Dk Tulia ataja fedha za mashindano kuboresha miundombinu ya elimu, afya

Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson akiwa kwenye picha ya pamoja ya washiriki wa mbio za watoto kwenye mashindano yaliyofanyika leo jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Mbio hizo zimeanza kutimua kivumbi leo Mei 9 na kuhitimishwa kesho Mei10, 2025 katika viwanja vya kumbukumbu ya Sokoine, huku mgeni akitarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko.
Mbeya. Spika wa Bunge na Mbunge Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ameweka bayana fedha za ushiriki wa mbio za mashindano ya ‘Betika Tulia Marathon 2025’ zitatumika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu, afya na ujenzi makazi ya wazee.
Mbali na kauli hiyo, Dk Tulia ameng'ara na kushika nafasi ya kwanza katika mbio za uwanjani za mita 100 kwa kushika nafasi ya pili kwenye mbio za watoto za mita 50.
Awali akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 9, 2025 baada kuzindua na kushiriki mashindano hayo, Dk Tulia amesema huu ni msimu wa tisa na kujivunia mwamko mkubwa wa washiriki wa ndani na nje ya nchi.
"Kwa msimu huu, tumeboresha kwa kuongeza ushiriki wa mbio za watoto zenye lengo kwa kuibua vipaji na kuviendeleza,"amesema.
Amesema ushiriki wa watoto utawajenga uwezo wa kuwa wanariadha wakubwa jambo ambalo ni matarajio makubwa ya mashindano ya "Betika Tulia Marathon 2025," ambayo yameanza kutimua kivumbi leo Ijumaa Mei 9,2025 na kuhitimishwa Mei 10, 2025 .
Amesema mbali na kuibua vipaji, Taasisi ya Tulia Trust imeweke mikakati ya kuwepo kwa mashindano hayo kila mwaka na kushirikisha wadau ili kuunga mkono jitihada za serikali kuwekeza kwenye sekta ya elimu afya sambamba na wahitaji wengine.
"Kupitia mashindano ya Tulia Marathon misimu iliyopita tumefanya mambo mengi hususani kuboresha miundombinu ya chumba cha upasuaji katika kituo cha afya Ruanda, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike na ujenzi wa makazi ya wazee wasiojiweza," amesema.
Mratibu wa mashindano "Betika Tulia Marathon 2025", Lwiza John amesema kwa sasa wameanza na mbio za awali za uwanjani lakini kesho Mei 10,2025 , zitaanza rasmi mbio za barabarani kuanzia kilometa 42.
"Mashindano haya yana sehemu mbili, mbio za uwanjani ambazo zimeanza leo Mei 9, 2025 ,lakini kesho tunaanza mbio za barabarani kuanzia kilometa 42, tuombe wadau kuchangia zaidi mbio za uwanjani msimu ujao ili kuibua vipaji hususani kwa watoto," amesema.
Lwiza amesema miongoni mbio zilizofanyika ni kuanzia mita 1,500- 800-400-200-100 ,kwa wanawake na wanaume, huku mbio za mita 50 zimeshirikisha watoto walio na umri kuanzia miaka mitano na kuendelea.
"Msimu ujao tunatarajia kuongeza ushiriki wa michezo ya kurusha kitufe, mkuki na mingine mingi, licha ya msimu huu kuendelea kupata maombi ya ushiriki katika mikoa mbalimbali nchini," amesema.
Wakati huohuo, Lwiza ametoa wito kwa wazazi kutoa fursa kwa watoto kushiriki mashindano ya mbio za uwanjani ili kuibua vipaji na kuviendeleza.
Mmoja wa washiriki aliyeshika nafasi ya kwanza katika mbio za watoto, Diana John (6), amemshukuru Dk Tulia kwa kuandaa mashindano ya "Betika Tulia Marathon 2025".
"Mimi ni miongoni mwa watoto ambao tuliingia kwenye mashindano ya mbio za mita 50, nilipomuona Spika nilikuwa na hofu, lakini nikijivisha ujasiri, kuondoa hofu na hatimaye kuwa mshindi wa kwanza hilo linanipa moyo kwa msimu ujayo ntafanya vizuri zaidi,"amesema.