Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi alivyojinasua katika kifungo cha miaka 30, kuachiwa huru

Muktasari:

  • Mahakama Kuu masjala ndogo ya Dar es Salaam, imemwachia huru mkazi wa eneo la Msata huko Bagamoyo, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka bibi kizeee mwenye umri wa miaka 70.

Dar es Salaam. Amejinasua, ndilo neno unaweza kulitumia kuelezea namna mkazi wa Msata Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Hamis Luvumbagu alivyoepuka kifungo cha miaka 30 jela kwa tuhuma za ubakaji.

Uamuzi wa kumwachia huru umetolewa na Jaji Awamu Mbagwa wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, katika hukumu aliyoitoa Februari 10, 2025 na nakala kuwekwa mtandao wa Mahakama leo Jumatano, Februari 12, 2025.

Hii ni baada ya kukubaliana na sababu za rufaa zilizowasilishwa na mrufani huyo, akipinga kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa huku Jaji akiridhika Jamhuri haikuwa imethibitisha shitaka hilo.

Luvumbagu alihukumiwa kifungo hicho baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumwingilia kimapenzi mwanamke mwenye umri wa miaka 70 bila ridhaa yake, tukio lililotokea Aprili 30, 2023 eneo la Msata.

Siku hiyo usiku wa manane, ilidaiwa Luvumbagu aliingia ndani ya nyumba ya bibi kizee huyo, akamtoa hadi nje ya nyumba yake na kumbeba hadi shambani na kumlazimisha kufanya ngono.

Ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu za Mahakama,  bibi huyo hakumtambua mtu aliyembaka, ila alipiga kelele za kuomba msaada kisha mwenyekiti wa kijiji alimwamuru mgambo kwenda eneo hilo.

Shahidi wa pili, Hamis Farhan ambaye ni mgambo aliyetumwa na mwenyekiti, aliieleza Mahakama alifika eneo la tukio na kumkuta mrufani akimbaka bibi huyo na alipomuona, alimwachia na kukimbia.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, Farhan alimfuatilia mrufani na kufanikiwa kumkamata akiwa katika duka la shahidi wa nne, Winfrida Clemence, ambaye baada ya kuelezewa tukio la Farhan.


Alivyofungwa miaka 30

Katika utetezi wake mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, mrufani alikanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa, inatokana na chuki alizokuwa nazo na shahidi wa pili wa Jamhuri, Hamis Farhan.

Alidai kuwa, shahidi huyo ndiye aliyekuwa nyuma ya mchezo wa yeye kubambikiwa kosa hilo kwa kuwa Aprili 29, 2023, shahidi huyo alikuwa amekwenda eneo lake la biashara na kununua chipsi.

Mgambo huyo alimpa Sh10, 000 na yeye akawa hana chenji na akamtaka awe mvumilivu ili atafute chenji lakini hata hivyo, mteja wake huyo hakukubaliana na kauli hiyo na ndipo walipoanza kupigana.

Hivyo, akaiambia Mahakama kuwa amehusishwa na tuhuma hizo kutokana na ugomvi binafsi na mgambo huyo, lakini hata hivyo Mahakama ilitupilia mbali utetezi wake na kumfunga miaka 30 jela.

Hakuridhishwa na hukumu hiyo na akaamua kukata rufaa akiegemea sababu kuu nne, moja ikiwa ni hakimu kukosea kumfunga kwa kuegemea ushahidi wa utambuzi ambao haukuwa sahihi.

Pia, alijenga hoja kuwa hakimu aliyemfunga alikosea kisheria kwa kumfunga kwa kuegemea ushahidi wa uongo na uliojikanganya na pia upande wa Jamhuri haukuwa umethibitisha shitaka na kuacha shaka.


Uamuzi wa Jaji

Katika hukumu yake, Jaji Mbagwa alisema baada ya kupitia ushahidi, malalamiko ya mrufani na mawasilisho ya mrufani na Jamhuri, ni jambo la ambalo halina  ubishi bibi huyo aliingiliwa kingono bila ridhaa yake.

“Lakini swali muhimu la kujiuliza ni je ni mrufani ndiye aliyefanya kitendo kile? Mwathirika mwenyewe aliyekuwa shahidi wa tatu alisema hakumtambua na wala hakuweza kuelezea mwonekano wake.”

Jaji akasema, “kwa hiyo ushahidi pekee unaomhusisha na tukio hilo ulitoka kwa shahidi wa pili na wa nne. Shahidi wa pili anasema aliitwa na mwenyekiti na kuagizwa kwenda eneo la tukio.”

“Kwamba alienda pale na kumkuta mrufani anambaka bibi huyo na kwamba alipomuona yeye akakimbia. Alisema alimtambua lakini hakujali kuieleza Mahakama nini kilichomfanya aweze kumtambua.”

“Ni jambo linalofikirisha ni muda gani tukio la kubaka lilichukua kiasi kwamba shahidi wa pili aliitwa na mwenyekiti, akatoka alikokuwa na kwenda eneo la tukio na kukuta mrufani bado anambaka bibi.”

“Ushahidi pia uko kimya kuhusu namna mwenyekiti huyo anayedaiwa kumpa taarifa shahidi wa pili wa Jamhuri alivyopata taarifa za tukio hilo la ubakaji,”alisema Jaji katika uchambuzi wake.

“Ushahidi wote wa mashahidi wa upande wa mashitaka ulikuwa na simulizi kuwa, uhalifu huo ulitendeka usiku lakini ukisoma hati ya mashitaka inaeleza kuwa, tukio hilo la ubakaji lilitokea mchana kweupe.”

Jaji alisema dosari hizo zinafanya ushahidi wa shahidi wa pili na wa nne uwe ni wa kutiliwa shaka na baada ya kupima ushahidi huo, anakubaliana na mrufani kuwa Jamhuri haikuthibitisha shitaka hilo.

Ni kutokana na hitimisho hilo, Jaji akaamuru kubatilishwa kutiwa kwake hatiani na kufuta adhabu ya miaka 30 aliyohukumiwa na kuamuru aachiliwe mara moja kutoka mahabusu, isipokuwa tu kama anashikiliwa kwa makosa mengine.