Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Ulega apangua hoja za wabunge, bajeti yapitishwa

Muktasari:

  • Asema Serikali imelipa Sh2.5 trilioni za madeni ya makandarasi tangu 2021. Licha ya kuwepo kwa madeni mapya, jitihada za malipo zinaendelea.

Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/26, huku Serikali ikisema katika kipindi cha miaka minne imelipa deni la makandarasi lenye thamani ya Sh2.5 trilioni.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema hayo leo Jumanne, Mei 6, 2025, wakati akijibu hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26.

Bunge limeidhinishia wizara hiyo Sh2.28 trilioni katika mwaka 2025/26, ambapo kati ya hizo, Sh2.18 trilioni zinakwenda katika shughuli za miradi ya maendeleo, huku Sh90.46 bilioni zikienda katika matumizi ya kawaida.

Wakati Bunge linapitisha bajeti hiyo, mwaka 2024/25, wizara hiyo ilitengewa Sh1.77 trilioni, huku Sh1.68 trilioni zikienda katika shughuli za miradi ya maendeleo.

Ulega alikuwa akiwajibu wabunge, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, iliyoeleza kuwa hadi kufikia Februari 2025, Tanroads ilikuwa na jumla ya deni lililozalishwa la Sh1.299 trilioni, ambapo kati ya deni hilo, Sh187.605 bilioni ni deni la wakandarasi na wahandisi washauri wa ndani katika miradi ya barabara kuu.

Mjumbe wa kamati hiyo, Ally Jumbe, amesema hadi kufikia Februari 2025, Tanroads ilikuwa na jumla ya deni lililozalishwa la Sh1.299 trilioni, ambapo kati ya deni hilo, Sh187.605 bilioni ni deni la wakandarasi na wahandisi washauri wa ndani katika miradi ya barabara kuu.

Jumbe amesema pia Sh974.589 bilioni ni deni la wakandarasi na wahandisi washauri wa nje, na Sh136.983 bilioni ni riba.

Amesema katika deni hilo, miradi inayoendelea ilikuwa inajumuisha jumla ya Sh507.759 bilioni, na Sh652.213 bilioni ni deni la miradi iliyokamilika.

Akijibu hoja hizo, Ulega amesema tangu mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alivyoingia madarakani, Serikali imelipa Sh2.5 trilioni kwa makandarasi.

“Kazi inaendelea na sisi sote ni mashahidi kazi kubwa ya ujenzi imekuwa ikifanyika... Hata ukitazama makandarasi wa ndani walichokuwa wakidai, na kila mwezi Wizara ya Fedha imekuwa ikitupa fedha,” amesema.

Amesema ni ukweli usiopingika kuwa bado kuna madeni yanayodaiwa, lakini jitihada za kulipa zinafanyika na makubaliano yamefanyika kati ya Wizara ya Fedha na wizara yake, na kuwa kadri wanavyozipata, ndivyo wanavyowalipa wakandarasi.

Amesema pia kuwa madeni mapya yanaendelea kuzaliwa kwa sababu kazi ya kujenga nchi inaendelea.

Kuhusu kilio cha ujenzi wa barabara, Ulega amewataka wataalamu wake kuzichukua hoja zote za wabunge na kuwahakikishia kuwa watakwenda kuzifanyia kazi, na watapata majibu kabla ya Bunge kufikia ukomo wake Juni 2025.

Kwa upande wa malipo ya awali ya makandarasi, Ulega amesema wabunge wamezungumzia kuhusu malipo ya awali ya makandarasi, wapo waliolipwa kiasi ambacho hakijafika asilimia 15 na wengine hawajalipwa.

Ulega amemtaarifu Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi kuwa barabara aliyosema hapitiki imeshatengenezwa na watu wanaendelea kupita.

Pia amesema barabara ambazo zinadaiwa malipo ya awali (advance payment), ikiwemo ya Ifakara hadi Chita na ile ya Bigwa hadi Kisaki, zitapewa kipaumbele katika malipo ya awali.

Amesema bajeti hiyo wameita kuwa ni “kazi na utu” kwa sababu inatazama zaidi kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Aidha, akitolea ufafanuzi kuhusu maombi ya kuweka taa za barabarani, Ulega amesema wamefunga taa za barabarani 5,200, ambapo kwa wastani ni taa 200 kwa kila mkoa.

Amesema taa zinaleta nuru na kupunguza ajali, na pia wanaendelea kufanya hivyo. Kuhusu michango mingine iliyotolewa na wabunge, amesema watayatolea ufafanuzi kabla ya Bunge kuvunjwa: “Lakini tumezichukua hoja zote, tunakwenda kuzifanyia kazi.”