Watoto wawili wafariki wakidaiwa kula chakuka chenye sumu

Muktasari:
- Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia na mmoja pamoja na mama yao wamenusurika baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu.
Tabora. Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia na mmoja pamoja na mama yao wamenusurika baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 15, 2022 mjini Tabora, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika kijiji cha Ngukumo Wilaya ya Nzega.
Amesema wanafamilia wakiongozwa na mama yao, Janeth Jeremia (48) walikula ugali na dagaa na kuanza kupata maumivu ya tumbo.
Kamanda Abwao ameeleza kuwa maumivu ya tumbo yalipelekea watoto wawili Sadick Mustafa (3) na Laurencia Nassoro (4) kufariki dunia wakati mama yao na mtoto mwingine Lucia Maprosi (8) wakinusurika.
"Mama wa wa watoto hao pamoja na mtoto mwingine, wanaendelea na matibabu katika kituo cha afya cha Busondo na hali zao zinaendelea vizuri"amesema
Kamanda Abwao ameeleza kuwa wamechukua sampuli kwa ajili ya kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini kama ni kweli kulikuwa na sumu kwenye chakula hicho.
Amesema wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na hadi sasa hakuna mtu yoyote aliyekamatwa.