Aliyembaka bibi, jela miaka 30

Muktasari:
- Katika kesi ya msingi, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa tukio la ubakaji lilitokea Agosti 7, 2024, katika Kijiji cha Kinkina, Wilaya ya Chemba, Mkoa wa Dodoma. Inadaiwa kuwa mshtakiwa, Iddi Zuberi, alimbaka mwanamke mmoja aliyekuwa shambani kwake akivuna mbaazi.
Arusha. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dodoma, imeridhia hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela aliyopewa Iddi Zuberi, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 67.
Tukio hilo lilitokea Agosti 7, 2024, katika Kijiji cha Kinkima, Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma, ambapo mrufani alimbaka mwanamke huyo alipomkuta shambani kwake akivuna mbaazi.
Jaji Evaristo Longopa, aliyesikiliza Rufaa ya Jinai Na. 32818/2024, alitoa hukumu hiyo Mei 6, 2025, baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia mwenendo wa kesi ya msingi.
Baada ya kupitia hoja za pande zote, Jaji Longopa alisema kuwa upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.
Hivyo, Mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa mashiko na ikathibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya Iddi Zuberi.
Ilivyokuwa
Baada ya usikilizwaji wa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Chemba, mnamo Oktoba 3, 2024, Iddi Zuberi alikutwa na hatia ya kosa la ubakaji na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Akitoa ushahidi wake mahakamani, shahidi wa kwanza ambaye pia ni mwathirika wa tukio hilo, alieleza kuwa siku ya tukio, akiwa shambani kwake saa nne asubuhi akivuna mbaazi, Iddi alijitokeza ghafla, akamshika kwa nguvu, akamvua nguo na kisha kumbaka.
Nakala ya hukumu inaeleza kuwa, kutokana na matumizi ya nguvu katika utekelezaji wa kitendo hicho, shahidi huyo alipata majeraha na alitokwa na damu kufuatia tukio hilo.
Baada ya kusikiliza pande zote, Jaji alieleza kuwa mahakama imepitia kwa makini mwenendo wa kesi, hukumu, na sheria zilizotumika ili kubaini iwapo sababu zilizotolewa katika rufaa hiyo zina uhalali au la.
Jaji huyo alisema ni ukweli usiopingika kwamba tukio la unyanyasaji mkubwa wa kijinsia lilitokea wakati wa mchana, ambapo mwanga wa kutosha ulikuwepo, hivyo mashahidi walikuwa na muda wa kutosha kumtambua mrufani eneo la tukio.
“Ni maoni ya Mahakama hii kwamba, kwa kuzingatia uthabiti wa ushahidi wa upande wa Mashtaka katika kumbukumbu, hakuna shaka kwamba mrufani ndiye aliyetenda kosa hilo na alikuwa ametambuliwa ipasavyo na mwathirika wa ubakaji,” alisisitiza Jaji.
Kuhusu uthibitisho wa kosa hilo, Jaji alisema kuwa ni kanuni ya msingi ya sheria kwamba ushahidi bora zaidi katika makosa ya ngono unatolewa na mwathirika mwenyewe. Hivyo, kwa kuzingatia mazingira ya kesi hiyo, mwathirika alithibitisha kuwa Iddi ndiye alimbaka.
Baada ya kupitia hoja zote, Jaji alihitimisha kuwa ni wazi kwamba katika mazingira ya kesi hiyo, hakuna shaka yoyote kwamba upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha kesi dhidi ya mrufani pasipo kuacha shaka yoyote, na hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.