Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wauza gongo Moshi wadaiwa kushirikiana kuwakabili polisi

Muktasari:

  • Wazalishaji wa pombe haramu ya gongo kata za Kilema Kaskazini, Kati na Kusini wilayani hapa Mkoa wa Kilimanjaro, wamedaiwa kuanzisha umoja wa kuchangishana fedha ili kusaidiana endapo mmoja atakamatwa na polisi.

Moshi. Wazalishaji wa pombe haramu ya gongo kata za Kilema Kaskazini, Kati na Kusini wilayani hapa Mkoa wa Kilimanjaro, wamedaiwa kuanzisha umoja wa kuchangishana fedha ili kusaidiana endapo mmoja atakamatwa na polisi.

Fedha hizo hutumika kuwekeana dhamana polisi au mahakamani jambo lililotajwa na polisi kuwa, ni kikwazo katika vita dhidi ya biashara hiyo.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Moshi, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi, mrakibu mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Pili Misungwi, alidai kuwa umoja huo umeathiri juhudi za jeshi hilo za kutokomeza pombe haramu ya gongo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wilaya imeendelea kushamiri vitendo vya unywaji wa gongo huku wazalishaji wakiuza kwa kiwango kikubwa hadi kufikia hatua ya kusafirisha nchi jirani ya Kenya.

“Sheria bado hazina makali kwa mtu anayekamatwa akinywa au akiuza pombe hiyo; kata za Kilema Kusini na Kilema Kaskazini ndizo zinazoonekana kuzalisha kwa wingi na nyingine ikisafirishwa kwenda nchi jirani ya Kenya,” alisema Misungwi

Pia, alisema operesheni ya hivi karibuni katika Kata ya Kilema Kusini walikamata mapipa 300 ya pombe hiyo na baada ya hapo, siku tisa baadaye walikamata mapipa 80.

“ Kata ya Kilema Kusini ndipo kuna mitambo ya utengenezwaji wa pombe hiyo haramu ya gongo na tunapoenda kukamata viongozi wa vijiji huwa wanalalamika kwa nini hatuwapi taarifa, hiki ni kiashiria kuwa wao wanashiriki au kulea biashara hiyo haramu,” alisema Misungwi.

Diwani wa Kilema Kaskazini, Anna Lyimo alisema kutokana na kushamiri kwa unywaji wa gongo kwenye kata yake, vitendo vya ukatili vimeshamiri pamoja kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa ambao ni vijana.

Diwani wa Kilema Kati, Selisi Mosha alisema kutokana na kukithiri kwa pombe haramu, miradi mingi ya Serikali inayohitaji nguvu ya wananchi ili ifanyike haitawezekana tena kutokana na vijana wengi kuishiwa nguvu kwa unywaji wa gongo.

Alisema jitihada za Serikali za kujenga vyumba vya madarasa katika kata yake, zinaweza kuwa kazi bure kutokana na baadaye kukosa wanafunzi kwa sababu ya unywaji wa gongo.

Mwenyekiti wa Halmashuri ya Moshi, Moris Makoi alilitaka Jeshi la Polisi kujipanga upya ili kuondoa tatizo hilo ambalo limeonekana kuleta madhara.

Pia, alilitaka kuchukua hatua kali kwa wanaoendelea kuzalisha pombe hiyo.