Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyefungwa kwa wizi wa waya waTanesco, aachiwa huru

Muktasari:

  • Awali Mahakama ya Wilaya ya Mbeya ilimhukumu kifungo cha miaka 20 jela, Joseph Ngonyani baada ya kumkuta na hatia katika makosa matatu, ikiwemo wizi wa waya wa shaba mita 70 wenye thamani ya Sh1.54 milioni kutoka kwenye transfoma ya umeme, mali ya Tanesco.

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya imemuachia huru, Joseph Ngonyani, aliyetiwa hatiani kwa makosa matatu, ikiwemo wizi wa waya wa shaba mita 70 wenye thamani ya Sh1.54 milioni kutoka kwenye transfoma ya umeme, mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Joseph alikutwa na hatia na Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, ambapo alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela.

Baada ya kutokuridhika na adhabu hiyo, alikata Rufaa ambayo rufaa hiyo ya jinai namba 35482 ya mwaka 2024 ilisikilizwa na kutolewa uamuzi huo na Jaji Aisha Sinda, Januari 16, 2025. Nakala ya uamuzi huo imewekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Awali, alidaiwa kutenda kosa hilo Septemba 5, 2023, katika Hospitali ya K'S iliyopo wilayani na Mkoa wa Mbeya.

Jaji huyo alifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili, na kubaini dosari wakati wa usikilizwaji, ikiwemo ushahidi wa utambuzi wa mrufani katika eneo la tukio kuwa dhaifu.


Ilivyokuwa

Joseph alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa makosa matatu, ambapo kosa la kwanza ni wizi kinyume na kifungu cha 258(1) na 265 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Kosa la pili la kuingilia huduma muhimu kinyume na kifungu cha 57(1) na 60(2), kusomwa pamoja na aya ya 20(1), (2)(a) ya Jedwali la Kwanza la Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa (EOCCA).

Kosa la tatu ni kusababisha hasara kwa mamlaka maalumu kinyume na kifungu cha 57(1) na 60(2), vikisomwa pamoja na aya ya 10(1) na (4) ya EOCCA.

Awali, Mahakama ya Wilaya ya Mbeya ilimhukumu kutumikia kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la kwanza, miaka 20 jela kwa kosa la pili, na miaka 20 jela kwa kosa la tatu, adhabu ambazo zinatekelezwa kwa pamoja.

Katika kosa la kwanza, ilidaiwa Septemba 5, 2023, katika Hospitali ya K'S iliyopo wilayani na Mkoa wa Mbeya, aliiba waya wa shaba mita 70 wenye thamani ya Sh1.54 milioni kutoka kwenye transfoma ya umeme, mali ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Kosa la pili alidaiwa Septemba 5, 2023, katika hospitali hiyo ya K'S, bila kibali, aliingilia huduma hiyo muhimu kwa kukata waya wa shaba kutoka kwa transfoma ya Umeme, mali ya Tanesco.

Kosa la tatu alidaiwa siku hiyo katika hospitali ya K'S, bila kibali, alikata waya wa shaba kutoka kwa transfoma ya umeme ambayo hutumika kwa ajili ya kutoa huduma muhimu ya umeme, na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh1.54 milioni.


Rufaa

Katika rufaa hiyo, Joseph alikuwa na sababu nane, ikiwemo kwamba Mahakama ilikosea kisheria kumtia hatiani na kumhukumu bila kuona kuwa mashtaka dhidi yake hayakuthibitishwa bila mashaka yoyote. Mahakama ilikosea kumtia hatiani bila kuzingatia kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika kuchukua vielelezo cha kwanza hadi cha tatu.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Joseph hakuwa na wakili, huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Salmin Zuberi.

Wakili huyo alianza kwa kuunga mkono rufaa hiyo na kukubaliana na sababu ya kwanza ya kuwa shitaka dhidi ya Joseph halikuthibitishwa bila kuacha shaka kama inavyotakiwa na sheria.

Alisema amepitia ushahidi wa shahidi wa kwanza na pili na kueleza kuwa walishindwa kutoa ushahidi wa jinsi walivyomtambua mrufani usiku kama inavyotakiwa na kuwa ushahidi wa utambuzi haukuthibitishwa ipasavyo.

Alisema kutokana na Joseph kutokutambuliwa eneo la tukio, kosa hilo halijathibitishwa bila kuacha shaka, na kuamua kutokuwasilisha sababu zilizobaki za rufaa hiyo.

Kwa upande wake, Joseph aliomba mahakama iruhusu rufaa yake.


Uamuzi wa jaji

Jaji Sinda alisema amezingatia kumbukumbu ya kesi na hoja za pande zote mbili na kuchunguza iwapo kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Alisema amechambua na kutathmini ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na kukubaliana na Wakili wa Jamhuri kuwa ushahidi wa utambuzi wa mrufani eneo la tukio ulikuwa dhaifu.

Jaji huyo amesema katika ukurasa wa saba wa mwenendo wa kesi hiyo, shahidi wa kwanza alidai akiwa doria katika Hospitali ya K'Z saa 6:30 usiku, alimuona mtu akikata waya wa shaba kwenye transfoma ya umeme ya Tanesco, na kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.

Alisema shahidi wa pili alidai kupokea simu kutoka kwa shahidi wa kwanza akimwambia kuna mtu alikamatwa katika hospitali ya K'Z kwa kuiba waya wa shaba wa transfoma, na alikwenda eneo la tukio na kumhoji mtu huyo na kumpeleka kituo cha polisi.

“Miongoni mwa mambo mengine, ushahidi wa mashahidi hao haukutoa ufichuzi kamili iwapo walimfahamu au kuwaona washtakiwa awali, ukubwa wa mwanga wa eneo la tukio, rangi, au mavazi. Kwa kuangalia ushahidi wao, ni wazi kwamba miongozo ya ushahidi wa utambuzi ilikuwa dhaifu,” amesema.

Jaji alisema anaona upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote, kwani ushahidi wa mashtaka ulikuwa na mashaka mengi.

“Kwa hiyo, ninaruhusu rufaa, kufuta na kuweka kando hukumu, na kuamuru kuachiliwa mara moja kwa mrufani kutoka gerezani isipokuwa kama ameshikiliwa kwa sababu nyingine halali,” alisema Jaji.