Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya 'Bwana harusi' yachukua sura mpya

Mshtakiwa Vicent Masawe (aliyevaa kofia) akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi ya wizi wa gari inayomkabili kuahirishwa leo Jumanne Januari 7, 2025. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Masawe katika kesi hiyo anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo wizi wa gari aliloazimwa kwa matumizi siku ya harusi yake.

Dar es Salaam. Serikali imeeleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa imepokea barua kutoka kwa mlalamikaji katika kesi ya wizi wa gari inayomkabili 'Bwana harusi' Vicent Masawe (36), kuwa anaomba kuiondoa kesi hiyo mahakamani hapo.

Mlalamikaji katika kesi hiyo, Sylivester Masawe amewasilisha ombi hilo, akiomba shauri la kesi hiyo liondolewe mahakamani hapo.

Masawe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni wizi wa gari aina ya Toyota Ractis lenye thamani ya Sh15 milioni ambalo aliazimwa kwa ajili ya kulitumia katika sherehe ya harusi yake na kujipatia fedha taslimu Sh3 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali, Aron Titus ameieleza Mahakama hiyo, leo Jumanne, Aprili 29, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali (PH).

Titus ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, anayesikiliza kesi hiyo.

"Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa yupo mbele ya mahakama yako na kesi imeitwa kwa ajili ya kumsomea hoja za awali," amedai wakili Titus na kuongeza

"Lakini hatutaweza kumsomea kwa sababu tumepokea maombi kutoka kwa mlalamikaji katika kesi hii akiomba kuliondoa shauri hili, hivyo tunaomba Mahakama itupe wiki moja ili tuweze kufuatilia na kusubiri taratibu rasmi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS)," amedai Titus.

Wakili Titus baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alinyoosha mkono juu na alipopewa nafasi na Mahakama alidai kuwa anaomba mlalamikaji apewe gari yake.

"Mheshimiwa hakimu nilikuwa naiomba Mahakama yako tukufu, kuwa Sylvester apewe ile gari yake kwa sababu inaendelea kuharibika, ipo tu pale Polisi," alidai mshtakiwa.

Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza taarifa ya upande wa mashtaka, alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 6, 2025.

Itakumbukwa Aprili 14, 2025, mshtakiwa huyo alieleza Mahakama wamekaa na familia wanataka kufuta kesi kwani mmiliki wa gari hilo ni baba yake ndogo ambaye ndiye aliyemlea, hivyo baba yake huyo ndogo aliandika barua kwenda polisi kuomba kufuta kesi hiyo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 35738/2024, Massawe anadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 15, 2025 kinyume na vifungu  namba 258 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa mara ya kwanza Massawe alifikishwa mahakamani Desemba 24, 2024 na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Katika shtaka la kwanza la wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa kuwa akiwa wakala, tarehe hiyo  Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari lenye namba za usajili T 642 EGU aina ya Toyota Ractis.

Gari hilo lenye thamani ya Sh15 milioni, kwa mujibu wa upande wa mashtaka ni mali ya Silvester Masawe.

Anadaiwa aliazimwa gari hilo na Silvester kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake lakini baada ya hapo, hakurudisha gari kama ambavyo walikubaliana.

Katika shtaka la pili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa kuwa tarehe hiyohiyo ya tukio Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh 3 milioni kutoka kwa Silvester.

Anadaiwa alijipatia fedha hizo kwa kuahidi kuwa atamrudisha fedha hizo baadaye, wakati akijua kuwa ni uongo na hakuweza kurudisha fedha hizo hadi alipokamatwa.

Kabla ya kukamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es Salaam alidaiwa kupotea.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Novemba 18, 2024 Massawe ambaye alikuwa fungate baada ya kufungua ndoa, alitoa taarifa kwa marafiki zake kuwa alikuwa Mbezi na kwamba alikuwa anafuatiliwa na gari ambalo alikuwa halijui.

Tangu siku hiyo, hakuonekana wala kupatikana kwenye simu zake.

Hata hivyo, Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa za kukamatwa kwake.

Kamanda Muliro alisema Massawe alikamatwa Desemba 15, 2024, akiwa kwa mganga wa kienyeji, Pemba na kwamba alikuwa na tuhuma za wizi wa kuamimiwa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Alieleza kuwa kutoka na tuhuma hizo ndio maana alitengeneza mazingira ya uongo kwamba amepotea kisha akaenda kujificha kwa mganga huyo wa kienyeji.

Hata hivyo alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo, Massawe alikana kutenda makosa hayo, na aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana aliyopewa.