Huyu ndiye Rosalynn Mkurugenzi mpya wa Mwananchi

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia.
Muktasari:
- Rosalynn Mndolwa-Mworia amechukua wadhifa huo ambao kabla ya uteuzi wake ilikuwa ikikaimiwa na Victor Mushi aliyekuwa Mhariri Mtendaji Mkuu.
Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ambayo ni kampuni tanzu ya Nation Media Group (NMG), imetangaza uteuzi wa Rosalynn Mndolwa-Mworia kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa MCL.
Rosalynn mwenye uzoefu wa miaka 23 wa kuziongoza sekta za mawasiliano ya simu, usafirishaji, huduma za kifedha na bima, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bakari Machumu aliyestaafu kwa hiari Agosti 2024, baada ya kuitumikia nafasi hiyo tangu Julai 2020.
Machumu alijiunga na MCL mwaka 2004 na aliitumikia kampuni kwa nafasi mbalimbali kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji.
MCL inasimamia usafirishaji wa mizigo (Mwananchi Currier), uchapishaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen na mtandao wa kidijitali wa Mwanaclick.
Rosalynn amechukua wadhifa huo ambao kabla ya uteuzi wake ulikuwa ikikaimiwa na Victor Mushi aliyekuwa Mhariri Mtendaji Mkuu.
Taarifa ya uteuzi wa Rosalynn katika nafasi hiyo, imetolewa leo Jumanne Aprili 29, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, David Nchimbi alipozungumza katika kikao kilichoihusisha Bodi ya NMG na wafanyakazi wa MCL jijini Dar es Salaam.
Sambamba na taarifa ya kuteuliwa kwa Rosalynn, Bodi ya NMG pia imemtangaza Mushi kuwa Mhariri Mtendaji wa Ubunifu wa Kidijitali NMG, akiwa na jukumu la kuongoza mikakati ya usambazaji wa maudhui ya kidijitali na ushiriki wa hadhira katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Katika historia ya MCL, Rosalynn anakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, tangu kampuni hiyo ilipoanzishwa Mei, 1999.
Kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi huo iliyotolewa kwa umma leo, inaeleza hilo linafanyika katika kipindi ambacho MCL ipo kwenye safari ya mageuzi makubwa, yenye lengo la kuwa jukwaa bora la maudhui kwa njia ya kidijitali.
Rosalynn ni mbobevu katika ngazi za juu za uendeshaji wa biashara, akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 23 katika sekta za mawasiliano ya simu, usafirishaji na vifaa, huduma za kifedha na bima.
“Uwezo wake mkubwa katika mawasiliano ya kimkakati, usimamizi wa wadau na kukuza taasisi kwa ujumla unatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika kuharakisha dhamira ya MCL ya kuwahudumia Watanzania kwa habari zenye kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha,” imeeleza taarifa ya bodi ya MCL.
Taarifa hiyo, inaeleza mkurugenzi huyo mpya atasimamia shughuli zote za kampuni, huku akiongoza mkakati wa mageuzi ya kidijitali kwa nguvu mpya.
“Ataelekeza nguvu zake katika kukuza uwezo wa kidijitali wa kampuni, kupanua wigo wa biashara ya sasa na kuingia katika maeneo mapya yanayochipua ndani ya mazingira mapya ya vyombo vya habari.
“Uteuzi wa Rosalynn ni hatua kubwa katika safari yetu ya mageuzi. Ana uwezo uliothibitishwa katika kuongoza mikakati, kuendeleza ubunifu wa kidijitali, kujenga utamaduni wa kumjali mteja na kuhakikisha ukuaji endelevu wa biashara. Ana nafasi ya kipekee ya kuipeleka MCL katika hatua inayofuata ya mafanikio,” amesema Nchimbi.
Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya NMG na MCL kuwekeza kwa watu wake na kuhakikisha kuwa vipaji vinatumiwa ipasavyo ndani ya kundi la vyombo vya habari linaloongoza Afrika Mashariki.
Huyu ndiye Rosalynn
Kabla ya kuteuliwa kuiongoza MCL, Rosalynn ni Mkurugenzi na mwanzilishi wa Inspire Ventures Ltd.
Amewahi kuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Mahusiano wa Kampuni ya Vodacome PLC na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Foundation.
Mbali na nyadhifa hizo, pia amewahi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Mauzo cha kampuni ya kimataifa ya Maersk Line.
Mbali na uzoefu wa uongozi wa biashara, pia amejikita katika huduma kwa jamii. Ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Assemble Insurance Tanzania.
Pia, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Malipo na Marupurupu. Pia, amewahi kuwa mjumbe wa bodi katika Kitengo cha Hifadhi za Bahari cha Serikali na katika Shirika la Railway Children Africa.
Rosalynn ni muhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Biashara na Shahada ya Sayansi katika Uhasibu na Mifumo ya Taarifa za Usimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Wayne State College, Marekani.
Pia, ni Mkufunzi wa Uongozi mwenye cheti cha kimataifa kutoka Academy of Executive Coaching (AoEC).
Rosalynn anafahamika kwa weledi wake katika uongozi wa kimkakati, mawasiliano ya shirika na uwezo wa kuvuka mipaka ya sekta mbalimbali kwa ufanisi mkubwa.
Ujuzi wake katika kuoanisha biashara, teknolojia na vyombo vya habari unampa msingi imara wa kuongoza MCL kuelekea mustakabali wa mafanikio makubwa.