Kisa barabara, wabunge wambana Waziri Ulega

Muktasari:
- Wabunge wamechangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka 2025/26, huku suala la ubovu wa barabara likiibuka zaidi bungeni.
Dodoma. Mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/26 umejikita katika ujenzi wa barabara, huku baadhi ya wabunge wakionyesha hofu ya kurejea bungeni katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Hofu za wabunge hao zinatokana na kile walichoeleza kwamba iwapo baadhi ya barabara majimboni kwao hazitajengwa, watakuwa katika hatihati ya kuaminiwa na wapigakura kwa sababu waliahidi.
Katika mjadala huo, mbali na sifa za utekelezwaji wa miradi hiyo, zilitolewa kauli na wabunge kuonyesha magumu wanayoyapitia wananchi wao kutokana na kutopitika kwa baadhi ya barabara, jambo linalosababisha baadhi ya wananchi kujifungulia njiani.

Jana, Jumatatu, Mei 5, 2025, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliomba Bunge limuidhinishie Sh2.28 trilioni katika mwaka 2025/26. Kati ya hizo, Sh2.18 trilioni zinakwenda katika shughuli za miradi ya maendeleo, huku Sh90.46 bilioni zikitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kiwango hicho cha bajeti ni ongezeko kutoka ile ya mwaka 2024/25, iliyokuwa Sh1.77 trilioni.
Akichangia mjadala huo bungeni, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM), Hamisi Taletale, amesema kwa miaka mitano wananchi wa jimboni kwake wamekuwa wakililia barabara ya Bigwa hadi Kisaki.
“Kaka yangu Ulega, nionee huruma. Sijaja humu ndani (bungeni) kuchangia chochote, wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki wamenitum, wanataka barabara ya Bigwa-Kisaki. Mkandarasi anataka asilimia 75 ya malipo aingie kazini. Uongozi ni kuweka rekodi, na rekodi yangu mimi ni kuhakikisha barabara hii inajengwa,” amesema.
Amemuomba Ulega kutoa majibu kuhusu lini ujenzi huo utafanyika.
“Kaka, ubunge nautaka huu, kazi naitaka hii. Wananchi wa Bigwa-Kisaki wanataka barabara. Haiwezekani miaka mitano naongea jambo moja. Hii nchi ina Rais msikivu, ametupatia kilomita 78 na ameruhusu pesa ije. Kaka yangu Ulega, shida iko wapi? Unanasa wapi? Mimi nakuona jembe kabisa, lakini hapa unanasa wapi, Ulega?” amehoji.
Mwingine aliyeibuka na hoja kama hiyo ni Mbunge wa Mkalama (CCM), Francis Mtinga, aliyetaka barabara ya kutoka Iguguno kwenda Sibiti, inayounganisha mikoa ya Simiyu, Mara na Mwanza, ijengwe.
Amesema anatamani wabunge wa mikoa hiyo waungane ili bajeti hiyo isipite hadi Serikali iseme barabara hiyo itajengwa, kwa sababu ni muhimu kiuchumi.
“Mimi ubunge bado naupenda. Wananchi wa Mkalama wameniambia wanahitaji barabara tu, nikae vipindi vingine vitatu. Niombe sana, barabara hii ni mfupa wewe waziri utafune. Nimesikitika sana kuiangalia kwenye kitabu; hakuna sehemu ambayo barabara hii imetajwa kwa umuhimu.
“Wilaya nzima ya Mkalama ina kipande tu cha kilomita mbili za lami. Sijui nifanyaje, nipige magoti tena hapa ili niweze kusikilizwa? Mimi ni kijana, bado nahitaji ubunge. Wananchi wangu wananihitaji. Naomba, nipo chini ya miguu yako,natamani kulia kwa ajili ya wananchi wa Mkalama. Zaidi ya miaka 10 inazungumzwa, na hata waliopita,” amesema.
Barabara ya Sanzanti hadi Nata pia iliingia katika mjadala huo baada ya Mbunge wa Bunda (CCM), Mwita Getere, kusema mawaziri wote wa ujenzi wamefika eneo hilo, lakini haijawahi kujengwa.
Amesema thamani ya barabara hiyo ni Sh51 bilioni na hivyo bado wanadai zaidi ya Sh44 bilioni, na kuwa watu hao wameteseka na wametoka katika ujenzi wa barabara hiyo.
“Inasikitisha sana kutengeneza barabara nzuri kama ile halafu tumeshindwa kuimaliza. Ile barabara ndiyo inayotoka Makutano, Sanzanti inaenda Mugumu, imeshindwa kukamilika. Mbuga ya Serengeti asilimia 80 ndiyo wanakaa katika mji ule wa Musoma, lakini hakuna barabara kutoka Mugumu kwenda Musoma,” amesema.
Wajifungulia njiani
Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi, amesema katika jimbo lake kuna mwananchi aliyejifungulia njiani kutokana na kukatika kwa barabara iliyopo katika eneo la Mpanga.

“Sasa hizi ni kadhia ambazo wananchi wanazipata; you can feel (unaweza ukajisikia). Sasa tangu utoke (Ulega atoke kwenye ziara mkoani Morogoro), hakuna kinachofanyika. Magari yamebaki kule kule. Hata katika eneo la Ngwasi hakuna kilichofanyika,” amesema.
Mbunge wa Kishapu (CCM), Boniface Butondo, amesema barabara ya kutoka Kolandoto, Kishapu hadi Meatu na kuunganisha na Mkoa wa Shinyanga na Arusha ni muhimu na itaharakisha maendeleo ya kiuchumi.
Amesema Wilaya ya Kishapu kwa muda mrefu inahangaika na vumbi na kuhoji kwa nini Serikali isifike mahali ikatekeleze takwa la Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Barabara hiyo, amesema ina magari mengi yanayosafirisha pamba, kunde na kwa mwaka mmoja zinatumika Sh600 milioni kufanya matengenezo.
“Imefika mahali wazazi wanajifungua barabarani kutokana na barabara kuwa na mashimo makubwa. Kwa nini tusitengeneze barabara hii?” amesema Butondo.
Washauri jinsi ya kupata fedha
Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Sospeter Muhongo, amesema kila Mtanzania ukimuuliza mahitaji yake ni huduma za maji, umeme na barabara na kwa sababu bajeti ni finyu, haiwezi kutekeleza kwa haraka.
Amesema ili kupata fedha za kutengeneza barabara, waongeze bajeti ya miradi mikubwa kwa miaka miwili inayokuja kwa kupunguza kwa asilimia 40.
“Si kama tunaisimamisha, ila tunapunguzia, kwenda kwenye barabara, umeme na maji. Pendekezo langu la pili ni kukopa kwenye benki ambazo Serikali ni wabia, na riba isiwe zaidi ya asilimia nne,” amesema.

Profesa Muhongo amesema pendekezo lake jingine ni kuzijenga barabara hizo kwa ubia wa Sekta Binafsi na Serikali (PPP), na baada ya kukamilika watumiaji watozwe fedha.
Pendekezo lingine, amesema ni kukopa nje ya nchi, jambo ambalo halikwepeki ilimradi fedha zinazopatikana zitumike kama inavyopaswa.
Mbunge huyo ameshauri utaratibu wa kutumia wakandarasi wanaotafuta fedha, wanajenga barabara na kisha Serikali inalipa taratibu (EPC+F) utumike katika kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Hata hivyo, Profesa Muhongo ametoa tahadhari kuwa kabla ya kutumia utaratibu wa EPC+F, wanatakiwa kujua kwanza gharama halisi ya ujenzi.
Nyingine ni kwenda katika soko la hisa la Dar es Salaam, ambapo kampuni zenye viwanja vya ndege zinaweza kuingia na kupata fedha za kujenga barabara.
Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, amesema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wizara ya Ujenzi wangependa kujenga barabara zote nchini, lakini ili wajenge wanahitaji fedha.

Gambo ameshauri Wizara ya Ujenzi kukaa na Wizara ya Fedha ili watoe kipaumbele cha kutosha cha fedha kwa kuwa kazi ya kusukumana na wakandarasi wafanye kazi wanaiweza.
Naye Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Musukuma, amesema barabara ya Buchosa–Sengerema hadi Nkome ni ya kimkakati na ni muhimu kujengwa kutokana na maeneo hayo ndiyo yanayoilisha Mwanza.

“Daraja la Kigongo-Busisi ni kubwa, na mimi kwa siku pale kwenye kivuko napitisha gari kama 35. Tunalipa Sh10,000 hadi 15,000; kwenye malori ni Sh80,000 hadi Sh100,000. Tuachane na bure, tuweke tozo hata ya Sh5,000,” amesema.
Bajeti hiyo itahitimishwa jioni ya leo Jumanne kwa Waziri Ulega kujibu hoja mbalimbali za wabunge walioziibua toka walipoanza kuchangia jana.