‘Sekta binafsi ishiriki mapinduzi ya kilimo Tanzania’

Muktasari:

  • Kilimo kinachangia asilimia 26.1 ya pato la Taifa na kinaajiri takribani asilimia 60 ya Watanzania.

Dar es Salaam. Mhariri wa Habari msaidizi wa gazeti la The Citizen, Louis Kolumbia amesema sasa kuna haja ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha kuja pamoja katika kuhakikisha kwamba kilimo kinakuwa mkombozi wa Watanzania.

Kolumbia amebainisha hayo leo Machi 20, 2023 wakati wa mjadala wa Mwananchi Twitter Space unaoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ukiwa na mada isemayo “nini kifanyike kuwezesha wanawake na vijana kulisha dunia kupitia kilimo”.

Amesema utafiti wa ufuatiliaji wa kaya unaonyesha kwamba sekta ya kilimo imechangia asilimia 26.1 kwenye pato la taifa. Amesema nchini Tanzania, sekta ya kilimo imeajiri takribani asilimia 60 ikifuatiwa na sekta ya huduma.

Amebainisha kwamba vijana na wanawake ni kipaumbele kwa sababu matokeo ya sensa ya mwaka 2022 inaonyesha kwamba idadi ya watu ni milioni 61 ambapo kati yao watu milioni 31 ni wanawake. Hivyo, amesema wanawake ni jeshi kubwa katika sekta ya uzalishaji hususani kilimo.

“Kundi la wanawake na vijana ni kundi kubwa ambalo kama halitatafutiwa mikakati ya ajira, haliwezi kuleta tija ile inayokusudiwa.

“Tunatarajia kuona serikali ikiwekeza zaidi kwenye sekta hii, tunahitaji kuona sekta binafsi ikishiriki katika jambo hili na sekta binafsi nayo ikiweka mkono wake ili kufanikisha kilimo hiki,” amesema Kolumbia.

Kolumbia ambaye pia ni mwandishi wa kilimo, amesema takwimu zinaonyesha kwamba vijana 800,000 wamekuwa wakiingia kwenye soko la ajira huku asilimia 10 pekee wakiajiriwa kwenye sekta ya umma wakati watu 700,000 wakiangukia sekta binafsi.

“Sasa tunatarajia kuopna vijana wakihama kutoka mijini kwenda vijijini,” amesema Kolumbia wakati akizungumza kwenye mjadala huo.