Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasomi watakiwa kubuni teknolojia za kupunguza upotevu wa mazao

Mhadhili msaidizi kutoka Taasisi ya taaluma na maendeleo ya chuo kikuu Mzumbe, Emmanuel Zephania (katikati) akitoa maelezo ya namna mmea za azolla anavyoweza kutumika kama mbolea kwa zao la mpunga, maelekezo hayo ameyatoa kwa wananchi kwenye kambi ya wanafunzi wajasiriamali wa chuo hicho. Picha Hamida Shariff, Mwananchi

Muktasari:

  • Serikali imeeleza kuwa katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu na upotevu wa mazao, hususan mboga za majani na matunda, imeandaa mpango madhubuti wa kuhakikisha kuwa kila kijiji kinapata majengo ya kisasa yenye uwezo wa kuhifadhi mazao kwa kutumia mifumo ya baridi (cold room).

Morogoro. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema licha ya Serikali kuweka fedha nyingi katika miradi ya kilimo, bado kuna changamoto ya uharibifu na upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.

Kigahe amesisitiza kuwa vijana wasomi wanapaswa kuendeleza na kubuni teknolojia zitakazosaidia kupunguza changamoto hiyo.

Kigahe aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wabunifu, wajasiriamali, wahadhiri, na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe waliohudhuria kambi ya wajasiriamali iliyoandaliwa na chuo hicho, kwa lengo la kuonyesha na kuendeleza bunifu na shughuli za ujasiriamali.

Katika hotuba yake, ameeleza kuwa Serikali inatekeleza mpango wa kujenga majengo ya kuhifadhia mazao, yenye uwezo wa kutunza baridi (cold rooms), katika kila kijiji, ili kupunguza upotevu unaotokana na kuharibika mazao ya mbogamboga na matunda.

"Mpango huu wa kujenga majengo haya ya kuhifadhia baridi utaweza kupunguza upotevu wa mazao, lakini pia ni muhimu vijana wasomi waendelee kubuni bunifu zitakazoongeza thamani ya mazao hayo," amesema Kigahe.

Amesema Wizara ya Viwanda na Biashara, wanatoa kipaumbele kwa bunifu zitakazoweza kusaidia kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Kigahe ambaye alikwenda kumwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, pia alitoa wito kwa vijana waliomaliza masomo katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kutumia ujuzi wao katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kutoa chachu kwa wanafunzi wa sasa.

Amesema kwamba zamani chuo hicho kilikuwa kikitoa elimu ya uongozi, utawala, na sheria, lakini sasa kinatoa fursa kwa wanafunzi kufanya tafiti na kubuni teknolojia mpya.

Katika hatua nyingine, Mhadhiri Msaidizi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Emmanuel Zephania, amesema kuwa wasomi wa chuo hicho wamefanya utafiti wa mmea wa Azolla, ambao unasaidia kupunguza hewa ya kaboni inayochangia mabadiliko ya tabia nchi.

Utafiti huo pia umebaini kuwa mmea huo hutengeneza asidi ya nitrojeni inayoweza kutumika kama mbolea kwa mazao ya mpunga, hivyo kusaidia kuongeza tija katika kilimo.

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Shadrack Mofulu amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kubadili mtazamo wao kutoka kwenye mawazo ya kusoma ili kupata ajira, na badala yake watumie elimu yao kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.

Mofulu ambaye ni mtaalamu wa sheria, ameelezea mafanikio yake ya kujiajiri baada ya kumaliza masomo, akianzia na kazi ya uanasheria na sasa akiwa na kampuni yake ya utalii.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Hawa Tundui amesema kuwa kambi ya wajasiriamali ni sehemu muhimu ya mafunzo ya wanafunzi wa chuo hicho.

Amesema kuwa kambi hii ya wajasiriamali imekuwa ikifanyika kwa miaka nane sasa, ikilenga kuwasaidia wanafunzi kuonyesha ubunifu na mawazo yao katika sekta ya ujasiriamali, na hivyo kuendelea kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.