mlango ni mhudumu wa ndege akisaidiwa na abiria, ndivyo ambavyo Waziri Mbarawa alieleza.

Katika ufafanuzi wake, Waziri Mbarawa alisema wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi walifika eneo la tukio dakika tano baada ya ndege hiyo iliyokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam ikiwa na watu 43 kuanguka.

“Wananchi hawa waliendelea na jitihada za kufungua mlango kwa nje hali iliyompa ujasiri mhudumu wa ndege na abiria kuufungua baada ya kuona nje ya ndege kuna msaada,” alisema Profesa Mbarawa.

Vilevile, sawa na ambavyo ripoti hiyo iliyosambaa imeeleza, askari wa wanamaji licha ya kupewa taarifa mapema dakika 15 tangu ajali kutokea na walishindwa kufika kwa wakati, waziri naye aligusia suala hilo.

Katika maelezo yake, Waziri Mbarawa alikiri kweli taarifa (ya ajali) ilitolewa lakini boti ya uokozi ilikuwa mbali takribani kilomita 100 hadi 200 kutoka eneo la ajali, hivyo isingekuwa rahisi kufika kwa wakati.

“Tunayo boti ya uokozi katika Ziwa Victoria ambayo inatumiwa katika eneo kubwa la ziwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.

“Wakati ajali inatokea boti ilikuwa katika doria eneo la mbali na ulipo Uwanja wa Ndege wa Bukoba, zinaenda maili 30 kwa saa kama iko kilomita 100 hadi 200 itachukua hata saa tano ,ndiyo maana ikachelewa,” alisema Waziri Mbarawa

Katika ripoti hiyo iliyosambaa mtandaoni inaeleza askari hao wa wanamaji walikwama kuzamia na kufika eneo hilo, kwa kilichobainishwa kuwa mitungi ya oksijeni waliyokuwa nayo haikuwa na gesi hiyo, suala ambalo waziri hakuligusia.

Kama ambavyo ripoti hiyo inaeleza, hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba, iliyosababisha mvua, wingu zito na radi ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kutokea siku ya tukio, saa na dakika zinashabihiana na alizozitaja Waziri Mbarawa.

“Hali ya hewa ilikuwa nzuri hadi saa 2:20 asubuhi, ilibadilika ghafla mvua ikaanza kunyesha na radi, mawingu mazito na upepo mkali,” imeeleza ripoti hiyo sawia na alichokisema Waziri Mbarawa.

Akifafanua zaidi kuhusu ushiriki wa wavuvi katika uokozi, Profesa Mbarawa alisema katika ajali zinazotokea majini ipo miongozo na taratibu za kimataifa kuhusu uendeshaji wa mchakato huo na inayongozwa na mkataba wa kimataifa wa namna ya utafutaji na uokoaji majini wa mwaka 1974 ambao Tanzania imeridhia.

“Mkataba huu umetoa mwongozo kwamba pale inapotokea ajali katika maji, ziwa au bahari, inamtaka mtu au kikundi cha watu waliopo karibu na eneo la ajali kuwajibika na uokozi na kutoa taarifa kwa vyombo husika.

“Watu hawa wanawajibika kuendelea na uokozi hata pale inapotokea vyombo vya uokoaji vinapofika katika eneo la ajali, huu ndio mwongozo sahihi unaotolewa na unaendana na utamaduni wetu kwamba inapotokea ajali watu walio karibu husaidia kuwakoa manusura.” alisema.

Mbali na hayo, mapendekezo ya ripoti hiyo iliyonukuliwa na gazeti jana, yanashabihiana na yaliyotolewa Novemba 14 mwaka huu na Baraza la Mawaziri, lililokutana kwa dharura kujadili ajali hiyo.

Ilipendekeza kutengeneza utaratibu mzuri wa utafutaji na uokoaji katika matukio na uwepo muundo imara ulioratibiwa katika huduma za uokoaji na utafutaji katika usafiri wa majini na anga, masuala ambayo vilevile yamependekezwa na wadau mbalimbali wa masuala ya anga na yakagusiwa hata na waziri mwenyewe.

Alipoulizwa na waandishi wa habari ukimya wa Serikali kwa zaidi ya siku nzima tangu ripoti hiyo kusambaa mitandoni na yeye akiwa waziri mwenye dhamana ya usafiri wa anga kwanini asiwajibike, akajibu, “anayetakiwa kutoa ripoti yoyote ile ni waziri kwa mujibu wa sheria, mimi ndiye waziri ninayesimamia usafiri wa anga, wewe unaweza kutoa ripoti unavyotaka, hizo ripoti kama iko si sahihi. Kama Zitto ametoa taarifa ya ripoti yeye si waziri, ninayetakiwa kutoa ni mimi.”

(Nyongeza na Baraka Loshilaa na Bakari Kiango)