Waziri Bashe aeleza sababu ya kuwamilikisha vijana ardhi ya kilimo

Muktasari:

  • Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema Serikali imeamua kuzifanyia kazi changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili vijana na kuwafanya wasiingie kwenye sekta ya kilimo na moja ya changamoto hizo ni kukosekana kwa ardhi ya kilimo.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali imeamua kuwamilikisha vijana ardhi ya kilimo ili kuwavutia wengi kuingia kwenye sekta hiyo ili kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula Afrika.

Bashe amebainisha hayo leo Machi 20, 2023 wakati wa mjadala wa Mwananchi Twitter Space unaoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ukiwa na mada isemayo “nini kifanyike kuwezesha wanawake na vijana kulisha dunia kupitia kilimo”.

Amesema Serikali imeamua kuzifanyia kazi changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili vijana na kuwafanya wasiingie kwenye sekta ya kilimo na moja ya changamoto hizo ni kukosekana kwa ardhi ya kilimo.

“Tulifanya utafiti kujua kwanini vijana hawaendi kulima, tukabaini hawamiliki ardhi, lakini hawana teknolojia ya kisasa na hawana uhakika wa masoko.

“Vijana hawaingii kwenye kilimo kwa sababu hawana ardhi, hawapati mikopo na hawana miundombinu bora. Serikali tunajaribu kuwekeza kwenye maeneo hayo,” amesema Waziri Bashe.

Kuhusu kuwa na sheria ya kilimo, Bashe amesema ni kweli kama nchi hakuna sheria ya kilimo lakini mchakato umeshaanza ili kuwa na sheria ya kilimo. Hata hivyo, amesema zipo sheria nyingine za mazao.

Amesema miaka ya nyuma, miradi mingi ya sekta ya kilimo iliyogeuka kuwa “white elephant” (isiyo na faida) kwa sababu ya changamoto ya usimamizi.

“Mimi ninajiamini kwamba miradi hii tunayoianzisha haitageuka kuwa white elephant, vijana hawa ambao tunawaingia kwenye kilimo, wengi wao wanatoka kwenye familia za wakulima,” amesema Bashe.

Waziri huyo amesema vijana wanamaliza masomo yao ya vyuo kikuu lakini hawana ardhi ya kulima. Kwa hiyo, kwa hiyo, amesema wanawamilikisha ardhi ili wafanye kilimo na kuwajengea uwezo.

“Kuna vijana wameacha kazi kwenye taasisi wanaenda kwenye taasisi, wanakwenda kwenye kilimo. Wanaamini kwamba mshahara wa Sh300, 000 hautakidhi ndoto zao, nao wanataka siku moja waajiri watu na fursa pekee wanaiona kwenye kilimo,” amesema.