Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wauza pombe Moshi wapewa onyo

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Godfrey Mnzava, akizungumza na watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji, maofisa maendeleo ya jamii na maofisa ugani wa Kata ya Njiapanda, mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, wakati akifunga kikao kazi kilichowakutanisha viongozi hao kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo na utendaji.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amewataka watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji katika Kata ya Njiapanda, mji mdogo wa Himo, kuhakikisha wanadhibiti uuzaji wa pombe wakati wa saa za kazi akisema  hatua hiyo inalenga kuongeza uwajibikaji wa kazi katika maeneo yao.

Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amepiga marufuku wamiliki wa baa wilayani humo kuuza vileo kabla ya saa 9:30 alasiri, akieleza kuwa watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria.

Mbali na agizo hilo, amewataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika msako unaoendelea dhidi ya watengenezaji wa pombe haramu aina ya gongo, akisema biashara hiyo inachangia kuharibika kwa maadili na kupunguza uzalishaji katika jamii.

Mnzava ametoa kauli hiyo leo wakati akifunga kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji, maofisa maendeleo ya jamii na maofisa ugani katika Kata ya Njiapanda, mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi.

Amesema Kamati ya Usalama ya Wilaya imeamua kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo inayodhibiti uuzaji wa vileo.

"Kwa niaba ya Kamati ya Usalama ya Wilaya, ni marufuku kwa wamiliki wa baa au muuzaji yeyote wa vileo kufungua baa, kuuza pombe au kukusanya watu kwa ajili ya unywaji wa pombe kabla ya saa 9:30 alasiri, kama sheria inavyoelekeza," amesema Mnzava.

Amewataka wamiliki wote wa baa kuhakikisha wanafuata muda uliowekwa kisheria, akisisitiza kuwa uuzaji wa pombe nje ya utaratibu hautavumiliwa.

Pia, amewaagiza watendaji wa kata, watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji na Polisi Kata kusimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo na kuchukua hatua dhidi ya watakaokiuka sheria.

Kuhusu pombe haramu, Mnzava amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako dhidi ya watengenezaji wa gongo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahusika.

"Watengenezaji wa pombe haramu wapo katika maeneo yetu. Tupeni ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi ili waweze kuwakamata," amesema Mnzava.

Amesema  kuwa matumizi holela ya pombe, hususan kwa vijana wakati wa saa za kazi, yanaathiri maendeleo ya jamii na kuongeza changamoto katika kijamii.

"Hatuwezi kuwa na jamii ambayo vijana wake kuanzia asubuhi hadi mchana hawafanyi kazi kwa sababu ya ulevi. Haiwezekani viongozi tuliopewa dhamana tukayaangalia haya yakiendelea," amesema DC Mnzava.

Amesema: "Hakuna kuogopa, kwa sababu wanaotengeneza pombe hizi haramu hawana nia njema na jamii yetu. Watendaji lazima tusimame kwenye nafasi zetu na kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, Neema Festo amesema anaunga mkoni agizo hilo la mkuu wa wikaya hiyo kwa kuwa vijana wengi wamekuwa ni walevi muda wa saa za kazi.

"Ninaunga mkono uamuzi wa mkuu wa wilaya kwa sababu unywaji wa pombe mapema umekuwa ukiathiri uzalishaji katika jamii zetu. Watu wanapaswa kufanya kazi kwanza, halafu kunywa pombe wakati unaoruhusiwa sasa matokeo yake vijana wetu wamekuwa wakilewa kuanzia asubuhi hadi jioni," amesema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, Joshua Swai, ambaye pia ni dereva bodaboda amesema: "Kama sheria itasimamiwa kwa usawa itasaidia kupunguza ulevi kwenye maeneo yetu, maana unywaji wa pombe kiholela huku kwetu umezidi."