Prime
Aliyehukumiwa kwa kumuua baba yake mzazi aachiwa huru
Muktasari:
- Jopo la majaji watatu wa Mahakama wa Rufani, wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi dhidi ya Seni Lisesi, aliyekuwa amehukumiwa adhabu hiyo, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua baba yake mzazi.
Arusha. Mahakama ya Rufani imetengua adhabu ya kifo aliyokuwa amehukumiwa Seni Lisesi, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua baba yake mzazi, Gindu Kashinje.
Awali Mei 14, 2021, Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga ilimhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kumkuta na hatia ya kumuua baba yake.
Mahakama ya rufani imebatilisha adhabu hiyo baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka, haukuthibitisha kesi dhidi ya Seni bila kuacha shaka yoyote na hukumu iliyotolewa dhidi yake ilitegemea ushahidi dhaifu na usioaminika.
Rufaa hiyo ya jinai namba 319 ya mwaka 2021, ilisikilizwa na Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Barke Sehel, Dk Paul Kihwelo na Gerson Mdemu, waliotoa hukumu hiyo Januari 30,2025 katika kikao chake kilichoketi Sumbawanga.
Katika kesi hiyo ya msingi upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi wanne na vielelezo vitatu ikiwemo maelezo ya onyo na ya ziada ya mshitakiwa.
Ilivyokuwa
Desemba 4, 2016, Seni alidaiwa kumuua Gindu, kwa mujibu wa kielelezo cha kwanza, ambacho ni ripoti rasmi.
Kielelezo kilisema chanzo cha kifo hicho kilitajwa kuwa ni kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha ya kukatwa.
Shahidi wa kwanza, Mwalo Lisesi ambaye ni mtoto wa marehemu na mkazi wa Kijiji cha Ilanga, aliieleza Mahakama kuwa siku ya tukio, watu walivamia nyumba ya baba yake wakiwa na tochi. Baba yake alianza kupiga kelele akiomba msaada kutoka kwa majirani.
Alidai kuwa yeye alifanikiwa kutoroka na kukimbilia mtoni karibu na nyumba yao, ambako alijificha hadi usiku wa manane.
Amesema aliporudi nyumbani, alimkuta mama yake akiwa amejeruhiwa na amepoteza fahamu, huku baba yake akiwa tayari amefariki dunia. Mama yake alipelekwa hospitalini na siku iliyofuata, Seni alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Shahidi wa pili, Maghembe Kwilasi ambaye kwa wakati huo alikuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwadui, alidai siku ya tukio alipokea taarifa kutoka kwa ndugu zake wakimweleza kwamba Gindu na mkewe wameshambuliwa na kujeruhiwa watu wasiojulikana.
Amesema alipofika eneo la tukio, alikuta watu wakimhoji mrufani, ambaye alidai wauaji wa baba yake walitokea Mpanda.
Aidha, alidai kuwa mrufani huyo alikiri kumuua baba yake na tukio hilo liliripotiwa polisi.
Shahidi wa tatu, askari Polisi, Thomas Kilakoi aliieleza mahakama kuwa alipofika eneo la tukio, alikuta mwili wa marehemu ukiwa nje ya nyumba yake.
Hata hivyo, uchunguzi ulionesha kuwa Gindu alivamiwa ndani ya nyumba yake, lakini alifariki dunia nje wakati akijaribu kutoroka.
Alibaini pia uwepo wa dimbwi la damu mahali ambapo mwili wake ulikuwa, na kwamba mrufani tayari alikuwa amekamatwa na sungusungu.
Alipoandika maelezo ya onyo ya mrufani huyo, alisema kuwa alikiri kumuua baba yake.
Shahidi wa nne, Hakimu Mkazi Rosta Emmanuel aliyerekodi maelezo ya ziada ya Seni, alithibitisha kuwa mrufani huyo alikiri kutekeleza mauaji hayo.
Baada ya kesi kusikilizwa upande wa mashtaka na utetezi, Jaji aliyesimamia shauri hilo aliwasilisha majumuisho ya kesi kwa wazee watatu wa baraza waliokaa naye.
Katika maoni yao, wazee wawili wa baraza walipendekeza hukumu ya kutokuwa na hatia kwa sababu hakuna shahidi aliyemwona mrufani akitekeleza mauaji hayo. Hata hivyo, mzee mmoja wa baraza alirudisha hukumu ya hatia.
Jaji, baada ya kutafakari maoni hayo na kukubaliana na mzee wa baraza aliyepingana na wenzake, alimkuta mrufani na hatia ya mauaji na akamhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Rufaa
Katika rufaa hiyo, mrufani aliwakilishwa na mawakili Neema Charles na Peter Kamnyalile. Awali, hati ya rufaa iliyowasilishwa mahakamani hapo Julai 15, 2021, ilijumuisha sababu saba za kupinga hukumu.
Hata hivyo, Oktoba 15, 2024, waliongeza sababu tano zaidi, ingawa wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo waliwasilisha sababu nne tu ikiwamo ya Mahakama kwamba ilifanya makosa kwa kutowaongoza wazee wa baraza ipasavyo kuhusu mambo muhimu ya kisheria.
Pia ilikosea kumtia hatiani na kumhukumu mrufani, kwa kutegemea maelezo ya onyo na ya ziada ambayo yalipokelewa kinyume cha sheria.
Hati hiyo pia imeandika Mahakama ilikosea kuzingatia ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu ambayo haikusomwa mahakamani baada ya kupokelewa na kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Wakili Neema Charles alidai kuwa Mahakama Kuu haikutoa mwongozo sahihi kwa wazee wa baraza kuhusu mambo ya kisheria muhimu katika kesi hiyo.
Aliongeza kuwa kwa kuwa mrufani alitiwa hatiani kwa msingi wa maelezo ya onyo yasiyo ya haki, kesi hiyo ilipaswa kufutwa.
Kwa upande wake, Wakili Peter Kamnyalile alieleza kuwa maelezo ya onyo na ya ziada yalikubaliwa mahakamani kinyume cha sheria. Alidai kuwa maelezo ya onyo yalichukuliwa chini ya kifungu cha 58(3)(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambacho kinahusu mtu anayejua kusoma na kuandika na anayetoa maelezo kwa maandishi mwenyewe. “Hii ni tofauti na kifungu cha 57 cha CPA kinachotakiwa kutumika kurekodi maelezo ya mtu yeyote, aweze kusoma au la,” alisema.
Kuhusu maelezo ya nje ya mahakama, wakili alidai kuwa yalirekodiwa kinyume na mwongozo wa Jaji Mkuu wa majaji wa haki za amani kuhusu kurekodi taarifa za ungamo.
Alidai kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote unaoonesha kuwa taarifa hiyo ilitolewa kwa hiari au ilisomwa kwa mrufani kabla ya kusainiwa.
Ili kuimarisha hoja yake, Wakili Kamnyalile alinukuu kesi mbalimbali, ikiwemo ya Rufaa ya Jinai Na. 142 ya mwaka 2020 ya Manoja Masalu na wenzake dhidi ya Jamhuri, akieleza kuwa maelezo ya onyo na ya ziada hayakupaswa kukubalika mahakamani na hivyo yalistahili kufutwa kutoka kwenye kumbukumbu.
Kuhusu ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, wakili alieleza kuwa ilipokelewa mahakamani lakini haikusomwa, jambo ambalo ni kinyume cha matakwa ya kisheria.
Kutokana na hilo, aliomba ripoti hiyo iondolewe kwenye kumbukumbu na kesi dhidi ya mrufani itupiliwe mbali, kwa kuwa haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote.
Uamuzi wa majaji
Jaji Kihwelo alieleza kuwa, kama Mahakama ya kwanza ya rufani, wanayo mamlaka kwa mujibu wa Kanuni ya 36(1)(a) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania, kutathmini upya ushahidi uliowasilishwa na kufikia uamuzi wao wenyewe.
Alibainisha kuwa wameona ni muhimu kushughulikia msingi wa tatu wa rufaa, ambao unahusu kutegemea kimakosa ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, ambayo ilikubaliwa mahakamani bila kufuata utaratibu sahihi.
Jaji Kihwelo alisema kwa kuzingatia mazingira ya shauri hilo, hawahitaji kulifanyia uchunguzi zaidi suala hilo.
“Kwa kuwa ripoti hiyo haikusomwa mahakamani kama inavyotakiwa kisheria, jambo hilo ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu za mahakama, na hivyo wameamua kuiondoa kutoka kwenye kumbukumbu rasmi za kesi hiyo,” alisema jaji.
Baada ya kuondoa ripoti hiyo, ushahidi uliobaki ni maelezo ya onyo na ya ziada, ambayo nayo yamekuwa yakilalamikiwa.
Ilielezwa kuwa maelezo ya onyo yalichukuliwa chini ya kifungu cha 58(3)(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) badala ya kifungu cha 57 cha CPA, ambacho kingepaswa kutumika katika mazingira hayo.
Jaji huyo alisema kupitia kielelezo cha tatu kilichopo kwenye ukurasa wa 146 hadi 151 wa rekodi ya rufaa, hakuna sehemu yoyote inayothibitisha kuwa ofisa wa polisi aliyerekodi maelezo ya onyo, alihakikisha kama mrufani alikuwa na uwezo wa kusoma na kuandika.
Kwa kunukuu kesi mbalimbali zilizowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufaa, Jaji Kihwelo alisisitiza kuwa kutothibitisha kuwa maelezo hayo yalisomwa na kuelekezwa kwa mrufani ni kasoro kubwa.
Alisema hitilafu hiyo ni hatari kwa kuwa utaratibu huo ulilenga kuhakikisha usahihi wa taarifa zilizorekodiwa na kuzuia uwezekano wa kuwahukumu washukiwa kwa ushahidi usio wa haki.
"Kwa kuwa upungufu huu hauwezi kurekebishwa chini ya kifungu cha 169 cha CPA, tunaamua kuondoa kielelezo cha nne kutoka kwenye kumbukumbu za kesi," alisema Jaji Kihwelo.
Kuhusu sababu ya nne ya rufaa, ilidaiwa kuwa mrufani alilazimishwa kukiri kosa baada ya kupigwa vikali na sungusungu.
Baada ya kutafakari ushahidi huo, Mahakama iliridhika kwamba upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kesi hiyo pasipo shaka yoyote.
Hatimaye, Mahakama ilihitimisha kuwa hukumu dhidi ya mrufani ilitegemea ushahidi dhaifu na usioaminika.
Kwa msingi huo, Mahakama ilikubali rufaa hiyo, ikafuta hukumu, na kuamuru kwamba mrufani aachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.